Na SUPERIUS ERNEST
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan anaendelea ‘kuchanja mbuga’ ndani na nje ya nchi. Ndivyo unavyoweza kusema kwa sababu ya kazi kubwa anayoifanya ya kuchochea maendeleo nchini.
Dk. Samia ameendelea kuongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya maendeleo ikiwemo barabara, masoko, madaraja, miradi ya maji na nishati.
Miradi hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa wananchi na kuchochea maendeleo zaidi, jambo ambalo limempatia sifa nyingi Rais Dk. Samia na kuzidi kufahamika zaidi kwa uhodari wake wa uchapakazi.
Hivi karibuni, Rais Dk. Samia alitajwa kuwa miongoni mwa wanawake 100, wenye ushawishi na nguvu Barani Afrika kwa mwaka 2025 kutokana na uongozi thabiti, .
Ripoti hiyo ya utafiti ilifanywa na Kampuni ya Vyombo vya Habari, Utafiti na Mawasiliano ya Avance Media ya nchini Ghana.
Wanawake wengine waliyotajwa katika orodha hiyo ni Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Selma Malika Haddadi, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Shirley Botchwey.
Spika wa Bunge la Namibia Saara Kuugongelwa-Amadhila, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Veronica Mueni Nduva na Makamu wa Rais wa Angola Esperanca Da Costa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Avance Media, imemtambua Rais Dk. Samia kutokana na matokeo ya kazi zake ambazo zinaendelea kuhamasisha na kufungua fursa mpya kwa wanawake wa Kiafrika.
“Tunawaheshimu kwa matokeo makubwa ya kazi zao ambazo zinaendelea kuhamasisha na kufungua fursa mpya kwa wanawake wa Kiafrika,” ilisema.
Avance ilisema kupitia uongozi wa Rais Dk. Samia unadhihirisha ushawishi wa wanawake wa Kiafrika katika kuunda sera, utamaduni, uvumbuzi na mustakabali wa Bara la Afrika.
TUZO ZINGINE ZA HESHIMA ALIZOPATA RAIS DK. SAMIA
Agosti 2025, Dk. Samia alipata Tuzo ya Presidential Global Water Changemakers 2025, ambayo alitunukiwa Cape Town, nchini Afrika Kusini.
Tuzo hiyo ilipokelewa na kukabidhiwa kwake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo..
Tuzo hiyo ya Ulimwengu ya Marais wanaoleta Mabadiliko katika Sekta ya Maji ilitolewa kwa kutambua uongozi bora na dhamira ya dhati katika kuanzisha na kuendeleza mipango na miradi ya maendeleo katika sekta ya maji nchini Tanzania.
Aidha, kiongozi huyo, alipokea tuzo kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) Dk. Patrice Motsepe, kwa kutambua mchango wake mkubwa katika maendeleo ya mpira wa miguu.
Tuzo nyingine, aliyopata Rais Dk. Samia, ile Maalumu ya Kimataifa ya The Global Goalkeeper Award kutoka kwa Rais wa Kitengo cha Usawa wa Jinsia wa Taasisi ya Gates, Dk. Anita Zaidi, Februari 4, 2025.
Tuzo hiyo hutolewa kwa viongozi waliowezesha nchi zao kuharakisha maendeleo kuelekea kufikia malengo ya maendeleo endelevu, katika kipengele cha mapambano dhidi ya vifo vya mama wajawazito na watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.
Siyo mara ya kwanza kwa Rais Dk. Samia, kutajwa na majarida ya kimataifa, kwani hata miaka ya nyuma alitajwa mara kadhaa na majarida mashuhuri duniani kama lile la Forbes, likitambua kazi kubwa anazozifanya tangu kuapishwa rasmi kuwa Rais, Machi 2021.
Desemba 11, 2022 Dk. Samia alipata tuzo ya kimataifa ya kuwa mwongoza watalii bora kutoka Taasisi ya Kimataifa ya International Iconic Award ya India, aliyokabidhiwa jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Taasisi ya Miss Jungle International ya India, Haroun Kinega.
Desemba 8, 2022 jarida la Forbes la Marekani, lilimtaja Rais Samia kuwa miongoni mwa wanawake 100 wenye ushawishi duniani ikiwa ni mara ya pili kutambuliwa na jarida hilo ambapo kwa mara ya kwanza lilimtaja Desemba 2021.
Tuzo zingine za heshima za kimataifa alizopata Dk. Samia ni ile aliyopewa na Umoja wa Mataifa (UN) ni ile ya Babacar Ndiaye kwa kutambua jitihada za ujenzi wa miundombinu.
Pia, Mei 24, 2022, Rais Dk. Samia alitajwa na jarida la Time 100, kuwa miongoni mwa viongozi 100 wenye ushawishi mkubwa duniani kutokana na uongozi wake wa kipekee aliouonyesha tangu alipoingia madarakani mapema mwaka 2021, baada ya kifo cha Dk. John Magufuli ikiwemo kuanzisha maridhiano ya vyama vya upinzani.
Sifa zingine za Rais Dk. Samia zilizompatia umashuhuri ni kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari kuwateua wanawake katika wizara muhimu kama afya, utalii na ulinzi.
Viongozi wengine waliotajwa na jarida hilo ni rais wa Ukraine Volodymir Zelenskyy, Xi Jinping wa China, Vladimir Putini wa Russia, rais mstaafu wa Marekani Joe Biden, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Apple Tim Cook.
UWT YATOA NENO
Wakati Rais Dk. Samia akitajwa na kampuni hiyo, Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), ilisema hatua hiyo imetokana na uchapakazi, ubunifu, uhodari aliyonao katika kutatua changamoto za Watanzania, ambao unamfanya azidi kukubalika nchini na majukwaa ya kimataifa.
Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa UWT Suzan Kunambi, alisema jumuiya hiyo inajivunia kutajwa kwa Rais Dk. Samia na kampuni ya Avance, kwani ni matokeo ya utendaji mzuri.
Suzan alisema Rais Dk. Samia anakubalika ndani na nje ya nchi kutokana na jitihada mbalimbali za kujenga nchi, kukuza diplomasia na mataifa mbalimbali.
“Tunajivunia kuwa na kiongozi ambaye anakubalika duniani na majukwaa mbalimbali ya kimataifa, hii imetokana na uchapakazi wake, uwezo na namna anavyotatua changamoto za wananchi.”alisema.
Alisema Rais Dk. Samia ni mbunifu, anakipaji cha uongozi na uchapakazi wake na namna anavyotatua changamoto za wananchi, hivyo kuendelea kutambulika kimataifa.
Suzan, alisema UWT, inaona fahari kuona Rais Dk. Samia anaendelea kutajwa katika majukwaa mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Mchambuzi wa siasa
Naye Mchambuzi wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Gerson Mgonja, alisema kutajwa kwa Rais Dk. Samia katika majukwaa na tafiti mbalimbali za kimataifa kunaonesha umaridadi wa hali ya juu katika medani ya uhusiano wa kimataifa.
Alisema hatua hiyo itasaidia Tanzania kuzidi kuaminika zaidi kwa sababu Rais Samia ameendelea kuitangaza vyema, jambo ambalo litazidi kuvutia wawekezaji.
Mhadhiri wa Chuo Cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kigamboni, Dk. Philip Daninga alisema mafanikio ya Rais Dk. Samia kutambulikana kimataifa ni tafsiri chanya kwa nia yake ya dhati ya kuwatumikia wananchi.
Alisema mataifa hayo yanamtambua kwa umahiri wake wa utendaji kazi na ubunifu wa kukuza uchumi wake, kupitia filamu ya Royal Tour ambayo imevutia wananchi wa mataifa mbalimbali kufika nchini.
“Kupata tuzo za kimataifa siyo jambo jepesi kwa kuwa zinajumuisha wasomi na wataalamu mbalimbali ambao huwa wanafuatilia kwa ukaribu mwenendo na utendaji kazi na kumpima mhusika katika michujo mbalimbali, hivyo pongezi kwa kiongozi wetu kukubalika na viongozi hao mashuhuri,”alisema.
Aliwataka wananchi kumuunga mkono Rais Dk. Samia kwa dhamiri yake ya dhati anayoionyesha ya kuwatumikia watanzania kwa nguvu zake zote akizunguka sehemu mbalimbali kwaajili ya kutafuta maendeleo ya nchi.
Mwenyekiti wa umoja wa Madaktari Filosofi na Maprofesa Tanzania(APDPT), Profesa Rejoice Ndalima alisema tuzo na heshima hizo alizozipata Rais Dk. Samia siyo kwa bahati mbaya ni kutokana na ukomavu, weledi na umahiri aliyoonyesha katika kipindi kifupi cha uongozi wake.
Alisema tangu Dk. Samia kuingia madarakani amesaidia taifa kuwa imara na utulivu, licha ya kupitia katika changamoto kubwa za kitaifa na kimataifa, ikiwemo janga la Covid – 19, mabadiliko ya hali ya uchumi wa dunia kuliko sababisha mfumuko wa bei, lakini yote hayo ameweza kuyahimiri pasipo kuhofia.
“Kwa hayo na mengine, hakika anastahili heshima hizo alizozipata za kimataifa na kitaifa na kupitia hizo, taifa letu limezidi kutambulika duniani na kuleta tija ya ukuaji wa kiuchumi, hivyo kila mmoja ana kila sababu ya kumuunga mkono kiongozi wetu mahiri na mzalendo,”alisema.
Alisema kiongozi huyo ameonyesha uwezo mkubwa wa uongozi kwa kuondoa tofauti za kisiasa na kuleta maridhiano ya kisiasa, kuunganisha nchi kwa kidiplomasia ya uchumi na kutangaza utalii, mambo ambayo yameleta taswira nzuri ya kiongozi huyo duniani kote.
Profesa Ndalima alisema utendaji wa Dk. Samia unaonekana dhahiri kwa vitendo vyake, jitihada na dhamiri yake ya dhati ya kukuza uchumi na kusaidia wananchi wake.




