Na Mussa Yusuph,
Lindi
KIMBUNGA cha Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, kimeendelea kushika kasi kwa kusambaratisha ngome mbalimbali za vyama vya upinzani mkoani Lindi.
Hali hiyo imeendelea kudhihirika katika mikutano ya kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu, ambapo vigogo kutoka vyama hivyo, waliamua kujiunga CCM, huku wakieleza kuguswa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na mazuri yaliyopo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2025–2030).
katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi, wanachama kutoka vyama vya CHADEMA, CHAUMMA na CUF wamerejesha kadi za vyama hivyo kisha kupokelewa CCM mbele ya Mwenyekiti wa Chama Taifa, Dk. Samia.
Akizungumza katika mkutano huo, aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Lindi na Makamu Mwenyekiti Kanda ya Kusini, Salum Bar’wan, alisema ameguswa na Ilani ya CCM 2025–2030, ikiwemo dhamira ya kuufungua Mkoa wa Lindi kupitia uboreshaji wa miundombinu ya barabara, ujenzi wa uwanja wa ndege na utekelezaji mradi wa kimkakati wa gesi asilia (LNG).
Alisema ameamua kujiunga CCM kwa sababu kimeonesha dira ya maendeleo ya kweli, huku akiwataka wananchi wa Lindi kujitokeza kwa wingi kumpa kura Dk. Samia.
Naye, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mchinga kupitia CHAUMMA, Yusuph Issa Tamba, alisema amefikia uamuzi huo kwa ridhaa yake mwenyewe bila kushawishiwa na mtu yeyote.
“Natuma salamu kwa chama changu wametuma ujumbe wa vitisho, waambieni mimi siyo mtoto mdogo, sitishiki. Huku ndiyo nyumbani, mitano tena. Nimerudi nyumbani, naomba mnipokee,” alisema.
Tamba aliahidi kushirikiana na CCM kuhakikisha ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 na kuwataka wananchi wa Mchinga na Mkoa wa Lindi kwa ujumla kuunga mkono maendeleo yanayoletwa na Dk. Samia.