Na SUPERIUS ERNEST
NI maajabu! Ndivyo unavyoweza kusema ukisikiliza simulizi za wanufaika wa mikopo isiyo na riba inayotolewa na halmashauri nchini, ikitokana na asilimia 10 ya makusanyo yao ya ndani.
Miongoni mwa maajabu hayo, ni namna ambavyo wanufaika wanapiga hatua kubwa ya maendeleo na kuondoa umasikini wa kipato.
Ufuatiliaji wa gazeti hili kwa baadhi ya wanufaika ulibaini, kikundi cha kinamama kilichokopa sh. milioni 180 kimepata mwanga wa mafanikio ya kiuchumi.
Mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri, ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa katika kuchochea uchumi wa wananchi hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambao ndiyo walengwa wa mpango huo.
WANUFAIKA
Wakizungumza na UHURU kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo, walipongeza serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kusimamia jambo hilo.
Akisimulia namna mkopo huo ulivyokomboa uchumi wake na wenzake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Kata ya Miburani, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, Zaituni Twanga alisema mwaka 2018 walipata mkopo wa sh. milioni 189, ambao umewakwamua kiuchumi.
“Tulipata mkopo wa shilingi milioni 189 mwaka 2018 na hadi hivi sasa tumesharejesha shilingi milioni 110, ambao kwa marejesho tunayoendelea nayo tunatarajia kumaliza mkopo huo kama ulivyo utaratibu,” alisema.
Alisimulia kuwa, jukwaa hilo linaundwa na wanawake ambao wanajihusisha na uzoaji taka ngumu katika Kata ya Miburani, kwamba kupitia mkopo huo walinunua gari kubwa la kubebea taka ambalo linaendelea kuwasaidia kutekeleza majukumu yao.
Zaituni alifafanua, kupitia mradi huo wameinuka kiuchumi kwa kuwa licha ya kutakiwa kurejesha mkopo, pia unawasaidia kupata fedha za kujikimu kwa mambo mbalimbali huku wakiendelea kutekeleza miradi yao binafsi midogo.
Mwenyekiti Zaituni aliishukuru serikali chini ya Rais Dk. Samia, kwa kuendelea kuwatambua na kuwapa fursa ya kutekeleza mradi wao na kurejesha mkopo huo kama walivyopangiwa.
“Tunamshuru sana Rais Dk. Samia kwa kuendelea kutupatia fursa wanawake kujikwamua kiuchumi…,huu ni mradi wetu mkubwa wa thamani ambao tunautekeleza, hakika tunamshukuru sana kwa jitihada zake anazoendeleza nazo za kuwakwamua wananchi,”alisema.
Alisema kutokana na mafanikio wanayoendelea kuyapata yakiwemo kusomesha watoto, kujenga nyumba za makazi na kumudu kujisimamia kiuchumi, wanakusudia kuchukua mkopo mkubwa zaidi watakapomaliza kulipa wa hivi sasa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Vijana Kata ya Buza, Jacqline Beda, alisema jukwaa lao limenufaika na mkopo huo wa asilimia 10.
Alisema kikundi chao kinachoundwa na vijana 10, mwaka 2022 kilipata mkopo wa sh. milioni 39, ambazo walizielekeza katika mradi wa usafirishaji kupitia bajaji.
“Tulinunua bajaji nne, ambazo tunaendelea kutekeleza mradi wetu huu, na hivi sasa tunaendelea kurejesha mkopo wetu vizuri,” alisema.
Akieleza tija ya mkopo huo, Mwenyekiti Jacqline alisema umewasaidia kwa kiasi kikubwa kwa kuwa wengi wao walikuwa wamekata tamaa ya maisha kwa kutokuwa na mwelekeo wa kiuchumi, kupitia mkopo huo mambo yao ni mazuri.
Jacqline alisema mkopo huo umewapa uthubutu wa kuziendea fursa kujikwamua kiuchumi.
“Vijana wawe na uthubutu wasikate tamaa, mikopo inapatikana, wakivumilia na kutimiza vigezo wanapata mikopo kwa uhakika kama sisi tulivyonufaika, ahadi za serikali ni za kweli kama wakiwa na dhamira ya dhati,” alisema.
Kwa mujibu wa Jacqline, matarahio yao baada ya kukamilisha marejesho ya mkopo wa hivi sasa watachukua mwingine mkubwa zaidi kuboresha biashara yao.
Alieleza kuwa, ni ndoto ya kikundi hicho kumiliki vyombo vya juu zaidi katika biashara ya usafirishaji ikiwezekana wapate magari, ambayo watayaingiza katika biashara ya kukodisha.
WATARAJIWA
Kwa upande mwingine wapo wanaotarajiwa kupata mikopo kutoka kikundi cha GUFEM, ambacho Katibu wa kikundi hicho, Mohamed Yahya Mohamed alisema wamejipanga vema.
Alisema kikundi chao ambacho kipo Kata ya Buza Mtaa wa Kidagaa, kikijihusisha na masuala ya usafirishaji, kina matumaini makubwa ya kupata mkopo huo baada ya kupata semina ya matumizi.
Mohamed alieleza furaha ya kufikia hatua ya kusahiliwa na kupewa semina ya matumizi ya fedha watakazopata na kuongeza : “Tunaishukuru serikali kwa hatua hii tuliyofikia.”
Alisema nia ya serikali ni nzuri ya kutoa mikopo hiyo kuwafikia wananchi wake wakuze uchumi wao, hivyo ni jukumu lao kufuatilia na kupata taarifa sahihi za mikopo hiyo.
“Wapo baadhi ya wananchi wakiwemo vijana wanakatisha wenzao tamaa wenzao kwamba mikopo hii inatolewa kwa upendeleo, jambo ambalo siyo kweli, kwani hata sisi tuliambiwa hivyo, baada ya kufuatilia sasa tumefikiwa na tunaamini kuwa tutapata mkopo huo,”alisema.
Akieleza mkakati wao juu ya mkopo huo watakaoupata ni kuwekeza katika usafirishaji wa magari madogo ya biashara, ambayo wameomba jumla ya sh. milioni 92, hivyo wamejipanga vyema kuhakikisha wakipata wanaufanyia kazi na kurejesha kwa wakati.
Aliishukuru serikali ya Rais Dk. Samia, kwa kuendelea kutoa fursa hiyo huku akiwasisitiza vijana kuchangamkia fursa hiyo adhimu.




