Na NASRA KITANA
ZIKIWA zimesalia siku 38 kumalizika kwa mwaka 2025 na kuukaribisha mwaka 2026, Tanzania imepata heshima kubwa kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutunukiwa tuzo kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kutokana na mchango mkubwa katika maendeleo ya soka hapa nchini.
Tuzo hiyo ilitolewa kwa Rais Dk. Samia kutokana na kutambua kazi kubwa iliyofanywa katika kipindi cha uongozi wake na kufanya Tanzania kuendelea kupanda zaidi katika viwango vya michezo duniani.
Novemba 19, mwaka huu Rais wa CAF, Patrice Motsepe, alimtunuku tuzo Rais Dk. Samia katika hafla ya utoaji tuzo iliyofanyika mjini Rabat nchini Morocco huku ikipokelewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa.
Motsepe aliwapa tuzo hiyo, Rais wa Uganda, Yoweri Museven na Rais wa Kenya, William Ruto.
Baada ya kupokea tuzo hiyo, Msigwa alisema kuwa Serikali ya Tanzania inaahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa CAF na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), katika kuhakikisha mchezo wa soka unapiga hatua zaidi nchini.
Alisema serikali itaendelea kufanya uboreshaji na kujenga viwanja vya michezo nchini ikiwemo kuendeleza programu ya soka la vijana kwa wanawake na wanaume ili kuweza kushiriki katika michezo kila kukicha.
“Kwanza tunashukuru kwa tuzo hii mliotupatia na sapoti kubwa ambayo mmeendelea kutupa kuhakikisha tunaendeleza soka nchini, sisi tunaahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa CAF na FIFA ili kuhakikisha mchezo wa soka unapiga hatua zaidi,’’ alisema Msigwa.
Ndani ya miaka mine iliyopita, Rais Dk.Samia amejipambanua kuwa mdau mkubwa wa sekta ya michezo kwa ushiriki wake katika shughuli mbalimbali za sekta hiyo pamoja na mipango iliyowekwa na uongozi wake wa kuhakikisha michezo inapiga hatua na hivi sasa kila kitu kimeonekana kwa vitendo na siyo maneno.
Ushiriki huo wa Rais Dk.Samia katika michezo umeonekana kujenga imani ya wengi kuwa huenda sekta ya michezo ikapata mafanikio makubwa chini ya utawala wake kama imani ilivyo katika sekta nyingine.
Ipo mifano na uthibitisho wa wazi unaoonyesha jinsi Rais Dk. Samia anavyotamani kuona michezo siyo tu inakuwepo kwa ajili ya kujifurahisha bali kugeuka fursa ya ajira na kukuza uchumi wa nchi.
MWENYEJI WA CHAN
Kwanza Tanzania kuweza kuwa mwenyeji katika mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2024) iliyofanyika kuanzia Agosti 2 hadi 30, mwaka huu na Tanzania kuishia hatua ya robo fainali ya mashindano hayo huku Morocco ikitwaa ubingwa huo.
Tanzania ilikuwa mwenyeji ikishirikiana na Kenya na Uganda huku ikiwekwa historia kwa mara ya kwanza kufanyita Afrika Mashariki.
UJENZI, UKARABATI VIWANJA
Wakati utawala wa Rais Dk. Samia unaingia madarakani, uliahidi utatenga bajeti ya fedha kwa ajili ya kusaidia uboreshaji wa viwanja vya soka vilivyoonekana kuwa na uchakavu na tayari hilo limeshaanza kufanyika kwa vitendo ikiwemo kujenga viwanja vipya.
Kana kwamba haitoshi, uongozi wa Rais Dk.Samia umeahidi ujenzi wa viwanja viwili vya kisasa vya soka katika miji ya Dodoma na Arusha vilivyoanza ujenzi wake vikitarajiwa kutumika katika fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
AFCON 2027
Uongozi wa Rais Dk. Samia ulianzisha wazo la kuomba kuandaa fainali za AFCON zitakazofanyika mwaka 2027 ambapo itashirikiana na nchi za Kenya na Uganda.
Rais Dk. Samia kwa nafasi yake alifanikiwa kuwashawishi Rais wa Kenya, Ruto na Rais wa Uganda, Museveni ambao waliridhia wazo la kuandaa kwa pamoja mashindano hayo na kuwaagiza mawaziri wa michezo wa nchi zao, kukutana ili kuandaa mkakati wa kuhakikisha maombi ya kuandaa fainali hizo yaliyopewa jina la ‘Pamoja Bid’ yanapata ushindi katika kinyang’anyiro hicho.
GOLI LA MAMA
Utawala wa Rais Dk. Samia mwaka 2022, ulianzisha utaratibu wa kuzipa hamasa klabu za Tanzania zilizokuwa zinashiriki mashindano ya Afrika likipewa jina kama ‘Goli la Mama’ kwa kutoa kiasi cha sh. milioni tano kwa kila bao ambalo timu hizo zilikuwa zinafunga kuanzia makundi huku hatua za mbele dau hilo likiongezeka.
Hamasa hiyo ya fedha za ‘Goli la Mama’ ambazo Rais Dk. Samia alikuwa anatoa ilichangia kwa kiasi kikubwa kuzipa morali Simba na Yanga, ambazo zilijitutumua na kufika hatua za juu za mashindano hayo, kumbuka katika utawala wa wake timu hizo zote zimekuwa na mafanikio makubwa zaidi kwa soka, Yanga ikifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2022-2023 sawa na Simba 2024-2025.
Katika kipindi hiki cha Rais Dk. Samia, kutokana na sapoti ambayo amekuwa akiitoa katika timu imeonekana kuleta chachu, ambapo Tanzania imeandika historia ya kuingiza kwa mara ya kwanza timu mbili kwa mpigo hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu mmoja nyuma.
SOKA LA WANAWAKE CECAFA
Agosti 21, 2021, Rais Dk. Samia alikubali ombi la Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), la kuwa mdhamini wa Mashindano ya Wanawake ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Mashindano hayo yalifanyika katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na kuifanikisha Tanzania kuchukua ubingwa wa CECAFA 2025.
SAMIA NA STARS
Rais Dk. Samia amejipambanua kuwa mwanamichezo hodari na kiongozi anayetaka kuona timu ya taifa, Taifa Stars inafanya vizuri na kupata mafanikio, mwaka jana aliongoza harambee maalumu ya kuzichangia timu za taifa za michezo mbalimbali ili kuziwezesha kuwa na ushiriki mzuri katika mashindano ya kimataifa.
Katika kipindi cha uongozi wa Rais Dk. Samia, Stars imekuwa inaonyesha kiwango kizuri pale wanapokwenda kushindana na timu za mataifa mbalimbali yote ni kutokana na chachu aliyoionyesha.
MZIZE NAYE ANG’ARA TUZO ZA CAF 2025
Wakati huo huo, Rais Dk. Samia akiwa ametunukiwa tuzo hiyo ya heshima CAF mshambuliaji wa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Clement Mzize ameshinda Tuzo ya Bao Bora la Mwaka 2025.
Mzize ameshinda tuzo hiyo kutokana na bao alilofunga msimu wa 2024-2025 hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe wakati Yanga ikishinda mabao 3-1 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Januari 4, 2025.
Akizungumza kuhusu tuzo hiyo, Mzize alisema kuwa ni chachu kwake na imemwongezea thamani kubwa katika kazi yake ya soka na ataendelea kupambana ili kuweza kuonyesha ubora zaidi.

Alisema anawashukuru wachezaji wenzake kwa ushirikiano mkubwa waliompatia, benchi la ufundi pamoja na uongozi mzima wa klabu yake kwani tuzo hiyo ni ya kwao wote.
‘’Tuzo hiyo imeniongezea thamani kubwa katika kazi yangu ya soka na kunipa morari ya kupambana zaidi, niwashukuru wote walionipigia kura, CAF, wachezaji wezangu, benchi la ufundi pamoja na uongozi mzima wa timu yangu,’’ alisema Mzize.
BMT, TFF WADAU WA SOKA NCHINI WATOA NENO
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia alisema kuwa tuzo hiyo kubwa ni heshima kwa Tanzania kwani itaongeza chachu ya kukua kwa soka hapa nchini.
‘’Nifurahi kuona tuzo hiyo kwenda kwa Rais wetu Dk. Samia kwani anastahili kuipata, aliyoyafanya ni makubwa na anaimani ataendelea kufanya mengi zaidi kwa ajili ya maendeleo ya soka hapa nchini,’’ alisema Karia.
Uongozi wa Baraza la Michezo Taifa (BMT), chini ya Katibu Mtendaji Neema Msitha, limempongeza Rais Dk.Samia kwa tuzo hiyo kwani inaonyesha ni jinsi gani mchango mkubwa alioufanya katika michezo unaonekana Afrika nzima.
Alisema tuzo hiyo imetolewa kutokana na kazi kubwa iliyofanywa katika kipindi cha uongozi wake ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo viwanja vikubwa, kuwa wenyeji wa mashindano ya CHAN 2024 na maandalizi ya AFCON 2027 pamoja na mafanikio makubwa katika mashindano ya kimataifa.
“Kwanza niipongeze CAF kumtunuku tuzo kubwa Rais Dk. Samia kutokana na mafanikio aliyoyapata katika michezo katika kipindi cha uongozi wake, hii bora kwetu na imetuongezea kasi ya kufanya vyema zaidi,’’ alisema Msitha.
Naye mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Ally Mayay alisema kuwa ni hatua kubwa kwa Rais Dk. Samia kutunukiwa tuzo hiyo kubwa hiyo inaonyesha jinsi gani kwa hivi sasa Tanzania imeendelea kisoka.
“Ni furaha kwetu kwa Rais Dk. Samia kutunikiwa tuzo hiyo na hapo ndiyo inaonyesha jinsi gani tumeendelea kisoka na kutambulika duniani hivyo tuendelee na kasi ya kufanya vizuri kuanzia ngazi za klabu na timu zetu za taifa,’’ alisema Mayay.
Naye nyota wa zamani wa Simba na Yanga, Zamoyoni Mogella alisema kuwa amefurahi kuona Tanzania imepiga hatua kubwa katika soka na hadi kupata tuzo za CAF pia kutambua mchango mkubwa kwa Rais Dk. Samia.
“Hii ni ya thamani sana kwetu, mpira kwa hivi sasa umekuwa na Rais Dk.Samia amechangia kwa kiasi kikubwa tunaona timu zetu za Simba na Yanga zikifanya vziuri kimataifa lakini timu ya taifa pia kuwa wenyeji wa mashindano makubwa kiukweli tunatakiwa kujivunia katika hilo,’’ alisema Mogella.
Hafla hiyo iliyofanyika jijini Rabat nchini Morrocco ilihudhuriwa na Rais wa TFF na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF, Wallace Karia pamoja na Mwenyekiti wa Klabu Barani Afrika na Rais wa Yanga, Hersi Said.




