Na ATHNATH MKIRAMWENI
SERIKALI imeunda tume maalumu kuchunguza tuhuma za utendaji usioridhisha zinazoikabili Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke.
Kazi nyingine itakayofanywa na tume hiyo ni tuhuma za kuzimwa mashine za X-Ray.
Kauli hiyo, ilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Seif Shekalaghe, siku chache baada ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa kufanya ziara katika hospitali hiyo na kubaini changamoto kadhaa.
“Tumeandaa kamati maalumu ya kuchunguza tuhuma hizo na inaendelea na kazi yake, watakapokamilisha uchunguzi tutatoa taarifa, kwa maana kitu kinachofanyika kwa sasa ni uchunguzi wa kina wa tuhuma hizo,” alisema.
Hivi karibuni, serikali ilitangaza kuanza msako mkali dhidi ya watumishi wa afya wanaodaiwa kuhujumu utoaji huduma kwa makusudi na kusababishwa wagonjwa kukosa huduma ndani ya hospitali za umma na kulazimika kwenda binafsi.
Kauli hiyo, ilitolewa hivi karibuni na Mchengerwa, kuwepo tuhuma za kuzimwa mashine za X-ray katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke.
Kitendo hicho, kilisababisha wagonjwa kukosa huduma muhimu na kuelekezwa kwenda katika zahanati na maeneo mengine binafsi kupata matibabu.
Alisema watumishi wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo, watachukuliwa hatua kali za kisheria bila muhali.
Alisisitiza kuwa, serikali haitavumilia hujuma zinazolenga kunufaisha sekta binafsi kwa kuwaumiza wananchi.
Mchengerwa, alisema uchunguzi wa awali, umedai kuwa, baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu, walizima mashine za X-ray kwa makusudi, licha ya kuwa vifaa hivyo vinafanya kazi.
Alisema taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuhusu kuwepo kwa mashine za X-ray zisizofanya kazi katika Hospitali ya Temeke, hazina ukweli wowote, isipokuwa ni matokeo ya hujuma zilizopangwa.
“Mashine zote za X-ray zilizopo Temeke, zinafanya kazi na zimesimikwa kupitia uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha huduma za afya nchi nzima,” alisema.
Alisema baada ya kupokea taarifa hizo, aliagiza kufanyika uchunguzi wa kina kubaini ukweli wake.
Uchunguzi uliofanyika, ulibaini kuwa hujuma hizo, zilisababisha wagonjwa kukosa huduma ndani ya hospitali na kulazimika kupata huduma katika vituo binafsi.
Mchengerwa, alieleza vitendo hivyo ni usaliti mkubwa kwa serikali na wananchi kwamba, uchunguzi unaendelea kuwabaini wahusika wote.
“Natoa onyo kali kwa watumishi wote wa sekta ya afya, yeyote atakayehujumu huduma za afya kwa makusudi atachukuliwa hatua kali za kisheria na kinidhamu, zikiwemo kufukuzwa kazi na kutopata ajira yoyote ndani ya hospitali na kama ni daktari, tutamnyang’anya cheti chake na hatafanya kazi hata nje ya Tanzania,” alisisitiza.
Mchengerwa aliwahakikishia wananchi kuwa, serikali itaendelea kusimamia kwa ukaribu utoaji wa huduma za afya na kuhakikisha vifaa vyote vinavyonunuliwa kwa fedha za umma vinatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi.




