Na VICTOR MKUMBO
WAKATI ikiwa na kibarua cha kuikabili TRA United, Kocha wa Simba, Steve Barker amesema kikosi chake kipo kamili kuingia katika mchezo huo.
Simba itateremka dimbani kuikabili TRA United, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaofanyika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, jijini Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku.
Simba itaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya mabao 1-1 dhidi ya Pamba Jiji, huku TRA United ikisuluhu mbele ya Yanga.
Akizungumza kuelekea mchezo huo jijini Dar es Salaam, Kocha wa Simba, Barker alisema kikosi chake kipo kamili kuikabili TRA United.
Alisema wamejipanga vyema kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mchezo huo na kuondoka na pointi tatu muhimu.
Alisema anakwenda kukabiliana na TRA United yenye kikosi bora kwani hivi karibuni walitoka kupata sare mbele ya Yanga na walionyesha kiwango bora.
Alisema amefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha kikosi chake kinaibuka na ushindi na kutoa burudani murua kwa mashabiki wake kabla ya mapumziko mafupi kupisha mechi za Kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Alisema wachezaji wote wapo katika afya njema na wana morali ya kutosha kuelekea katika mchezo huo ambapo pia Seleman Mwalimu amerejea kikosini baada ya kumaliza adhabu yake ya kutocheza mechi tatu.
“Tupo kamili kwani tumefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo dhidi ya TRA United, tunatarajia utakuwa mchezo mgumu kutokana na wapinzani wetu kuonyesha kiwango bora mbele ya Yanga hivi karibuni.
“Tumejipanga vyema kuwakabili, wachezaji wangu wote wapo kamili kwa ajili ya mchezo huo na kwamba Mwalimu amerejea kikosini baada ya kumaliza adhabu ya kuzikosa mechi tatu, tutatengeneza nafasi na kuzitumia kupachika mabao,” alisema Kocha Barker.
Mchezaji Nickson Kibabage, alisema kwa ujumla wachezaji wote wamefanya maandalizi mazuri kuhakikisha wanafanya vyema katika mchezo huo.
Alisema kila mchezaji anajua umuhimu wa mchezo huo kwani wamekuwa wakihimizana kila mara mazoezini kuhakikisha wanaibuka na ushindi.
“Tumejipanga vyema na kila mchezaji anajua umuhimu wa mchezo unaofuata, tumekuwa tukihamasishana kuhakikisha tunapata ushindi na kutoa burudani kwa mashabiki, tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti,” alisema.
Kwa upande wake Kocha wa TRA United, Etienne Ndayiragije alisema wamejipanga vyema kuikabili Simba katika mchezo huo.
Alisema walisafiri salama kutoka Arusha na juzi walifanya mazoezi ya kwanza kabla ya jana, hivyo wanatambua umuhimu wa mchezo na wanahitaji kupata ushindi na kuendelea kusogea nafasi za juu katika msimamo.
Alisema mchezo utakuwa mgumu na wenye upinzani mkubwa kwani Simba ina kikosi bora chenye wachezaji wazuri, lakini watapambana kuhakikisha wanaibuka kidedea japokuwa watacheza ugenini.
“Tumejiandaa vyema kuhakikisha tunaibuka na ushindi katika mchezo unaofuata japokuwa tunatambua utakuwa mchezo wenye upinzani mkubwa.
“Tunatambua Simba ni moja ya timu zenye wachezaji wazuri zaidi, lakini tutapambana kuhakikisha tunafikia malengo ikiwemo kusogea nafasi za juu katika msimamo,” alisema.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ipo nafasi ya tatu kwa pointi 28 baada ya kucheza mechi 13 huku TRA United ikishikilia nafasi ya 10 kwa pointi 20 katika mechi 15 ilizocheza hadi hivi sasa.




