Na NASRA KITANA
LICHA ya kutinga nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi, Kocha wa Simba, Steven Barker, hajaridhishwa na kiwango kilichoonyesha na timu yake dhidi ya Fufuni juzi.
Simba ilitinga nusu fainali ya michuano hiyo baada ya juzi kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Fufuni katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini, alisema bado ana kazi kubwa ya kukinoa kikosi hicho, kuhakikisha kinakuwa bora kwa kucheza soka la kuvutia katika kila mechi.
“Tumeshinda lakini sijaridhishwa jinsi wachezaji wangu wanavyocheza, bado nina kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha tunakuwa na kikosi bora chenye ushindani, ninachohitaji ni kuona tunashinda katika kila mchezo,” alisema.
Wekundu hao wa Msimbazi kesho watashuka dimbani kuchuana na Azam FC katika nusu fainali ya michuano hiyo.




