KAULI ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres kuwa Tanzania ni nchi ya kupigiwa mfano wa amani katika bara la Afrika na duniani kwa ujumla, ni ushahidi dhahiri wa utambulisho wa kihistoria wa nchi yetu kimataifa, hivyo hapana budi hadhi hiyo kulindwa na kudumishwa.
Umoja wa Mataifa ni chombo kilichoanzishwa Oktoba 1945 baada ya kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kikiwa na malengo ya kudumisha amani, usalama, kujenga na kuendeleza uhusiano wa utengamano miongoni mwa mataifa.
Guterres anaposema Tanzania wakati wote imekuwa ni rejea muhimu ya amani na mshikamano wa kijamii Afrika na duniani, anajua thamani ya amani kwani kile ambacho jamii ya watu duniani imepitia wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, ni maafa makubwa kuwahi kutokea katika historia ya wanadamu ambayo UN inajitahidi kuhakikisha hayajirudii tena.
Umoja wa Mataifa umekuwa ukishughulikia kurejesha amani katika nchi ambazo zimepoteza tunu hiyo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za vurugu, migogoro na hata vita kamili, na Guterres kutamka Tanzania ni rejea ya amani duniani anajua mchango wa Tanzania katika kuhahikisha dunia ni mahali salama kwa kila binadamu.
Kauli hiyo ya Guterres kuhusu amani ya Tanzania ni ujumbe mzito kwa Watanzania kwamba hawana budi kujivunia hali hiyo, kwa sababu kuna mataifa ambayo wameipoteza amani na sasa wanahangaika kuitafuta na kuirejesha kwa gharama kubwa.
Ni miaka 64 sasa, tangu Tanzania ilipopata uhuru Desemba 9, 1964 na kujijengea sifa ya kipekee Afrika na duniani ya kuwa taifa lenye amani na umoja, likivuka mipaka ya udini, ukabila, rangi ya ngozi ya mtu na hata itikadi za kisiasa na kuendelea kuwa lenye amani na umoja.
Lakini, Oktoba 29, mwaka huu, kama alivyosema Guterres amani ya nchi ilijaribiwa na kupongeza uwezo wa Tanzania kuvuka salama katika jaribio hilo, hatua inayodhihirisha uimara wa uongozi wa nchi, moyo wa uzalendo wa Watanzania katika kulinda amani.
Matamanio ya Katibu Mkuu Guterres ni kutaka kuona amani ya Tanzania inaendelea kudumu, ndiyo maana ameunga mkono hatua ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuunda Tume Huru ya Uchunguzi wa matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29, ili kujua chanzo chake na matokeo ya uchunguzi kufanyiwa kazi ili kamwe zisijirudie tena.
Kimsingi, Umoja wa Mataifa unaitazama Tanzania kama mwalimu wa amani kwa bara la Afrika na duniani, msimamo ambao Watanzania kwa ujumla wanapaswa kuhakikisha unaendelezwa kwa kudumisha amani ya taifa kwa sababu inategemewa pia na wananchi wa mataifa mengine.
Wakimbizi wanaokimbilia kujihifadhi Tanzania na kuhudumiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR), inadhihirisha amani ya taifa letu si kwa ajili ya Watanzania pekee, bali hata wale wa mataifa mengine.
Kauli ya Katibu Mkuu Antonio Guterres kwamba Tanzania ni rejea ya amani kwa bara la Afrika na duniani, ni ujumbe kwa Watanzania kwamba nchi yetu kimataifa ina hadhi ya kipekee inayostahili kudumishwa na kulindwa kwa gharama zozote.




