Na MWANDISHI WETU
KIKAO maalumu cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), kikiongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kimefanyika leo Novemba 5, 2025 jijini Dodoma.
Hiki ni kikao cha kwanza cha Kamati Kuu kufanyika tangu kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Katika kikao hicho, viongozi wametathmini mazingira ya kisiasa kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Kamati Kuu imewapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kuonesha imani kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kipindi cha uchaguzi.
Aidha, chama kimekemea na kulaani vikali vitendo vya uvunjifu wa amani na uharibifu wa mali uliyofanywa na baadhi ya watu.
Vilevile, CCM imeazimia kuendelea kujitathmini na kujiimarisha ili kuliongoza taifa kwa ufanisi, sambamba na kuitaka Serikali kuchukua hatua stahiki kuhakikisha nchi inabaki kuwa ya amani na utulivu.




