NA WAANDISHI WETU
ASKOFU Mkuu Mstaafu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, marehemu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, anatarajiwa kuzikwa leo katika Kituo cha Hija Pugu, Dar es Salaam, huku kanisa hilo likitaja sifa 13 za zilizomtambulisha na kumkumbuka.
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, aliungana na mamia ya waombolezaji na viongozi wa kitaifa kuuaga mwili wa Kardinali Pengo, tukio lililofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, Dar es Salaam.
Kardinali Pengo alifariki dunia Februari 19 mwaka huu, katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya moyo na mgongo.
Akizungumza jana katika ibada ya kuaga mwili wa Kardinali Pengo, Askofu Msaidizi Jimbo Kuu Dar es Salaam, Henry Mchamungu, alizitaja sifa 13 ambazo Kardinali Pengo atakumbukuwa kuwa ni kuwa na moyo wa ibada, sala na unyenyekevu.
Alisema sifa ya pili ya marehemu Kardinali Pengo, kupenda kuishi maisha ya ufukara kwa sababu hakupenda kujilimbikizia mali.
“Aliishi maisha ya kifukara, hakupenda kabisa kujilimbikizia mali maana kila alichokipata alikitoa kwa kanisa, kwa mfano baada ya kustaafu alichopewa kama zawadi alikitoa mara moja kwa miradi ya kanisa,” alisema.
Askofu Mchamungu alitaja sifa ya tatu ya marehemu Kardinali Pengo ni kujinasua na mambo ya ulimwengu, kwani hakuwa na akaunti binafsi, wala hakuwahi kumuona na simu.
“Alitoa nguvu yake katika sala na alijinasua na mambo ya ulimwengu huu, tulisikia alitoa mali zake zote hakuwa na mali binafsi, hakuwa na akaunti binafsi, simu sikuwahi kumuona nayo, sikuwahi kumpigia nilikuwa nampata kupitia simu za wasaidizi,” alisema.
Alisema sifa ya nne ya marehemu Kardinali Pengo ni nidhamu binafsi ya pekee hasa katika kusali, kuheshimu muda na kufanya kazi kwa bidii.
Askofu Mchamungu alieleza sifa ya tano ni kujiepusha na upendeleo, kwa sababu alipenda kusimamia ukweli, haki, amani na maadili.
Alisema sifa ya sita alipenda watoto, aliendeleza kituo cha Hija Pugu na sifa ya saba alisimama katika imani ambayo haikutetereka na iliendelea kukua.
Alisema sifa ya nane alikuwa mkweli anayezungumza kwa upendo.
CHANZO CHA KIFO
Askofu Mchamungu alisema Kardinali Pengo alipata maradhi ya mgongo na moyo yaliyomsumbua kwa muda mrefu, ambapo alipata matibabu nchini, Ujerumani, Marekani na India.
Alisema matatizo ya kiafya yaliongezeka na kugundulika zaidi kuanzia Novemba mwaka jana, ambapo alianza matibabu nchini Desemba 27 mwaka jana alipelekwa India.
Alisema alifariki dunia Februari 19 saa nne usiku kwa maradhi ya moyo ikiwa ni muda mfupi baada ya kutoka India.
WASIFU WA KARDINALI PENGO
Askofu Mchamungu alisema, Kardinali Pengo alizaliwa Agosti 5 mwaka 1944, kijiji cha Mwaziya, Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, akiwa ni mtoto wa sita kati ya tisa.
Alibatizwa Agosti 6 mwaka 1944, alipata komunio ya kwanza Juni 20, 1952, sakramenti ya kipaimara Agosti 15, 1952 huko Parokia ya Mwaziya.
Alisema, Kardinali Pengo alisoma elimu ya msingi katika shule mbili tofauti za Mwaziya -Mpito na Kalema kuanzia mwaka 1953 hadi 1958.
Aliongeza kuwa, katika kipindi cha mwaka 1959 hadi 1964 alijiunga na seminari ya Mtakatifu Yosefu iliyopo Sumbawanga.
MASOMO YA UPADRI
Askofu Mchamungu alisema 1965 hadi 1971, alisoma masomo ya falsafa na theolojia katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo Kipalapala mkoani Tabora.
Kwa mujibu wa Askofu Mchamungu, Kardinali Pengo alipewa daraja takatifu la ushemasi, Desemba 9, 1970 na Juni 20, 1971 alipewa daraja takatifu la upadri.




