Na ABDUL DUNIA
ILE ndoto ya Watanzania kuishuhudia timu ya taifa ‘Taifa Stars’, ikifanya vyema katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), pengine ndio wakati wake wa kukamilika.
Hatua hiyo inakuja baada ya Taifa Stars kujifunza katika AFCON tatu zilizopita na sasa ikiwa AFCON yake ya nne haina chochote cha kufanya isipokuwa kuweka rekodi ya kupata ushindi wake wa kwanza na pengine kutinga hatua ya mtoano.
Michuano ya AFCON 2025 iliyoanza jana nchini Morocco inatarajiwa kumalizika Januari 18, mwaka huu.
Katika michuano hiyo ya 35 ya fainali hizo, Taifa Stars ipo kundi C na timu za Nigeria, Tunisia na Uganda.
Fainali hizo zinatarajiwa kufanyika katika majiji ya Rabat, Casablanca, Agadir, Fez na Marrakech.
Michuano hiyo inayoshirikisha timu 24, jumla ya makundi sita yamepangwa ambapo kila kundi limehusisha timu nne.
Kundi A linaundwa na mwenyeji Morocco pamoja na timu za Mali, Zambia na Comoros. Morocco imewahi kucheza fainali hizo mara 20, Zambia 19, Mali mara 14 na Comoros ikicheza mara mbili.
Misri inaunda kundi B na timu za Afrika Kusini, Angola na Zimbabwe. Misri imefuzu fainali hizo mara 27, Afrika Kusini mara 12, Angola mara 10 wakati Zimbabwe ikicheza mara sita.
TAIFA STARS IKO HAPA
Tanzania ‘Taifa Stars’ inaunda kundi C na timu za Nigeria, Tunisia na Uganda.
Katika kundi hilo, Taifa Stars ndiyo timu iliyofuzu fainali hizo mara chache (4), Tunisia mara 22, Nigeria mara 21 wakati Uganda ikitinga mara nane.
Katika kundi hilo, Taifa Stars ndiyo timu pekee ambayo haijawahi kupenya hatua ya mtoano wakati Nigeria ikiwa ni bingwa mara tatu mwaka 1980, 1994 na 2013, Tunisia mara moja mwaka 2004 huku Uganda ikiwahi kushika nafasi ya pili mwaka 1978.

Wadau wa soka wanaamini Taifa Stars chini ya Kocha Miguel Gamondi, ina kila sababu ya kufanya vyema mwaka huu kama itajipanga vyema.
Wakizungumza kwa nyakati tofati na gazeti hili, straika wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Abdallah Kibadeni, alisema hivi sasa ni wakati wa Stars kufanya vyema na kufikia katika hatua nzuri.
“Kutokana na viwango vya wachezaji wetu na tayari tumeshatambua tunakutana na kina nani, nina imani tutafanya vyema na kuliletea heshima taifa letu,” alisema.
Kibadeni ambaye pia amewahi kuinoa timu ya soka ya Ashanti United, alisema wachezaji wa kikosi cha Taifa Stars katika fainali hizo, wanapaswa kujituma kwa hali ya juu kuibeba timu hiyo.
Kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella, alisema: “Jambo kubwa ni maandalizi ya kutosha na wachezaji kujitoa kila kitu kinawezekana, kwa sababu tuna timu nzuri ambayo inaweza kutupatia matokeo mazuri,”.
Mogella alisema ana imani Stars ikiandaliwa mapema na wachezaji wakitambua kitu cha kufanya, watafanya vyema katika michuano ya AFCON na kuacha historia nchini Morocco.
JESHI LA GAMONDI
Wakati wakipa ni Yakoub Suleiman, Hussein Masalanga na Zuber Foba, mabeki ni Bakari Mwamnyeto, Shomari Kapombe, Lusajo Mwaikenda, Mohamed Hussein, Nickson Kibabage, Wilson Nangu, Pascal Msindo, Ibrahim Bacca, Haji Mnoga na Dickson Job.
Viungo wanaounda timu hiyo ni Morice Abraham, Feisal Salum, Yusuph Kagoma, Habib Idd, Kelvin Nashon, Novatus Dismas na Alphonce Mabula huku washambuliaji ni Mbwana Samatta, Simon Msuva, Kelvin John, Kibu Denis, Idd Nado, Abdul Sopu, Charles M’mombwa na Tarryn Allarakhia.

KUNDI D
Senegal inaunda kundi D na timu za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Benin na Botswana.
DRC imefuzu fainali hizo mara 21, Simba wa Teranga (Senegal) mara 18, Benin mara tano wakati Botswana mara mbili.
Algeria ipo kundi E na timu za Burkina Faso, Guinea ya Ikweta na Sudan.
Katika michuano hiyo, Algeria imewahi kufuzu mara 21, Burkina Faso mara 14, Sudan mara 10 na Guinea ya Iketa ikifuzu mara tano.
Bingwa mtetezi Ivory Coast ipo kundi F na timu za Cameroon, Gabon na Msumbiji.
Ivory Coast imefuzu fainali hizo mara 26, Cameroon mara 22, Gabon mara tisa wakati Msumbiji ikifuzu michuano hiyo mara sita.
TANZANIA ILIVYOFUZU
Taifa Stars ilifuzu fainali hizo baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Guinea katika mchezo wa mwisho wa kundi H, kuwania kufuzu AFCON uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Bao la mshambuliaji nyota, Simon Msuva katika dakika ya 61, limeipeleka Tanzania katika AFCON baada ya kufikisha pointi 10 na kukwea hadi nafasi ya pili katika kundi hilo.

Msuva aliiandikia Stars bao katika dakika ya 61, akiuweka mpira kimiani kwa kichwa baada ya kuunganisha pasi ya Mudathir Yahya.
Bao hilo liliibua shangwe la aina yake kutoka kwa wachezaji na mashabiki walioujaza uwanja wa Benjamin Mkapa wenye uwezo wa kuingiza watu 60,000.
TAKWIMU AFCON ZILIZOPITA
Katika fainali zote tatu zilizopita ambazo Stars ilishiriki, timu hiyo haijawahi kutinga hatua ya mtoano hata mara moja.
Katika michuano ya mwaka 1980 iliyofanyika Nigeria, Taifa Stars ilipangwa kundi A na timu za Nigeria, Misri na Ivory Coast.
Taifa Stars iliburuta mkia kwa pointi moja baada ya kutoka sare na Ivory Coast. Awali, ilifungwa mabao 3-1 dhidi ya Nigeria na mabao 2-1 ilipovaana na Misri.
Katika AFCON mwaka 2019 zilizofanyika nchini Misri, Tanzania ilipangwa kundi C na timu za Algeria, Senegal na Kenya.
Taifa Stars ilimaliza katika kundi hilo ikiwa nafasi ya nne baada ya kufungwa mechi zote tatu.
Kikosi hicho kilichokuwa kikinolewa na Amunike, kilianza kwa kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Senegal, kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Kenya na kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Algeria.
Pia, Taifa Stars iliburuta mkia katika hatua ya makundi ya AFCON mwaka 2023 zilizofanyika nchini Ivory Coast.
Ikiwa imepangwa kundi F, Stars ilivuna pointi mbili (nyingi zaidi ya AFCON ilizoshiriki awali), ikianza kwa kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Morocco, sare ya bao 1-1 kutoka kwa Zambia na suluhu dhidi ya DRC.
SAFARI YA MABILIONI
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), michuano ya AFCON inatarajiwa kutumia dau la dola za Marekani milioni 32 ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 78.3 za Tanzania kwa ajili ya zawadi pekee.
Katika mchanganuo wa fedha hizo, bingwa wa michuano hiyo anatarajiwa kuvuna dola za Marekani milioni saba ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 17.1.
Timu itakayoshika nafasi ya pili itavuna dola za Marekani milioni nne ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 9.7 za Tanzania.
Timu mbili zitakazoishia hatua ya nusu fainali, kila moja itaondoka na dola za Marekani milioni 2.5 ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 6.1 za Tanzania.
Timu nne zitakazoishia hatua ya robo fainali zitavuna dola za Marekani milioni 1.3 ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 3.1 za Tanzania.
CAF pia imeeleza kwamba, miamba minane itakayoishia hatua ya 16 bora itavuna dola za Marekani 800,000 ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 1.9 za Tanzania.
Timu zitakazoishia nafasi ya tatu katika kundi, kila moja itaondoka na dola za Marekani 700,000 ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 1.7 wakati zile zitakazoburuta mkia katika kila kundi zitavuna dola za Marekani 500,000 ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 1.2 za Tanzania.





