Na ELIZBAETH JOHN
MAANDALIZI ya ujenzi wa njia za treni za mijini katika majiji ya Dar es Salaam na Dodoma yameanza rasmi, hatua inayotarajiwa kubadili kwa kiasi kikubwa mfumo wa usafiri wa abiria na kupunguza msongamano wa magari.
Akizungumza Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji wa Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema treni hizo zitakuwa za juu na zitaunganishwa na mtandao wa Reli ya Kisasa ya SGR.
Alisema katika jiji la Dar es Salaam, awamu ya kwanza ya ujenzi itahusisha njia itakayoanzia Kawe, Mwenge, Mlimani City, Ubungo hadi Kariakoo, ambako mtandao utaunganishwa na SGR.
Aidha, kutakuwepo na tawi jingine kutoka Bibi Titi, Morocco kupitia Barabara ya Ali Hassan Mwinyi hadi Mwenge.
Alisema serikali imepanga kila baada ya kilometa mbili kuwe na kituo, lengo likiwa ni kujenga mtandao wa kilometa 160 utakaobadili mfumo wa usafiri jijini Dar es Salaam.
“Kwa upande wa Dodoma, serikali imepanga kuanza na njia itakayotoka stesheni ya SGR kuelekea katikati ya jiji, kuendelea hadi Mtumba na Chamwino kupitia stendi mpya ya mabasi.
“Awamu inayofuata itafika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, huku mtandao mzima ukitarajiwa kuwa wa angalau kilometa 105,” alisema.
Msigwa alisema Tanzania inaendelea kusonga mbele kwa kasi katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo SGR ambayo imeendelea kuwavutia wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali.
Alisema kazi ya ujenzi wa SGR inaendelea vizuri katika vipande vyote vinane, kutoka Dar es Salaam, Dodoma, Tabora, Isaka, Mwanza, Kigoma hadi Burundi, huku miradi mipya ya reli ikiongezeka ukiwemo ujenzi wa reli ya Tanga-Arusha-Musoma yenye kilometa 1,028 na reli ya Mtwara-Mbambabay yenye kilometa 1,000 kwa ajili ya kusafirisha mizigo kutoka Bahari ya Hindi hadi nchi za kusini.
Alisema katika sekta ya bandari, serikali imeeleza kuongezeka kwa ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam maradufu kufuatia ushirikiano wa kimkakati na kampuni ya DP World, hatua iliyosaidia kupunguza muda wa meli kusubiri kutoka siku 46 hadi saba.
“Uwezo wa bandari hiyo kuhudumia mizigo umeongezeka kutoka tani milioni 21 hadi tani milioni 32 ndani ya miaka mitatu, huku mapato yakipanda kutoka sh. bilioni 900 hadi sh. trilioni 1.8.
“Serikali inaendelea kuboresha Bandari za Mtwara, Tanga, Kigoma, Bagamoyo na zile za Ziwa Tanganyika, ukiwemo uzinduzi wa meli mpya ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 2,000 kati ya meli nne zinazojengwa kuimarisha usafiri na biashara kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na masoko mengine ya ukanda huo,” alisisitiza.
Pia, katika sekta ya utalii, Msigwa alisema Tanzania imevuka lengo lake baada ya kupokea watalii milioni 5.3 mwishoni mwa mwaka jana, idadi ambayo awali ilipangwa kufikiwa mwaka huu. Serikali inalenga kufikia watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030.
Kwa upande wa usafiri wa anga, alisema serikali imeimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ambalo hivi sasa lina ndege 16 na linahudumia vituo 29 vya ndani na nje ya nchi.
“Ndege nane zaidi zinatarajiwa kuongezwa kufikisha jumla 24 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, huku vituo vipya vya Cape Town (Afrika Kusini), Accra (Ghana) na Victoria Falls (Zimbabwe), vikitarajiwa kuongezwa na kufikia mwaka 2030, malengo ni ATCL kuhudumia vituo 50 ndani na nje ya nchi,” alisema Msigwa.
Msemaji huyo aliongeza uchumi wa taifa unaendelea kukua kwa wastani wa asilimia sita na kwamba akiba ya fedha za kigeni imefikia dola bilioni saba za Marekani.
“Serikali inatarajia kuongeza ajira kupitia miradi yote ya kimkakati inayotekelezwa nchini, ikiwemo ya reli, bandari na sekta ya utalii,” alisema Msigwa.




