Na MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki amesema uwekezaji wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Airtel nchini umeongeza mapinduzi makubwa katika sekta ya mawasiliano.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maduka 17 ya Airtel, Goba jijini Dar es Salaam, Waziri Kairuki ameeleza kuwa uwekezaji huo ni ishara ya nia ya dhati kwa kampuni hiyo, kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya mawasiliano na kuonyesha imani yake katika mazingira ya biashara Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
“Maduka haya mapya yanaonyesha dhati ya Airtel katika kuleta huduma karibu na wananchi huku yakiboresha uzoefu wa wateja. Pia unaashiria imani thabiti katika mazingira ya biashara Tanzania,” amesema Waziri Kairuki.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, amesema maduka hayo hayako tu kama maduka ya rejareja bali yameundwa kama vituo vya kisasa vya huduma mbalimbali zikiwemo za kidijitali.
“Maduka haya yamewekwa katika maeneo yenye shughuli nyingi jijini Dar es Salaam, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakazi na wajasiriamali,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Uzoefu wa Wateja Airtel Tanzania, Adriana Lyamba, amesema maduka hayo yameundwa kutoa huduma haraka, bila karatasi, na kwa ufanisi.




