Na ZIANA BAKARI
WACHAMBUZI wa siasa wakiwemo wanasiasa wakongwe, wasomi na viongozi wa dini, wamepongeza uteuzi wa Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge na Watu wenye ulemavu huku wakisema kwa uwezo na uzoefu wake viatu vya mtangulizi wake vitamtosha.
Wamesema matarajio yao makubwa ni kuona wizara hiyo ikiendelea kufanya vizuri zaidi, kutokana na uzoefu mkubwa wa uongozi alionao Profesa Kabudi.
Pongezi na ushauri huo unatokana na uteuzi uliofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, juzi, ambapo pamoja na viongozi wengine, alimteu Profesa Kabudi kushika nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na marehemu William Lukuvi.
Wakizungumza na UHURU kwa nyakati tofauti, jana, baadhi ya wadau hao walisema uteuzi wa Profesa Kabudi ni ishara ya imani kubwa aliyopewa kutokana na umahiri na uzoefu wake katika uongozi.
Mwanasiasa mkongwe nchini, Kapteni mstaafu John Chiligati, alisema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amefanya uamuzi sahihi kwa kumteua Profesa Kabudi kushika nafasi hiyo.
Alisema ofisi ya waziri mkuu ina umuhimu mkubwa katika uendeshaji wa shughuli za serikali hivyo, anahitajika kiongozi mwenye uzoefu mkubwa na anayejua vyema mifumo ya kiutendaji serikalini.
“Majukumu haya yanahitaji mtu mwenye uzoefu mkubwa na anayeijua serikali vizuri, kwa vigezo hivyo, Profesa Kabudi anatosha, tunafahamu namna anavyotekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
“Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amepata mtu sahihi kwa nafasi hiyo, tunategemea kuona mambo mazuri ndani ya wizara hiyo, jambo la msingi ni kuendelea kufanya kazi kwa bidii siku zote,” alisema.
Katibu mstaafu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Kanali Ngemela Lubinga, alisema Profesa Kabudi ni mwanasiasa imara katika uongozi.
Alisema Profesa Kabudi ana uzoefu mkubwa wa kiutendaji katika uongozi na kubainisha kuwa ana matarajio makubwa kwamba kutokana na uwezo huo wizara hiyo itazidi kusimamia vyema majukumu yake.
“Kumteua Kabudi matumaini yetu ni makubwa sana, kutokana na uzoefu na ukomavu wake katika siasa na uongozi, tunaamini Rais Dk. Samia amefanya uamuzi sahihi na tumepata kiongozi mwingine ambaye atatekeleza majukumu yake kulingana na matarajio ya wananchi.
“Niwatoe hofu viongozi tunapaswa kujua kwamba, nafasi za uongozi siyo za mtu mmoja, bali ni za kupokezana vijiti kwa kuzingatia misingi ya kidemokrasia na mabadiliko hutokea kulingana na mahitaji ya wakati,” alisema.
Akieleza mtazamo wake, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Dk. Philip Daninga, alimshauri Profesa Kabudi aendelee kufanya kazi kwa uadilifu na weledi katika nafasi hiyo mpya ya uongozi.
Alifafanua kuwa, nidhamu uadilifu na ubunifu ni vitu muhimu vinavyohakikisha malengo ya wizara yanatimizwa, na kwamba kutokana na sifa na uzoefu wa Kabudi ana uwezo wa kuyatekeleza kwa ufanisi.
“Tulikuwa na majonzi makubwa kutokana na kuondokewa na kiongozi wetu Lukuvi ambaye tulimzoe na alikuwa na uzoefu mkubwa katika nafasi yake, Rais Dk. Samia amefanya vizuri kumteua Profesa Kabudi kumrithi Lukuvi.
Kwa upande wake, Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tabora, Dk. Joseph Isaya, alimtakia kila la heri Profesa Kabudi katika majukumu hayo mapya, huku akimhimiza kuendelea kusimamia haki, uwajibikaji na maslahi ya wananchi hususani makundi maalumu, likiwemo la watu wenye ulemavu.
Aprili 2, mwaka huu, Rais Dk. Samia alimteua Profesa Kabudi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), akichukua nafasi ya marehemu Lukuvi.
Taarifa kuhusu uteuzi huo iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka ilisema Rais Dk. Samia amefanya uteuzi wa Profesa Kabudi ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Ikulu (Kazi Maalumu).
Pia, taarifa hiyo ilisema Rais Dk. Samia ametengua uteuzi wa Dk. James Mwainyekule, ambaye alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na kwamba atapangiwa majukumu mengine.




