Na NJUMAI NGOTA
MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk. Diwani Msemo, amesema anajivunia mageuzi makubwa yaliyofanyika katika taasisi hiyo katika kipindi cha uongozi wake, akisisitiza azma ya kuhakikisha huduma za saratani nchini zinafikia viwango vya juu ikiwemo kupata ithibati ya kimataifa.
Ameeleza hayo jijini Dar es Salaam kupitia mahojiano maalumu yaliyofanyika na UHURU, kuhusu huduma za matibabu ya saratani zinazotolewa na taasisi hiyo.
“Ninajivunia mambo mengi, ninamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuniteua miongoni mwa Watanzania zaidi ya milioni 60…nitafanya kazi kuhakikisha huduma za saratani zinakua kwa kiwango cha juu,” alisema.
Alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa serikali ambayo imeendelea kuwekeza katika sekta ya afya na kuboresha huduma za saratani nchini.
Dk. Msemo alisema moja ya malengo makubwa ya uongozi wake ni kuhakikisha ORCI inafikia viwango vya kimataifa katika utoaji huduma za saratani.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, taasisi hiyo tayari imeanza mchakato wa kupata ithibati za kimataifa kwa huduma zake mbalimbali.
“Hadi Hivi sasa tumeshajielekeza katika kupata ithibati ya kimataifa na tunatarajia katika miaka miwili hadi mitatu ijayo, huduma zetu zitakuwa zimepata ithibati za kimataifa. Huduma za maabara zina ithibati za kimataifa, hizi nyingine nazo tunazielekeza huko,” alisema.
Dk. Msemo alisema mashine tatu mpya za mionzi zinazotarajiwa mwishoni mwa mwezi huu au ujao kuanza kufanya kazi, zote zimeshanunuliwa chini ya uongozi wake.
“Siyo fedha zangu ni za serikali. Ule ushawishi wa kupeleka hoja serikalini kuwaambia tuna shida, serikali ikachukua, wizara na Rais akatoa fedha ni kitu ambacho najivunia,” alisema Dk. Msemo.
“Nimeboresha mazingira kwa kiwango kikubwa, mazingira ya wagonjwa, mazingira ya wafanyakazi, hayo ni mambo ambayo najivunia na nitaendelea kuyapambania yakae sawa,”alisema.
Mbali na uboreshaji huo ndani ya taasisi, Dk. Msemo alisema ORCI inaendelea kushirikiana na mashirika ya kimataifa katika mapambano dhidi ya saratani kwa ngazi ya dunia, Afrika na taifa.
Alitaja miongoni mwa washirika wakuu hao ni Shirika la Afya Duniani (WHO), ambalo barani Afrika lina makao makuu katika mji wa Brazzaville, Congo na linaongozwa na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi kutoka Tanzania.
Dk. Msemo anaeleza shirika hilo hutoa miongozo ya kitaalamu kuhusu namna ya kukabiliana na saratani ikiwemo kusaidia mafunzo ya wataalamu wa afya.
Pia, ORCI inashirikiana na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) linalofuatilia matumizi sahihi na salama ya mionzi katika tiba.
Alisema ushirikiano huo umewezesha wataalamu wengi wa Tanzania kupata mafunzo ya tiba ya saratani.
“Hivi sasa kuna wataalamu wetu ambao wapo Afrika Kusini kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki na mimi nilifadhiliwa na Shirika la Afya Duniani nchini Afrika Kusini kwa miaka minne na baadaye nilifadhiliwa na shirika lingine miaka miwili,”alisema.
Dk. Msemo alisema ORCI inashirikiana na vyuo vikuu duniani katika utafiti na mafunzo kwa wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu, akitaja miongoni mwa vyuo hivyo ni Louisiana State University na taasisi nyingine za kimataifa na za ndani.
Alibainisha hayo yote yanafanyika kutokana na ukweli mapambano dhidi ya saratani hayawezi kufanywa na mtu mmoja au taasisi moja pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa wadau wengi wa ndani na nje ya nchi.
Katika kuimarisha kinga na uchunguzi wa mapema wa saratani, Dk. Msemo alisema ORCI ina kitengo maalumu kinachozunguka maeneo mbalimbali ya nchi kutoa huduma za uchunguzi na kuelimisha umma.
Alisema timu hizo hutoa mafunzo nchi nzima kwa watumishi wa afya katika hospitali wanazozitembelea ziendelee kutoa huduma za uchunguzi hata baada ya timu hiyo kuondoka.
Hata hivyo, alisema changamoto kubwa inayokwamisha kufikiwa maeneo mengi zaidi ni uhaba wa rasilimali fedha kutokana na ukubwa wa nchi.
“Ni vigumu kufika kila mahali nchini kwa sababu ya ukosefu wa fedha za kutosha, tunaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,” alisema.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi mtendaji huyo, katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wa Rais Dk. Samia, timu za uchunguzi ziliwafikia zaidi ya Watanzania 200,000.
Akizungumzia uelewa wa jamii kuhusu saratani, Dk. Msemo alisema ugonjwa huo unaweza kutokea katika sehemu yoyote ya mwili na mara nyingi huonesha dalili ambazo mtu anaweza kuzitambua mapema.
Dk. Msemo alisema saratani inaweza kutokea katika ngozi, uso, kinywa, utumbo au katika viungo vya uzazi na katika baadhi ya maeneo dalili zake huonekana wazi.
“Hakuna kitu kinachoitwa saratani kujificha. Inategemea iko sehemu gani mwilini, dalili zake zipo,” alisema.
Alifafanua mabadiliko yasiyo ya kawaida mwilini yanapaswa kumfanya mtu kumwona daktari mapema.
“Ndiyo maana tunasisitiza suala la elimu. Kama wewe ulikuwa unakwenda haja bila shida, halafu siku tatu huendi au tumbo linakuwa gumu, lazima ujiulize kuna nini. Ukifanya kipimo wanaweza kugundua kuna kitu kimeanza kuota.
“Kama wewe ulikuwa unapata siku zako za mwezi bila shida. Katika hali ya kawaida leo unakwenda siku 10, unatakiwa ujiulize kuna kitu ambacho hakipo sawasawa,”alisema.
Dk. Msemo alisema gharama za matibabu ya saratani ni kubwa ikilinganishwa na magonjwa mengi mengine.
“Kumtibu mgonjwa wa saratani gharama yake inaweza ikawa sawa na kutibu pengine wagonjwa 5,000 wa malaria. Gharama ya kutibu ni kubwa zaidi,”alisema.
Dk. Msemo anaeleza kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2022 duniani, kulikuwa na takribani wagonjwa wapya milioni 20 wa saratani, huku zaidi ya watu milioni saba wakipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Aliongeza kwa upande wa Tanzania, takribani wagonjwa wapya 45,000 hugundulika kila mwaka kati ya idadi ya watu zaidi ya milioni 60, huku vifo vinavyotokana na saratani vikifikia 31,000 kwa mwaka.
“Kati ya wagonjwa watatu waliogundulika kuugua saratani, wawili walipoteza maisha. Kuna nchi nyingine ambazo hazina kabisa hata hizi huduma,”alisema.
“Wakati wenzetu kule wameweka utaratibu wa kuzuia mambo ya kuvuta sigara katika maeneo ya wazi, kwetu watu wanaoona kuvuta sigara ni fasheni. Kunywa pombe inaonekana kama ni fasheni tena pombe kali kabisa,”alisema.

WAGENI WAMIMINIKA ORCI
Dk. Msemo alisema ORCI imekuwa kituo muhimu cha tiba ya saratani katika Kanda ya Afrika Mashariki na Kati, ambapo wagonjwa kutoka nchi mbalimbali hufika kupata huduma.
Alitaja baadhi ya nchi hizo ni Comoro, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia na Malawi.
Dk. Msemo alisema ujio wa wagonjwa kutoka nchi hizo unaonesha jinsi taasisi hiyo ilivyoendelea kuwa kitovu muhimu cha huduma za saratani katika ukanda wa Afrika.
Alibainisha hata viongozi kutoka baadhi ya nchi wamekuwa wakifika nchini kujadili ushirikiano wa matibabu ya saratani.
“Gavana mmoja kutoka Jimbo la Kasai, DRC alifika hapa na mwezi huu tunatarajia kupokea magavana wawili kutoka majimbo ya Lualaba na Katanga kuweka ushirikiano wa matibabu,” alisema.
JANETH PASCAL
Mgonjwa wa saratani ya titi, Janeth Pascal, aliitaka jamii kutowaficha wagonjwa wa saratani kwa kuwa ugonjwa huo unatibika.
Alisisitiza kuwapeleka wagonjwa katika taasisi hiyo kupata matibabu ya kibingwa.
Janeth alisema baadhi ya watu wamekuwa wakiwatenga wagonjwa wa saratani kutokana na imani potofu.
Kwa mujibu wa Janeth, afya yake imeimarika baada ya kupata matibabu ya kibingwa katika Taasisi ya Ocean Road.
“Baadhi ya watu wamekuwa na dhana potofu kwamba ugonjwa wa saratani hauna tiba, mtu akipata ndiyo mwisho wake wa maisha,” alisema.
Janeth alisema jamii inapaswa kuondoa dhana hiyo na elimu zaidi inatakiwa kutolewa kwa wananchi.
Alisema alipoanza matibabu ya saratani ya titi mwaka 2023 katika hospitali hiyo, afya yake ilizidi kuimarika akiwa chini ya uangalizi maalumu wa madaktari.
Alisema matibabu aliyopata Ocean Road yamefufua matumaini mapya, baada ya kutengwa na baadhi ya jamaa zake.
“Baadhi ya jamaa na marafiki walinitenga baada ya kuwapa taarifa nimegundulika nina saratani, lakini sikukata tamaa baada ya kuanza matibabu hali yangu ni nzuri nina uwezo wa kufanya shughuli zangu kama kawaida,”alisema.
Janeth alitoa rai kwa watu kuwahi hospitali kupata vipimo wanapoona mabadiliko ya mwili kwa lengo la kugundua ugonjwa huo mapema na kuanza matibabu.
Janeth alisifu matibabu bora aliyopata Ocean Road, akisema yamerejesha tabasamu kulinganisha na awali ambapo alipata mshituko baada ya kupokea majibu kuwa ana saratani ya titi.
“Baada ya kupata majibu kwa kweli nilipata mshtuko makubwa, lakini daktari alinipa ushauri mzuri nikarejea katika hali yangu, jambo la kufurahisha nilipokutana na wagonjwa wenzangu walinipa faraja,”alisema Janeth mwenye umri wa miaka 33 akitokea mkoani Tanga.
Taasisi ya Ocean Road imepata mafanikio makubwa katika utoaji tiba ya saratani chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuwapa chanjo ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi watoto wa kike milioni 1.2 wenye umri wa miaka tisa hadi 14.
Mafanikio mengine ni kupokea sh. bilioni 40 kutoka serikalini kwa lengo la kubadilisha miundombinu ya matibabu ambapo zimenunuliwa mashine za kisasa za ugunduzi wa saratani.
Taasisi hiyo iliyoanzishwa miaka 30 iliyopita, ina vifaatiba vya kisasa na imekuwa kimbilio la wagonjwa wengi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika.




