Na Jacqueline Liana
WAZIRI wa Afya Mohamed Mchengerwa, amewataka waandishi wa habari kuandika habari za uchunguzi kufichua uovu wowote utakaofanyika dhidi ya bima ya afya kwa wote.
Waandishi wa habari ambao ni weledi wa taaluma, wito huo wa Mchengerwa, ambao ni nadra kutolewa na kiongozi mwandamizi serikalini, ni ushirikishwaji wa kizalendo katika taifa lililokusudia kutoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa pasipo ubaguzi.
Mtumishi wa umma wa ‘levo’ ya Mchengerwa kutamka kwamba waandishi wa habari wako huru kuandika habari za uchunguzi kufichua ulaghai katika mpango huo iwapo utatokea, ni dhahiri serikali inataka umma wa Watanzania ufahamu dhamira yake kwa afya za Watanzania ni njema.
Uzoefu unaonyesha walio serikalini hujitahidi kufanya kila wawezalo kukwepa waandishi wa habari, lakini Mchengerwa ameng’amua kuwa mpango wa bima ya afya kwa wote ufanikiwe, waandishi wa habari hapana budi washirikishwe.
Alipozungumza na wahariri na waandishi wa habari, wiki ya kwanza ya mwezi huu, katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam, Mchengerwa alisema, kuna nguzo moja ya uandishi wa habari ambayo huamua kama taifa litaongoza kwa ukweli au litasukumwa na uvumi, nguzo hiyo ni uandishi wa habari za kiuchunguzi.
“Huu si uandishi wa kuiga maneno, wala wa kusukumwa na mihemko; huu ni uandishi wa kuuliza maswali magumu, kufuatilia ushahidi, na kuweka ukweli mezani kwa masilahi ya umma,” alisema Mchengerwa.
Uandishi wa habari za uchunguzi, waziri huyo alisema ni taa inayomulika giza la mifumo, ni doria inayozuia uovu kabla haujawa janga, na ni kioo kinacholazimisha viongozi kujisahihisha.
“Penye uandishi wa kiuchunguzi, uwajibikaji huongezeka; na uwajibikaji ukiongezeka, mfumo unakuwa salama na imani ya wananchi inaimarika,” alibanisha Mchengerwa.
Alisema sekta ya afya inashughulika moja kwa moja na maisha ya watu, ni muhimu nguzo hiyo ya uandishi wa habari ikatumika katika kurekebisha mambo pale yaendapo mrama.
“Hivyo tunapolinda uandishi wa kiuchunguzi, hatulindi taaluma tu, tunalinda haki ya mwananchi kuishi, tunalinda fedha za umma, na tunalinda usalama wa taifa,” alifafanua Mchengerwa.
Bima ya afya kwa wote inakusanya mchango wa mwananchi; mchango mdogo, wa jasho, na wa imani na kuuweka kwenye mfumo ulinde maisha yake.
Ndani ya mfumo huo, Mchengerwa aliwaambia waandishi wa habari kwamba, kuna maadui wawili; kwanza ni magonjwa, ambayo kupambana naye ni kwa kinga, tiba, na ubora wa huduma.
Adui wa pili ni ulaghai na udanganyifu, ambaye mapambano dhidi yake ni uwazi, ukaguzi, mifumo thabiti, na uandishi wa habari wa kiuchunguzi.
“Ndiyo maana ninaweka hadhi yenu mahali pake. Nyinyi ni macho ya wananchi na walinzi wa uaminifu wa mfumo”, alisema Mchengerwa.
Mara nyingi, kwa mujibu wa waziri huyo, dalili za ubadhirifu huonekana katika vituo vya kutolewa huduma za afya, katika madai, kwenye foleni, kwenye risiti, na malalamiko ya wananchi.
“Hapo ndipo uandishi wa kiuchunguzi unafanya kazi kama doria, unaona mapema, unazuia mapema na unaokoa mapema. Uandishi wa habari wa kiuchunguzi ni kinga ya mfumo; bila kinga, mfumo huumwa,” alifafanua.
“Sitakubali chini ya uongozi wangu, NHIF ichezewe hata kidogo, kwenye hili nipo tayari kuchukiwa na watu na tunaomba waandishi wa habari mtubainishie haya mapungufu kupitia kalamu zenu kwa sababu tumedhamiria kuboresha sekta ya afya”, alisema Mchengerwa.
Alisema, NHIF kuchelewa kulipa madai kwa sababu ya ulaghai, wizi na utapeli kupitia mifumo ni mambo anayoyataka yamulikwe akisema hayupo tayari wakati wake kuona mifumo ikiyumba.
“Ulaghai ukiachwa, fedha zinaanza kutoka na kupotea, wahudumu wasiwafanye wananchi wakakatia tamaa bima, na wagonjwa kurudi kwenye hofu ya gharama. mwisho, imani ya wananchi itaondoka.
Hata sera itakuwa ngumu kutekelezeka, ulaghai si wizi wa fedha pekee, ni wizi wa huduma. Msimamo wa serikali ni kulinda mifumo na kulinda wanaofichua maovu.
Tutaongeza nguvu katika malipo ya madai, tutakagua nyayo za miamala ili kudhibiti, na tutagundua mapema kupitia ukaguzi wa ndani, tukishirikiana na vyombo vya uchgunguzi,” alisema.
Ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka ya nyuma zimekuwa zikibaini upotevu wa fedha ndani ya NHIF.
Taarifa ya CAG iliyotolewa Machi 2023, ilieleza watumishi 148 walibainika kuhusika na vitendo vya udanganyifu, miongoni mwao 129 walikuwa ni wa vituo vya afya binafsi na 19 NHIF.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa wakati huo, hatua za kisheria na nidhamu zilichukuliwa dhidi yao kupitia mamlaka za ajira; bodi au mabaraza ya kitaaluma huku watumishi wa NHIF waliohusika nao walichukuliwa hatua za kinidhamu.
Madhali kumewahi kutokea matukio ya kuhujumu NHIF, mwaliko wa Mchengerwa kuwataka waandishi wa habari kushiriki katika kuhakikisha bima ya afya kwa wote haichezewi, hauna budi kuzingatiwa.
“Mfumo wa bima ukivumilia ulaghai, huanza kufa taratibu. Ulaghai ukiingia na kuachwa, fedha zinaanza kutoka kuliko kuokoa. Vituo vinaanza kucheleweshewa malipo na huduma zinaanza kukatika. Wahudumu wanakata tamaa na wagonjwa wanarudi katika hofu ya gharama,” alisema Mchengerwa.
Imani ya wananchi ikiporomoshwa na vitendo viovu dhidi ya bima ya afya kwa wote, itakuwa ni janga na Watanzania wasikubali kufikishwa katika hali hiyo.
Mchengerwa alisema kwamba ulaghai katika bima ya afya si wizi wa fedha tu; ni wizi wa huduma na wizi wa maisha.
“Ukichezea uaminifu wa NHIF, unachezea uimara wa Taifa. Msimamo wa serikali ni kwamba tutajenga ulinzi wa mifumo, na tutawalinda wanaofichua uovu,” alisema waziri huyo.




