Na MUSSA YUSUPH,
Musoma
MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema mkakati wa serikali katika miaka mitano ijayo ni kuendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Musoma Mjini mkoani Mara, Dk. Samia alisema kipaumbele cha serikali ni kuimarisha maisha ya wananchi.
“Kwa upande wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, serikali inakuja na mradi wa kujenga stendi na masoko nchi nzima kutoa fursa kwa wafanyabiashara ndogondogo.
“Kupitia mfuko wa halmashauri wa asilimia 10 ambao tumeugawa kwa makundi ya wanawake, vijana na wenye ulemavu nayo hiyo ni fursa nyingine ya kuwezesha wananchi kiuchumi,” alisema.
Alisisitiza: “Hivyo kijana jipange ujue unataka kufanya biashara gani, stendi tunajenga, masoko tunajenga, mifuko ya kukuwezesha ipo hivyo sema unataka kufanya biashara gani?
“Kubwa zaidi tumesema katika ilani mpya tunakwenda kurasimisha biashara ndogondogo zitambulike, ziwe rasmi mfaidike sawa na wafanyabiashara wengine.”
Dk. Samia alisema katika kuwawezesha wananchi, serikali pia imekuja na mfumo wa ruzuku katika kilimo na pembejeo.
Alisema serikali inaendeleza mkakati wa kilimo cha umwagiliaji kwa kujenga skimu na mabwawa huku upande wa uvuvi imefanya mengi zaidi ikiwemo ufugaji samaki kwa mabwawa na vizimba.