• ePaper
Friday, May 8, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home Makala

KIPIGO, KUNYIMWA UNYUMBA UKATILI MPYA KWA WANAUME

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
January 4, 2026
in Makala
0
KIPIGO, KUNYIMWA UNYUMBA UKATILI MPYA KWA WANAUME
0
SHARES
26
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

>Kiongozi wa chama cha kutetea wanaume atoa ushuhuda, aeleza kwa kina machungu

Na ATHNATH MKIRAMWENI

KWA miaka mingi, jamii imezoea kusikia simulizi za wanawake na watoto wanaonyanyaswa nyumbani, lakini nyuma ya pazia hilo kuna kundi jingine la wanaume linateseka kimya kimya, wakiwa wamefungwa na aibu, hofu na mitazamo hasi ya kijamii.

Baadhi ya wanaume wamekuwa wakipigwa, kudhalilishwa na kunyimwa haki zao za msingi likiwemo tendo la ndoa ndani ya ndoa zao lakini, hawathubutu kusema chochote.

USHUHUDA

Huu ni ukweli mchungu uliomsukuma Ernest Komba, mwanaume aliyepitia mateso ya ukatili wa nyumbani kwa zaidi ya miaka mitatu, kuamua kuvunja ukimya.

Kupitia kipigo, udhalilishaji wa kisaikolojia, kunyimwa haki ya ndoa na hata kumwagiwa maji ya moto, Komba aliyakimbia maisha yake kuokoa uhai wake, kabla ya kugundua kuwa mateso yake hayakuwa ya kwake peke yake.

Kutokana na maumivu hayo, Komba ambaye kwa hivi sasa ni Mwenyekiti wa Shirika la Wanaume wanaopitia changamoto kwenye ndoa na rais wa wanaume wanaopigwa na wake zao, alisema aliamua kuanzisha shirika hilo, baada ya kubaini kuwa hakuna taasisi, wala sauti ya wazi kuwatetea wanaume wanaoteswa ndani ya ndoa.

 “Mimi binafsi katika kipindi cha ndoa yangu nilipitia changamoto nyingi, zikiwemo kupigwa makofi mara kwa mara, kunyimwa maneno ya faraja na kubezwa kwa jitihada zangu za kiuchumi niliposhindwa kurejea nyumbani na fedha,”alisema.

Kwa mujibu Komba, hata majukumu ya kifamilia yaligeuzwa chanzo cha migogoro, ikiwemo kupingwa kwa uamuzi mdogo kama kununua nguo za mtoto, licha ya mtoto mwenyewe kuzithamini.

Akizungumza zaidi na gazeti hili, Komba alisema ilifikia hatua ya hatari zaidi baada ya kukumbwa na vitendo vya ukatili wa kimwili, ikiwemo kumwagiwa maji ya moto kwa hasira na kuvunjiwa mali za nyumbani hali iliyomlazimu kukimbia nyumbani kuokoa maisha yake.

Baada ya kurejea kwa lengo la kumuangalia mtoto, Komba alisema changamoto zilezile ziliendelea, jambo lililomfanya kutafakari iwapo wanaume wengine nao wanapitia mateso kama hayo.

Kupitia dawati la jinsia na ziara mikoani, alikutana na wanaume waliopitia vitisho, kunyimwa haki, unyanyasaji wa kimwili na kisaikolojia, huku wengine wakidai hata kuwekewa sumu lakini wote wakiwa hawana mahali pa kukimbilia au kuripoti kwa uhuru.

Kutokana na hali hiyo, waliwasilisha hoja zao Manispaa ya Kigamboni, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, hatua iliyowezesha kuanzishwa rasmi kwa shirika hilo la wanaume.

CHANZO, HOFU YA WANAUME

Kupitia ziara zake mikoani, Komba alisema changamoto kubwa iliyobainika ni suala la kiuchumi, ambalo wanawake huwezeshwa kupitia mikopo bila kuwashirikisha waume zao, hali inayochochea migogoro ya ndoa.

Alitoa mfano wa mkoani Morogoro, ambako baadhi ya wanawake huanzisha biashara au kujenga nyumba bila wenza wao kujua, hali inayosababisha migogoro mikubwa na wakati mwingine kuvunjika kwa ndoa.

Komba alisema eneo la Bukoba, ilibainika kuwa ingawa dawati la jinsia lipo, wanaume wengi hawaripoti ukatili wanaoupitia kutokana na hofu na mila, jambo linalowafanya kubeba maumivu moyoni.

Komba alisema bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii inayotenga zaidi ya sh.bilioni 70 inalenga zaidi kuwawezesha wanawake na watoto, huku wanaume wakiachwa bila msaada wa kiuchumi, kiafya na kisaikolojia.

Aliongeza kuwa wanaume wenye umri wa kuanzia miaka 45 hawaruhusiwi kupata mikopo ya serikali, hali inayowaacha nyuma kiuchumi wakati nguvu za kufanya kazi zikiwa zimepungua.

Kutokana na hali hiyo, Shirika hilo, limeiomba serikali kuanzisha idara maalumu ndani ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii itakayoshughulikia masuala ya wanaume, kuhakikisha usawa, ustawi wa familia na kupunguza migogoro ya ndoa.

Shirika hilo kwa hivi sasa limeenea katika mikoa kadhaa ukiwemo Dar es Salaam, Morogoro, Bukoba, Manyara, Singida na Dodoma, likiwa na mamia ya wanaume waliokwisha jiunga rasmi.

DAWATI LA JINSIA

Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limethibitisha kuwa ukatili dhidi ya wanaume ni changamoto halisi ya kijamii inayojitokeza kwa kasi, hasa ndani ya ndoa na uhusiano wa kifamilia.

Kaimu Mkuu wa Dawati hilo, Inspekta wa Polisi, Mudathiru Makora, alisema kwa muda mrefu wanaume walikuwa hawajitokezi kuripoti ukatili kutokana na mtazamo hasi uliokuwepo kuhusu dawati la jinsia, ambalo awali lilijulikana kama dawati la wanawake na watoto.

Hali hiyo iliwafanya wanaume kuona ugumu wa kwenda kutoa taarifa wakihofia kutotendewa haki au kudharauliwa.

Changamoto hiyo iliongezeka kutokana na ukweli kwamba, zaidi ya asilimia 90 ya watendaji wa dawati hilo hapo awali walikuwa wanawake, hali iliyozua hofu kwa wanaume waliokuwa wahanga wa ukatili ndani ya ndoa au uhusiano.

Kutokana na mazingira hayo, wanaume wengi walichagua kunyamaza na kubeba maumivu yao kimya kimya.

Makora alisema Jeshi la Polisi lilitambua changamoto hiyo mapema na kufanya maboresho kwa kubadilisha jina na mwelekeo wa dawati hilo na kulifanya kuwa Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto, kuondoa hisia za ubaguzi na kuonyesha wazi kuwa linahudumia jinsia zote.

Alifafanua kuwa, dhana ya jinsia inawahusisha wanaume, wanawake na watoto na kwamba ukatili hauchagui jinsia.

Kwa msingi huo, dawati la jinsia linashughulikia matendo yote ya ukatili bila kujali kama mhanga ni mwanaume au mwanamke.

Makora alisema ukatili unaotambuliwa na dawati hilo upo katika aina kuu tano ambazo ni ukatili wa kimwili, kisaikolojia, kiuchumi, kingono na ukatili wa kimtandao. Aina hizo zote zinaweza kumkumba mwanaume ndani au nje ya ndoa.

Alieleza kuwa, kwa upande wa wanaume, ukatili unaoongoza zaidi ni wa kimwili na wa kisaikolojia. Katika ukatili wa kimwili, kuna matukio ya wanaume kupigwa na wake zao, jambo ambalo limekuwa likiripotiwa katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na hata mikoa mingine nchini.

Makora alitaja mfano wa Kigamboni, ambako kuna chama maalumu cha wanaume wanaodai kunyanyaswa au kupigwa na wake zao, hali inayothibitisha kuwa jamii yenyewe tayari imetambua uwepo wa tatizo hilo na kuanza kutafuta njia za kujisaidia.

Kwa upande wa ukatili wa kisaikolojia, alisema huu ni ukatili unaoathiri kwa kina utu na heshima ya mwanaume. Ukatili huu unajumuisha matusi, kejeli, kudhalilishwa mbele ya watu, kunyimwa heshima na kunyimwa haki za msingi ndani ya ndoa.

Aliongeza kuwa, mabadiliko ya hali ya uchumi katika familia yamekuwa chanzo kikubwa cha ukatili wa kisaikolojia, hasa pale mwanamke anapokuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kifedha kuliko mume wake, hali inayosababisha baadhi ya wanawake kushusha heshima ya waume zao.

Alisema wanaume wanaokumbwa na ukatili wa kisaikolojia hupoteza kujiamini, hupata msongo mkubwa wa mawazo na kushindwa kushiriki kikamilifu katika majukumu ya kifamilia na kijamii, hali inayohatarisha ustawi wa familia nzima.

Makora alionya kuwa, migogoro ya ndoa isiyoshughulikiwa vizuri inaweza kusababisha madhara mapana zaidi katika jamii, ikiwemo kuathiri malezi ya watoto na kuibua matendo mengine ya ukatili dhidi ya makundi dhaifu.

Alieleza kuwa dawati la jinsia lina watendaji waliopata mafunzo maalumu ya kisaikolojia, ustawi wa jamii na masuala ya kisheria, hivyo wanaume wanaojitokeza kuripoti ukatili hupokelewa na kuhudumiwa kwa weledi na usiri.

Hata hivyo, alisema bado kuna idadi kubwa ya wanaume wanaoendelea kunyamaza kutokana na aibu, hofu ya jamii au kutokujua mahali pa kupata msaada, jambo linalofanya baadhi ya matukio kubaki gizani.

Makora alisema jeshi la polisi limeongeza juhudi za utoaji elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari, shule, vyuo, maeneo ya mikusanyiko na kushirikiana na viongozi wa dini, hatua iliyoongeza uelewa na idadi ya wanaume wanaojitokeza kutoa taarifa.

Akizungumzia suala la sheria, alisema adhabu kwa makosa ya ukatili haibagui jinsia na kwamba mwanaume au mwanamke akibainika kufanya ukatili, huchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za jinai zilizopo.

Alisisitiza kuwa, hakuna ushindi katika ukatili wa kifamilia, kwani wote wanaohusika huathirika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, ikiwemo watoto na jamii kwa ujumla.

Makora alitoa wito kwa wanaume wanaofanyiwa vitendo vya ukatili kuacha kunyamaza, kujitokeza kutoa taarifa katika madawati ya jinsia yaliyopo katika vituo vya polisi, akisisitiza ukatili ni uhalifu unaodhalilisha utu wa binadamu na lazima ukomeshwe kwa ushirikiano wa jamii nzima.

MWANASAIKOLOJIA

Kwa upande wake, Mwanasaikolojia kutoka Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Mbeya, Daniely Mbuwi aliibua taswira halisi ya mateso wanayopitia baadhi ya wanaume katika jamii, akieleza wamekuwa wakiishi katika maumivu makubwa ya kisaikolojia bila msaada, hali inayochangia ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza, matumizi ya pombe kupita kiasi na changamoto kubwa za afya ya akili.

Mbuwi alisema jamii imejenga dhana kwamba mwanaume ni kiumbe imara asiye na haki ya kulia, kuonyesha udhaifu au kuomba msaada, jambo ambalo kitaalamu ni mfumo kandamizi unaomuumiza mwanaume kisaikolojia.

Alisema katika tamaduni nyingi, mwanaume huaminika kuwa “hateseki”, hasa anapokuwa ameoa, hali inayofanya jamii ipuuze kabisa mateso yake hata anapopitia manyanyaso makali ndani ya ndoa au uhusiano.

Kutokana na mtazamo huo, wanaume wengi hushindwa kufunguka au kuripoti ukatili wanaofanyiwa na wake zao, kwa kuhofia kubezwa, kudharauliwa au kutochukuliwa kwa uzito na jamii pamoja na vyombo husika.

Mtaalamu huyo alisema ni nadra kumuona mwanaume akienda polisi au kwa mtaalamu wa saikolojia kusema ananyanyaswa,kupigwa au kudhulumiwa na mwenza wake, si kwa sababu mambo hayo hayatokei, bali kwa sababu ya aibu na mifumo ya kijamii iliyomjenga mwanaume kuvumilia kimya kimya.

Kubeba maumivu kwa muda mrefu bila msaada husababisha msongo mkubwa wa mawazo, huzuni ya kudumu (sonona), wasiwasi, kukosa usingizi na kupoteza furaha ya maisha.

Alisema hali hiyo huwafanya wanaume wengi kutafuta nafuu ya muda kupitia matumizi ya pombe, sigara, bangi na dawa nyingine za kulevya kama njia ya kuficha maumivu na kujipa ujasiri wa muda.

Matumizi hayo hatarishi huja na madhara makubwa ya kiafya, ikiwemo kupata magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, kisukari na matatizo mengine ya mwili yanayotokana na msongo wa mawazo wa muda mrefu.

Mwanasaikolojia huyo aliongeza kuwa, matatizo ya kisaikolojia kwa wanaume pia yanachangia changamoto pana za kijamii, ikiwemo idadi kubwa ya wanaume waliopo magerezani, wanaojihusisha na ukatili na vifo vinavyotokea bila jamii kujiuliza chanzo chake.

Alisema hali hiyo inaweza kueleza kwa nini kuna idadi kubwa ya wanawake wajane kuliko wanaume wagane, kwani wanaume wengi hufariki wakiwa wamebeba mzigo mkubwa wa kisaikolojia bila msaada wa kitaalamu.

Mtaalamu huyo aligusia pia suala la uwezeshaji wa kijamii na kiuchumi, akisema katika miaka ya hivi karibuni nguvu kubwa imeelekezwa kumwezesha mwanamke, huku mwanaume akisahaulika, jambo linalowaacha baadhi ya wanaume wakipoteza mwelekeo na uthabiti wa maisha.

Kwa mujibu wake, mwanaume anayejikuta hana nafasi ya kujieleza, hana msaada wa kihisia na anakandamizwa kijamii huingia kwenye hali ya kujiona duni na kukosa thamani, hali inayozidisha matatizo badala ya kuyatatua.

Mbuwi alitoa wito kwa jamii kubadili mtazamo hasi dhidi ya mwanaume anayefunguka, kulia au kuomba msaada na kutambua kuwa mwanaume pia, ni binadamu mwenye hisia na mahitaji ya kisaikolojia kama wengine.

Aidha, alizitaka taasisi za haki, vyombo vya usalama na huduma za kijamii kuwapa wanaume heshima na kipaumbele wanapowasilisha malalamiko yao, kujenga jamii yenye usawa wa kweli.

Kwa upande wa wanaume, mwanasaikolojia huyo amewahimiza kutathmini afya ya akili, kufunguka kwa watu wanaowaamini na kuwatafuta wataalamu wa saikolojia waliopo hospitalini na katika jamii, akisisitiza kuwa kuomba msaada sio udhaifu bali ni hatua ya ujasiri.

Alisema utu na afya ya akili ya mwanaume ni nguzo muhimu ya familia na taifa na kwamba jamii ikianza kumthamini na kumsaidia mwanaume, itapunguza magonjwa yasiyoambukiza, ukatili na misukosuko mingi ya kijamii inayoshuhudiwa sasa.

WALICHOSEMA VIONGOZI WA DINI

Kwa upande wake, Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini Kiongozi wa kijamii Kilaini alisema wanaume wengi waliopo kwenye ndoa wanapitia ukatili wa kimwili na kisaikolojia kimya kimya kwa hofu ya aibu na kuhukumiwa na jamii.

Alisema wanaume hao hawatoi taarifa kwa viongozi wa dini, serikali wala marafiki, hali inayowafanya kubeba maumivu moyoni kwa muda mrefu na hatimaye kupata magonjwa kama shinikizo la damu, kisukari na msongo wa mawazo, huku wengine wakifariki mapema.

Kilaini alionya kwa muda mrefu jamii imejikita zaidi katika kusaidia wanawake waliodhulumiwa, jambo ambalo ni la haki, lakini bila kujua imewaacha wanaume wengi nyuma bila mifumo ya msaada.

Alisisitiza kuwa, ukatili hauna jinsia na kwamba mwanaume anaponyanyaswa kisaikolojia au kimwili, madhara yake huathiri familia nzima, watoto na hata usalama wa jamii kwa ujumla.

Askofu Kilaini alitoa wito kwa jamii, viongozi wa dini na serikali kufungua mjadala wa wazi na kuanzisha maeneo salama ya ushauri kwa wanaume waweze kuzungumza kwa heshima na faragha.

Kiongozi huyo alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuzuia migogoro ya kifamilia, mauaji ya hasira na kurejesha amani inayopaswa kuanzia ndani ya familia.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Shekhe Khamisi Mataka alisema mwanamke kumzidi kipato mwanaume imekuwa changamoto kubwa ya unyanyasaji ndani ya ndoa.

Alisema wanapata kesi nyingi za uhusiano kwa wanawake kutotimiza wajibu wao ndani ya ndoa na changamoyo hizo husababisha wazazi hao kutengana na kuwaacha watoto kulelelewa na mzazi mmoja.

Alisema mtoto kulelewa na mzazi mmoja huku akiwa ameshazoea kulelewa na wazazi wawili, inakuwa changamoto hivyo aliwashauri wazazi kusikilizana na kuheshimiana bila ya kujali vipato vyao kwa lengo la kulea watoto wao katika mazingira mazuri.

Mhadhiri Mwandamizi wa masuala ya Uchumi na Uongozi kutoka Chuo cha Mwalimu Nyerere, Dk. Philip Daninga aliwataka wanaume wasikubali kukaa kimya wanaponyanyaswa, kwa sababu hofu na aibu ni mtazamo wa mfumo dume zimefanya wanaume wengi kushindwa kutafuta msaada.

Jambo hilo linasababisha msongo wa mawazo na kuathiri afyua zao, ikiwemo vifo vya mapema na kuacha familia katika changamoto .

Alisisitiza kuwepo kwa madawati ya jinsia ni fursa kwa wanaume kama ilivyo kwa wanawake, madawati hayo yameanzishwa kutoa msaada wa kisheria, ushauri na suluhu ya migogoro ya kifamilia .

Dk. Daninga alitoa wito kwa wanaume kuacha hofu na kuyatumia madawati hayo kupata msaada mapema, badala ya kubaki na matatizo moyoni yanayoweza kuharibu afya na familia zao.

KAULI YA WIZARA

Hivi karibuni, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Dorothy Gwajima, alisema ukatili unaoendelea kushuhudiwa katika jamii kwa kiasi kikubwa unatokana na mila, desturi na mitazamo kandamizi inayorithishwa kizazi hadi kizazi bila kupitiwa upya.

Pia, alisema mapambano dhidi ya ukatili si jukumu la serikali au wizara pekee, bali ni la jamii nzima.

Dk. Dorothy alisisitiza mkakati wa pamoja kwa kuwahimiza wananchi kutokaa kimya wanapoona dalili za ukatili,bali kutumia mifumo iliyopo kutoa taarifa mapema. Alisema mapambano dhidi ya ukatili yanahitaji mabadiliko ya fikra, mapitio ya mila na desturi, na ujasiri wa jamii kusema “hapana” pale haki za binadamu zinapokiukwa.

“Mikakati ya kupambana na ukatili ni mipana kuliko serikali au wizara moja. Ni wajibu wetu sote kama jamii,” alisisitiza.

Previous Post

SARE ZA SHULE ZISIWE KIKWAZO – MARC

Next Post

TANZANIA ILIVYOWEKA HISTORIA AFCON 2025

Next Post
TANZANIA ILIVYOWEKA HISTORIA AFCON 2025

TANZANIA ILIVYOWEKA HISTORIA AFCON 2025

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

MRADI WA BILIONI 18.9/- BUKOBA WAMPA SIFA RAIS DK. SAMIA

MRADI WA BILIONI 18.9/- BUKOBA WAMPA SIFA RAIS DK. SAMIA

1 month ago
YANGA YATAMBIA REKODI LIGI KUU

YANGA YATAMBIA REKODI LIGI KUU

1 month ago

Popular News

  • YANGA MBELE KWA MBELE

    YANGA MBELE KWA MBELE

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • WATAALAMU WAFUNGUKA MITAZAMO YA MIKATABA 8

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • RAIS DK. SAMIA AKEMEA VIONGOZI ‘KUVIMBA’

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • DEMOKRASIA ISIZICHAFUE NCHI ZETU – RAIS DK. SAMIA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • ZIARA YA RAIS KAGAME, RUTO KUIMARISHA DIPLOMASIA KIUCHUMI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?