RABAT, Morocco
WAKATI michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), ikitarajiwa kuanza kesho nchini Morocco, timu saba zinaingia michuano hiyo zikiwa na rekodi tofauti.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari imeeleza kwamba timu hizo zinashiriki AFCON na baadaye baadhi yake zitashiriki fainali za Kombe la Dunia.
Mataifa saba kati ya tisa ya Afrika ambayo tayari yamefuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani, yatashiriki AFCON 2025 huko Morocco na kuongeza ushindani katika michuano hiyo.
Mataifa hayo ni Morocco, Misri, Tunisia, Algeria, Afrika Kusini, Senegal na Ivory Coast ambayo yametajwa kuwa na ushindani mkubwa kuwania taji hilo.
Katika fainali hizo za AFCON 2025 timu za Ghana na Cape Verde zinakosa michuano hiyo Afrika ingawa zimefuzu kushiriki Kombe la Dunia hapo mwakani.
Hata hivyo, baadhi ya timu nyingine ambazo zinaweza kuleta upinzani katika AFCON ni Cameroon na Nigeria ambazo zimeshindwa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2026.
Katika michuano ya Kombe la Dunia, mara nyingi michezo ya Kombe la Mataifa ya Afrika imekuwa ikitumika kama kiashirio cha maanfalizi kwa timu za Afrika kushiriki fainali za Kombe la Dunia.
Timu hizo tisa kutoka Bara la Afrika, zitakuwa zinajipanga kuhakikisha mwakani zinapepeperusha vyema bendera za nchi zao katika Kombe la Dunia, michuano itakayopigwa nchi za Marekani, Canada na Mexico.




