Na SIMON NYALOBI
KATIBU Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amekitaka kituo cha runinga cha kimataifa cha CNN, kuzingatia weledi wa uandishi wa habari katika kuripoti habari zake.
Msigwa alisema hayo alipozungumza na vyombo vya habari kuhusu mambo yanayoendelea nchini baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.
Alisema kituo hicho cha runinga cha nchini Marekani kimeripoti taarifa za matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29, mwaka huu, bila kufuata misingi ya uandishi wa habari wa kupata pande zote, huku kikisingizia kutopewa ushirikiano upande wa serikali ya Tanzania.
“Chombo hiki (CNN) kimefanya makosa ya uweledi katika uandishi wa habari kwa kuchapisha na kutangaza maudhui yaliyoegemea upande mmoja, siyo kweli CNN ilishindwa kuupata upande wa serikali kwa ripoti zao zote wanazozitoa,” alisema.
Msigwa alisema kutokana na ripoti hiyo, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na viongozi wa serikali wamesikitishwa na upotoshaji wa kutangaza taarifa za matukio hayo.
Alisema CNN imepewa nafasi kufuata upande wa serikali kwa nia ya kupata ukweli wa matukio hayo ya Oktoba 29, mwaka huu.
Hata hivyo, alisema taarifa za takwimu za vifo na uharibifu wa mali zilizoharibiwa katika vurugu hizo, zitatolewa na Kamati ya Uchunguzi wa Matukio hayo iliyoundwa na Rais Dk. Samia, pindi itakapomaliza kazi yake.
Kamati hiyo imepewa siku 90 kukamilisha jukumu ililokabidhiwa.
Aidha, Msigwa alishauri iwapo kuna chombo cha habari kilichofanya uchunguzi wa matukio hayo, kipeleke taarifa katika tume hiyo iliyoundwa na Rais Dk. Samia, ambayo ina mamlaka ya kutoa ripoti baada ya kukamilisha kazi yake.
TAARIFA ZA MTANDAONI
Msemaji huyo wa serikali, pia alikanusha maudhui yaliyotengenezwa katika mtandao wa kijamii yanayodai Rais Dk. Samia, ameagiza mmoja ya waandishi wa habari wa kimataifa nchini ashitakiwe kwa kesi ya uhaini.
Alisema taarifa hizo hazina ukweli na badala yake, alirejea kauli ya Rais Dk. Samia, kwamba malalamiko yote yatasikilizwa na kutafutiwa ufumbuzi.
Vilevile, Msigwa alisema anashangazwa na baadhi ya wanaharakati kutoa takwimu za vifo kutokana na matukio ya Oktoba 29, mwaka huu, kwa sababu haijulikani njia walizotumia kupata takwimu hizo.
VYOMBO VYA HABARI NCHINI
Akizungumzia utendaji kazi wa vyombo vya habari vya nchini, Msigwa alivipongeza vyombo hivyo kwa kufanya uandishi wa habari wa uwajibikaji katika kazi yao.
Alisema vyombo hivyo vimeripoti taarifa zake kwa kujali maslahi ya nchi kwa kuhakikisha amani inaendelea kuwepo nchini.
“Historia itawatambua waandishi wa Tanzania, hatuhitaji kusifiwa na mtu wa nje, waandishi msihofu mnaposimamia maslahi ya taifa na mnapofanya uandishi wa uwajibikaji,” alieleza Msigwa.
Aidha, msemaji huyo wa serikali alibainisha serikali inatarajia kuanzisha Mfuko wa Waandishi wa Habari utakaowasaidia wanahabari kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.
WATANZANIA WASHAURIWA
Pamoja na hayo, Msigwa aliwasihi Watanzania kujiepusha na taarifa za uchochezi na baadhi ya watu wasioitakia mema nchi hususan wanaotoka nje ya nchi.
“Tusiendelee kusikiliza taarifa za uchochezi kutoka kwa watu wanaotoka nje ya nchi, kwa sababu tunaoumia ni sisi wenyewe na hata katika tukio la Oktoba 29, mwaka huu, tulioumia ni si wenyewe,” alisema.
Alifafanua wanaofanya uchochezi wanatumia silaha ya simulizi mbaya za kuonesha nchi si salama na haifai kwa kupata maslahi ya kisiasa na kiuchumi.
Aliweka wazi lengo kubwa la wachochezi hao kuona miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa kasi nchini inakwama kisha nchi iporomoke kiuchumi.
“Lengo lao kuona watalii hawafiki nchini hali itakayowafanya wanufaika wa mnyororo wa thamani katika sekta hiyo wakiwemo madereva na mama lishe waathirike,” alifafanua Msigwa.
Aliwataka wananchi kuwauliza wachochezi kutoka nje ya nchi, wanapodai haki katika nchi zao kama huwa wanafanya hivyo kwa njia za kuchoma vituo vya mafuta au magari.
VIONGOZI WA DINI, WATALII
Kwa upande mwingine, Msigwa aliwasisitiza viongozi wa dini na siasa, kuepuka kauli za uchochezi zitakazowagawa wananchi huku akisema serikali imeanza kuzungumza na viongozi hao kuhusu suala hilo.
Alitumia fursa hiyo kuwakaribisha watalii kuendelea kuja nchini, kwani kuna hali ya usalama na amani tofauti na taarifa za upotoshaji zinazoandikwa mitandaoni.
Msigwa alieleza watalii wanaweza kutembelea vivutio na mbuga zikiwemo za Serengeti, Mlima Kilimanjaro na kwingineko ambako usalama umetamalaki.
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa serikali, vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha wakati wote nchi inakuwa na ulinzi na usalama na kulinda mali za wananchi.




