Na MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema hasita kumwondoa mganga mkuu wa mkoa au wilaya, ambaye atashindwa kutatua changamoto za wananchi katika eneo lake.
Mchengerwa alisema katika baadhi ya maeneo nchini, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi ya ukosefu wa dawa hatua ambayo haikubaliki.
Mchengerwa alisema hayo katika kikao kazi na wadau wa dawa na vifaatiba, kilichofanyika makao makuu ya Bohari ya Dawa (Msd) jijini Dar es Salaam.
Alisema mganga mkuu wa mkoa au wilaya ana jukumu la kuhakikisha changamoto zote katika maeneo yao yamepatiwa majibu kuliko kusubiri viongozi wa ngazi za juu kuzitatua.
Mchengerwa alisema hatakubali kuona malalamiko ya wananchi yakiendelea kujitokeza licha ya serikali kuweka mifumo bora ya upatikanaji wa dawa katika hospitali, vituo vya afya na zahanati.
Alisema waganga wa mikoa na wilaya wana nafasi nzuri ya kutatua changamoto zilizopo chini yao, hivyo hatakubali kusikia kuna baadhi ya maeneo kuna ukosefu wa dawa.
Alisema hataki kusikia maswali madogo kutoka kwa wananchi ambayo waganga wa mikoa ya wilaya wana uwezo wa kutatua kuliko kusubiri wizara au wataalamu wapatie ufumbuzi changamoto hizo.
“Nataka kuwaleza ukweli baada ya kikao hiki sitegemei kusikia mwananchi akilalamikia changamoto ambazo viongozi mna uwezo wa kuzipatia majibu, kama kutakuwa na changamoto zikiendelea tutachukua hatua
“Kwa mujibu wa taratibu za uteuzi wenu kama kuna kiongozi atashindwa kutatua changamoto katika eneo lake tutamuweka kando kwa mujibu wa taratibu, Watanzania hawataki maneno maneno, wanataka dawa
“Ukipewa nafasi fanya kazi, nikiangalia hapa viongozi wengi ni vijana, ukipewa nafasi onyesha uwezo wako, natambua kuna baadhi ya maeneo kuna ufinyu wa bajeti lakini sikuwahi kusikia malalamiko ya dawa, kuna maeneo tunafanya vizuri na kuna maeneo hatufanyi vizuri,”alisema Mchengerwa.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kutoa fedha nyingi za ununuzi wa dawa, lakini baadhi ya maeneo hayafanyi vizuri na wananchi wameendelea kutoa malalamiko.
Mchengerwa alisema wajibu wa serikali ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora katika maisha yao ya kila siku, hivyo ni muhimu takwimu ziendane na utoaji mzuri wa huduma.
Waziri huyo aliwataka viongozi hao kuweka uwiano mzuri kati ya takwimu na uhalisia wa huduma inayotolewa kwa mwananchi, hivyo alisema ni muhimu kila mmoja kutimiza wajibu wake.
Katika kikao hicho, Mchengerwa alizungumza na wananchi ambapo walipiga simu kuuliza masuala mbalimbali katika sekta ya afya na wataalamu wakiongozwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Magembe, walitoa majibu.
Naibu Waziri TAMISEMI
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshughulikia afya, Dk. Jafar Seif, alisema serikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaatiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya unaimarika.
Alisema katika mwaka wa fedha 2024-2025, serikali ilitenga zaidi ya sh. bilioni 128 kwa ununuzi wa dawa na vifaatiba kupitia Bohari ya Dawa (Msd) na mifumo mingine ya ugavi.
Alisema katika mwaka wa fedha 2025-2026, serikali iliongeza bajeti na kufikia takriban sh. bilioni 250 ikiwa ni sehemu ya kuimarisha huduma ya afya kwa wananchi.
Pia, alisema vituo vya kutolea huduma za afya ngazi za msingi nchini, vimeendelea na ukusanyaji wa mapato kutoka katika vyanzo mbalimbali.
“Haya yote anayafanya Dk. Samia Suluhu Hassan chini ya maelekezo yake na ile kauli ya Kazi na Utu,”alisema Naibu Waziri huyo.
Dk. Seif alisema katika mwaka wa fedha 2024-2025 vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi, vilikusanya takriban sh. bilioni 108 na makusanyo yanatarajiwa kuongezeka na kufikia sh. bilioni 192 katika mwaka huu wa fedha.
Mganga Mkuu wa Serikali
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Magembe, alisema hospitali za wilaya nchini, zimeanza kupima wagonjwa wa sikoseli.
Dk. Magembe alisema zamani wagonjwa wa sikoseli walikuwa wakipata matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), lakini hivi sasa hospitali za wilaya zinatoa matibabu.
“Sikoseli ni ugonjwa adimu, upatikanaji wake wa dawa ni adimu, lakini hivi sasa Chuo chetu cha Muhimbili MUHAS wameanza kuona namna kutengeneza dawa hizi na bei yake itaendelea kushuka,”alisema Dk. Magembe.
Aidha, Dk. Magembe alitoa wito kwa wananchi kuacha kutumia dawa zilizomalizika muda wake, kwa kuwa ni sumu na zimekuwa na madhara makubwa kwa binadamu.
Akizungumzia dawa kumalizika muda wake, alisema serikali ipo makini kuhakikisha dawa zote zisizofaa hazitumiki kwa binadamu, kwasababu zina madhara.
“Dawa kumalizika muda wake ni jambo la kawaida duniani kote, lakini serikali tumeendelea kuchukua hatua kudhibiti dawa zilizomalizika muda wake, hatuwezi kutumia dawa ambazo zimeisha muda wake, tumekula kiapo,”alisema Dk. Magembe.
Daktari huyo alisema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya dawa, lengo ni kuhakikisha afya za Watanzania zinaendelea kuimarika.




