Na VICTOR MKUMBO
MASTAA wa klabu ya Yanga, wameibuka na kutaja kwamba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, bado upo wazi, lakini wamejipanga kupata ushindi katika mechi tano zilizobaki ili kuchukua tena taji hilo.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga ipo kileleni ikiwa na alama 60, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 58 ambapo timu zote zimecheza mechi 25 hadi hivi sasa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam, mastaa wa Yanga walisema kuwa kusema wao wametwaa taji hilo ni mapema kwani wana mechi tano na lolote linaweza kutokea.
Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alisema mbio za ubingwa bado zipo wazi, lakini Yanga wana nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo kwa mara nyingine msimu huu.
Alifafan ua kuwa anaamini hadi mwishoni mwa msimu huu watatangaza ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara nyingine.
Tshabalala alisisitiza kuwa Yanga imekuwa ikicheza kwa ushirikiano katika kila mechi kitu ambacho kimesababisha kupata matokeo chanya.
“Mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara bado zinaendelea na hadi muda huu, sisi tuna nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa.
“Tunaamini hadi kufikia mwishoni mwa msimu tutatangazazwa mabingwa wa michuano hii kwa mara nyingine,” alisema Tshabalala.
Kwa upande wake, Maxi Nzengeli alisema wataendelea kuhakikisha wanashinda katika mechi zote tano zilizobaki.
Hata hivyo, mchezaji huyo amekiri kuwepo kwa ushindani mkubwa wanaoupata kutoka kwa timu pinzani.
“Mechi zilizobaki hazitakuwa rahisi kwani kila timu itapambana kupata matokeo mazuri na sisi tutahakikisha tunafanya vizuri,” alisema.
Nzengeli alisema wachezaji wote wameahidi kuendelea kupambana kuhakikisha timu inabakia katika kilele cha ligi hiyo.
“Tutaendelea kupambana kuhakikisha tunazilinda pointi mbili zilizopo japokuwa mechi tano zilizobakia hazitakuwa rahisi.
“Kila timu imekuwa ikipambana kupata matokeo mazuri, tunaendelea kuhamasishana mazoezini kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea,” alisema Maxi.
Naye Bakari Mwamnyeto alisisitiza kwamba ligi hiyo ni ngumu lakini wamejipanga kusikiliza maelekezo ya benchi la ufundi na kuhamishia wanafuata ili kupata ushindi.
Pia, alisema mashabiki wamekuwa wakiwapa hamasa kwa kufika kwa wingi viwanjani, hivyo wachezaji hawana cha kuwalipa zaidi ya kuwapa furaha ya ushindi.
“Ligi ni ngumu kwa hapa ilipofikia kwani kila timu imebakisha mechi tano na kila mmoja anapambana kutaka kutimiza malengo aliyojiwekea.
“Tunawaomba mashabiki waendelee kutusapoti kwa kujitokeza kwa wingi uwanjani na kutupa hamasa zaidi kuhakikisha tunatetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu,” alisema Mwamnyeto.




