Na SELINA MATHEW, Dodoma
WABUNGE wameitaka serikali kuongeza uwekezaji katika sekta za uzalishaji, kukuza uchumi na kuongeza ajira, huku wakionya kuchezea amani na utulivu wa nchi ambao ni msingi muhimu wa kufanikisha utekelezaji wa bajeti kuu ya serikali ya mwaka wa fedha 2026/27.
MBUNGE WA SINGIDA MASHARIKI
Akichangia bajeti hiyo bungeni, jijini Dodoma, Mbunge wa Singida Mashariki, Elibariki Kingu, aliipongeza serikali kuandaa bajeti inayolenga kukuza uchumi wa taifa na kuongeza kipato kwa kila mwananchi, akisema hatua hiyo, inaonesha dhamira ya dhati ya kujenga uchumi unaojitegemea.
Alishauri serikali kupunguza matumizi yasiyo ya lazima katika shughuli za kawaida, hususani ununuzi wa magari na gharama nyingine za uendeshaji ili fedha zielekezwe katika sekta za uzalishaji kama kilimo, viwanda, uvuvi na usafirishaji.
Alisema fedha zitakazookolewa kupitia hatua hiyo, zitasaidia kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha mchango wa sekta za uzalishaji katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Pia, aliitaka serikali kuimarisha uratibu kati ya taasisi za uwekezaji, mipango na sekta za uzalishaji ili wawekezaji wanaokuja nchini, waendane na vipaumbele vya maendeleo vilivyowekwa na taifa.
Aidha, alieleza wasiwasi wake kuhusu pendekezo la kuharakisha malipo ya marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ndani ya siku 30 na kutoza riba kwa serikali endapo itachelewa kulipa.
Alisema hatua hiyo, inaweza kuongeza mzigo mkubwa wa kifedha kwa serikali.
Pia, Kingu alisifu uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya, akisema uboreshaji wa hospitali na upatikanaji wa vifaatiba vya kisasa, vimeongeza ubora wa huduma kwa wananchi na kupunguza utegemezi wa matibabu nje ya nchi.
Kingu aliwataka wanasiasa kuacha kuwahamasisha wananchi kufanya vurugu na maandamano yanayoweza kuvuruga shughuli za maendeleo na kuathiri mazingira ya uwekezaji nchini.
Alisema Tanzania imeendelea kunufaika na amani na mshikamano wa kitaifa muda mrefu, hivyo ni wajibu wa viongozi wote wa kisiasa kuhakikisha hali hiyo inalindwa ili utekelezaji wa miradi ya maendeleo na mipango ya uchumi usikwame.
MBUNGE WA VWAWA
Kwa upande wake, Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga, alisema bajeti hiyo, imeonesha mafanikio makubwa ya serikali katika kuimarisha uchumi na kupunguza utegemezi wa mikopo ya nje.
Alisema kiwango cha mikopo ya nje, kimeendelea kushuka na kufikia asilimia 14 kutoka zaidi ya asilimia 40 katika miaka iliyopita, jambo alilosema linaashiria kuimarika kwa mapato ya ndani na usimamizi wa fedha za umma.
Hasunga, alisema hatua hiyo ni ishara kuwa Tanzania inaendelea kuelekea katika uchumi unaojitegemea, huku akisisitiza kuwa sekta za uzalishaji zinapaswa kupewa kipaumbele kikubwa zaidi ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.
Alitaja sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, madini, utalii na viwanda kuwa nguzo muhimu za uchumi ambazo zikiwekewa mazingira bora zinaweza kuongeza mapato ya taifa na kutoa ajira kwa maelfu ya wananchi.
Mbunge huyo, alisisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa nchini kupitia viwanda vya ndani badala ya kuuza malighafi ghafi, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa.
Pia, aliitaka Serikali kuendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo reli ya kisasa, bandari na viwanja vya ndege ili kuimarisha biashara na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
MBUNGE WA MULEBA KASKAZINI
Naye Mbunge wa Muleba Kaskazini, Oscar Kikoyo, alisema Tanzania ina rasilimali za kutosha zinazoweza kuiwezesha kugharamia bajeti kubwa zaidi iwapo mfumo wa ukusanyaji wa mapato utaimarishwa na wananchi wengi zaidi kuingizwa katika mfumo wa ulipaji kodi.
Kikoyo alisema badala ya kutegemea nguvu kubwa katika ukusanyaji wa kodi, serikali inapaswa kuwekeza zaidi katika elimu kwa wananchi na wafanyabiashara ili kuwajengea uelewa wa umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari.



