Na ATHNATH MKIRAMWENI
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa onyo kali kwa watu wote wanaojaribu kuvuruga amani ya nchi.
Amewataka waache mara moja kwa sababu, vitendo hivyo ni hatari kwa mustakabali wa taifa.
Amesema serikali itaendelea kushirikiana na wananchi, kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanaendelea kuwa rafiki, huku amani ikilindwa.
Dk. Samia, alitoa kauli hiyo, alipozindua hoteli ya Jaz Elite Aurora iliyopo eneo la Michamvi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
Alisema kuwa, amani na utulivu wa kisiasa ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi.
“Kwa hiyo amani ikivunjika haichagui, niwaombe sana maendeleo yetu, kunawiri kwetu kupendeza kwetu, kulala na kuamka salama, tutunze amani ya nchi yetu, tofauti za mawazo zipo, lakini zisitugawe wala tusiharibu utulivu wa kisiasa na amani ya nchi yetu,” alisema.
Rais Dk. Samia, alikumbusha kuwa, amani ndicho chanzo cha ukuaji wa sekta ya utalii, ambayo imeendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa.
Alisema kuwa, serikali itaendelea kushirikiana na wananchi, kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanaendelea kuwa rafiki, huku amani ikilindwa.
UMUHIMU WA UWEKEZAJI
Rais Samia, alisema uwekezaji unaofanyika nchini, umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la pato la taifa, ajira na kuboresha maisha ya wananchi, huku akisema sekta ya utalii, imeendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi.
Alieleza kuwa, kuanzia mwaka 2022 hadi 2025, sekta ya utalii imeajiri zaidi ya Watanzania milioni 2.5, huku idadi ya watalii wa ndani na nje, ikiongezeka kwa kasi kutoka kipindi cha changamoto za UVIKO-19.
Kwa upande wa Zanzibar, Rais Samia, alisema idadi ya watalii, imeongezeka hadi kufikia zaidi ya 816,000 katika mwaka 2024/2025, huku mchango wa sekta ya utalii katika mapato ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ukifikia zaidi ya asilimia 30.
Rais Samia, aliipongeza Kampuni ya ‘Reliance Resort Insurance Limited’ kupitia Jazz Elite Aurora kwa uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani takribani milioni 135, ambao umeajiri zaidi ya wafanyakazi 1,058, wengi wao wakiwa Watanzania kutoka maeneo ya jirani.
Alisema tofauti na ilivyokuwa zamani, vijana wa maeneo ya karibu, walikosa ajira kutokana na ukosefu wa ujuzi, kampuni hiyo, imeweka mkazo kuwajengea uwezo, kuwapatia mafunzo na kuwapa nafasi ya kushindana katika soko la ajira.
Rais Samia, alipongeza ujenzi wa hoteli hiyo, kuzingatia uhifadhi wa mazingira, akisisitiza kuwa, maendeleo ya utalii, lazima yaende pamoja na ulinzi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali asilia.
Akizungumzia Mkoa wa Kusini Unguja, Rais Samia, alisema umeendelea kuongoza kwa kasi ya ujenzi wa hoteli mpya, hali iliyochochewa na uwekezaji wa miundombinu ya barabara, umeme na majisafi na salama unaotekelezwa na serikali.
Alisisitiza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji kwa kulinda amani, usalama na utulivu wa kisiasa.
WAZIRI WA KAZI
Kwa upande wake, Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, alisisitiza uwekezaji wa kimkakati kama hoteli ya kimataifa ya Jazz Aurora, umechangia pakubwa kukuza uchumi wa Zanzibar.
Alisema kuwa, uwekezaji huo, umeongeza ushindani chanya katika sekta ya utalii, kuboresha huduma na kuinua hadhi ya Zanzibar katika soko la kimataifa.
Alieleza kuwa, kwa upande wa uchumi, hoteli ya Jazz Aurora ni mfano mzuri wa mafanikio ya sekta ya binafsi, ambayo imeongeza mapato ya serikali na kuchangia pato la taifa.
Waziri Sharif alisisitiza kuwa, hatua za kuimarisha miundombinu kama vile barabara, maji, umeme na mawasiliano zimewezesha ufanisi wa miradi ya uwekezaji nchini na kuongeza kuwa, imani ya wawekezaji, inatokana na utulivu wa kisiasa.
Vilevile alisema mafanikio hayo yamefanikisha kuongezeka kwa ajira, hasa kwa vijana, wanawake na kuiwezesha Zanzibar kuwa kitovu cha uwekezaji endelevu Afrika Mashariki.
Pia, aliipongeza kampuni ya Jazz Aurora kwa kuonyesha imani kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kusisitiza kuwa sera, sheria na miongozo ya uwekezaji nchini ni rafiki na zenye tija kwa wawekezaji.
MKURUGENZI WA ZIPA
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Saleh Saad Mohammed alisema eneo la Zanzibar limebadilika kutoka kuwa na hoteli moja ya kitalii hadi kuwa kitovu cha kisasa cha utalii.
“Takwimu zinaeleza hadi Desemba 2025, zaidi ya miradi 635 ya utalii imewekezwa na kuchangia kiwango cha uchumi, ajira na taswira ya Zanzibar kimataifa.
“Katika kipindi cha miaka mitano cha serikali ya awamu ya nane kuanzia mwaka 2020/2025 jumla ya miradi 588 imesajiliwa na ZIPA yenye mtaji wa makisio ya sh. bilioni 6.9 na kutegemea kutoa ajira ya zaidi ya 25,000,” alisema.
Alisema mafanikio hayo yanasababishwa na uongozi, mazingira na miongozo bora, uwepo wa amani na utulivu nchini.
Mohammed alimpongeza Dk. Samia kwa juhudi zake za kuipambania Tanzania kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji kwa lengo la kukuza uchumi.




