Na WARIOBA IGOMBE
UBUNIFU ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya kiuchumi katika kipindi hiki cha kidijitali.
Kwa mantiki hiyo, serikali duniani kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa chini ya Umoja wa Mataifa UN, zimekuwa zikisisitiza na kushirikiana katika kutambua umuhimu wa ubunifu na kuujengea mazingira mazuri ya kuzalisha wataalamu.
Ifahamike kuwa ubunifu ni uwezo wa kuunda kitu kipya au kupata njia mpya ya kutatua changamoto.
Wabunifu mbalimbali wamekuwa wakitumia bunifu zao kujipatia kupato, hivyo kujiimarisha kiuchumi na kuondokana na umasikini.
Ubunifu wa aina yoyote, unawasaidia wabunifu kutoka katika hali yao ya kimaisha na kujiimarisha kiuchumi.
Idd Juma Kilongola ni mkazi wa Manispaa ya Morogoro, ambaye ni mbunifu hodari wa mitego ya panya.
Mbunifu huyo, anazungumza na gazeti hili, alivyoamua kuachana na kazi yake ya utingo na kuwa mtengenezaji wa mitego ya kudhibiti wanyama waharibifu shamabini, ikiwemo panya, hali ambayo imempa mafanikio makubwa ikiwemo kujenga nyumba.
“Awali nilikua nafanya kazi ya kushusha na kupakia mizigo katika malori ya mizigo nikiwa kama utingo, huku nikilipwa sh. 1,000 kwa kutwa, kazi ambayo ilinipa mtaji nikaanza kuuza mitego na sumu ya panya mitaani ambayo ilikuwa ikitoka nje ya nchi,” alisema Kilongola.
Mbunifu Kilongola anayeendesha maisha kwa kipaji chake cha kutengeneza mitego ya panya, anasema anajivunia kazi hiyo licha ya kutokwenda shule.
Alieleza kuwa akiwa katika kazi yake ya kuuza mitego ya panya iliyotengenezwa kutoka nje ya nchi, baadhi ya wateja wake walikuwa wakilalamika kuwa mitego hiyo inawahi kuchakaa kwa kutu jambo lililogeuka kuwa changamoto kubwa kwake.
Aliongeza kuwa baada ya kuona malalamiko hayo yamekuwa mengi, aliamua kuja na ujuzi huo wa kutengeneza mitego ya panya kuondoa malalamiko ya wateja wake ndipo wazo la ubunifu wa kutengeneza mitego hiyo ilipomjia na kuanza rasmi kutengeneza.
“Nilianza kwa mtaji wa sh. 5,000 nikiwa na uwezo wa kutengeneza mitego mitano tu kwa siku ambapo mtego mmoja nilikuwa nauza kwa sh. 2,500, hali iliyonifanya niwe na wateja wengi ambao walipenda kazi yangu na kuniamini,” alisema.
Kilongola mwenye umri wa miaka 41, alisema kazi ya mitego ya panya alianza mwaka 2007, kutokana na ubunifu huo, amefanikiwa kuondoa malalamiko ya wateja wake tofauti na hapo awali alikuwa akiuza mitego ya awali ya kichina mitaani.
Alisema baada ya kuwa mkongwe katika kazi hiyo amejizoea umaarufu maeneo mbalimbali ya mkoa wa Morogoro na kwamba watu wengi wameachana na mitego ya kichina na wameamua kununua mitego yake.
“Kwa siku nina uwezo wa kutengeneza mitego kuanzia 25 hadi 30 na kupata sh. 62,500 kwa mwezi huwa napata fedha nyingi na kuendesha maisha yangu vizuri,” alisema Kilongola.
Alisema hakuwahi kutegemea kuwa angekuwa fundi mbobevu wa mitego ya panya, kwa sababu ya kukosa fursa ya kwenda shule, aliamua kupambana kuhakikisha anaondoka na umaskini .
“Sikufanikiwa kwenda shule, sijui kusoma na kuandika nimetumia ujanja tu, niweze kuwasiliana na wateja wangu kwani wapo wanaonitafuta kwa simu, hivyo ilinilazimu kujua kusoma na kuandika iwe rahisi kutekeleza majukumu haya,” alisema Kilongola.
Malengo yake
Alisema malengo yake ni kumiliki kiwanda cha mitego ya panya, kuhakikisha watu wote nchini wanatumia bidhaa zake za ndani na kuepuka kunufaisha mataifa ya nje kwa kununua vitu kinachoweza kutengenezwa nchini.
Kilongola alisema mbali na mitego ya panya, amekuwa akitengeneza mitego ya kukamata wanyama waharibifu hasa maeneo ya mashambani, ambapo wakulima wengi wamekua wakimtafuta na kuinunua kudhibiti wanyama hao.
Kilongola mwenye mke mmoja na watoto watatu, alisema kutokana na ubunifu wa kazi yake hiyo fedha ambazo anazipata zimemwezesha kujenga nyumba yenye vyumba vitano,huku familia yake ikiishi maisha mazuri.
“Kuzaliwa maskini ni kawaida ila kufa maskini ni kujitakia, mbali na kwamba nimelelewa na mzazi mmoja wa kike pekee na sikuweza kwenda shule hata siku moja lakini mtu akiniona hawezi kuamini ninachokisema,” alisema Kilongola.
Ufunifu wake wamkutanisha na viongozi
Alisema baada ya kazi yake hiyo kuwa bora, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), kimemchukua kwa kutengeneza mitego ya panya, ambapo wanafunzi wa chuo hicho huitumia kujifunzia na kufanya tafiti zao mbalimbali.
Alieleza kitendo hicho, kimemwezesha kupata fedha na kupata fursa ya kuweza kukutana na viongozi mbalimbali wa serikali, akiwemo Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kitendo ambacho anakiona kwamba ubunifu wake wa mitego ya panya na wanyama wengine waharibifu umekuwa neema kwake.
Alisema mbali na kutengeneza mitego ya panya pia hutengeneza mitego ya wanyama waharibifu shambani, ambapo watu wengi hususan wakulima huinunua na kuweka mashambani mwao kuwadhibiti wanyama.
SUA yazungumza
Dk. Martine John ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kudhibiti Viumbe hai Waharibifu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo(SUA),alisema ubunifu wa Kilongola umeleta tija na umepunguza gharama wa uagizaji wa mitego nje ya nchi.
Alisema chuo hicho kimekuwa kikiwakamata panya kwa ajili ya majaribio ya wanafunzi, kufanya tafiti mbalimbali na kwamba awali walikuwa wanatumia gharama kubwa kuagiza mitego kutoka nje ya nchi.
“Nampongeza sana kijana huyu kwani mbali na kujipatia kipato kupitia ubunifu wake, pia Taasisi ya Kudhibiti Viumbe hai Waharibifu Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), inajivunia ubunifu wake kwani mitego yake imesaidia kupungua gharama zilizokuwa zikitumika kuagiza mitego ya nanma hii nje ya nchi,” alisema John.
Alitoa wito kwa vijana wabuniufu nchini kuacha kujificha na badaala yake wajitokeze kuonesha vipaji vyao, jamii iweze kuwatambua kwa maslahi mapana yao na taifa nzima.
Dira ya Taifa ya Maendeleo
Kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ifikapo mwaka 2050 kila mwananchi awe na uwezo wa kupata wastani wa dola za Kimarekani 7,000 kwa siku, hivyo kitendo cha kijana huyo mbunifu ni njia nzuri ya kufikia azma ya dira hiyo.
Aidha, Sera ya Maendeleo ya Vijana ni Dira katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya vijana nchini, hivyo uwepo wa sera inayotekeleza inahitaji ushiriki na ushirikishwaji wa vijana wote katika ngazi zote mjini na vijijini.
Mkakati wa utekelezaji wa sera ya kimaendeleo kwa vijana umeainisha bayana majukumu ya kila mdau katika kufanikisha sera ya maendeleo ya vijana na muda wa utekelezaji, kuwezeshwa kufikiwa kwa lengo la vijana nchini katika nyaja mbalimali.
Wizara ya Viwanda na Biashara
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Denis Londo mbali na kupongeza ubunifu wa kijana huyo, anatoa wito kwa vijana nchini kuhakikisha wanakuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu sera ya maendeleo kama dira inayoongoza maisha yao ili kuhakikisha wanajikwamua kiuchumi na kuondokana na wimbi la umaskini .
Londo alisema katika kipindi hiki cha ukuaji wa sayansi na teknolojia vijana wanawajibika kuchukua majukumu yao kama viongozi wa leo na kesho ili waweze uleta maendeleo.
Alisema vijana wanatakiwa kutumia vipaji vyao ikiwemo ubunifu kuleta mawazo mapya kuendelea na shughuli zao na mwendelezo wa dira kama vile dira ya taifa 2050 inayohusu mkakati kuondoa umaskini.
VETA Kihonda
Naye Mkuu wa Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA), Kihonda kilichopo Manispaa ya Morogoro, Salumu Ulimwengu, alisema chuo chao kinahusika na ujuzi wa aina mbalimbali kwa vijana wakiwemo wabunifu ambao wamekuwa wakiwafundisha kuendeleza fani zao.
“Kwa hiyo sisi kama VETA tunawakaribisha vijana wenye ubunfu kama huo wa mitego ya panya kuja kujifunza zaidi, kwani kutawaongezea ujuzi na maarifa zaidi hali itakayowasaidia kufahamika kila kona ya nchi hii,”alisema Ulimwengu.
Alisema chuo hicho kimekua kikiwapokea vijana wabunifu na kukaa nao ili kuona ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia kuwaendeleza zaidi ambapo VETA huendeleza kipaji hicho na kwamba kipaji hupanuka zaidi na kuweza kufanya vitu vizuri zaidi hivyo kijana mbunifu kuona matunda mazuri ya kazi yake hiyo.
Mkuu huyo anatoa wito kwa vijana wote hapa nchini hasa wabunifu kuwa Veta ipo kwa ajili yao hivyo wanatakiwa kwenda Veta ili kukuza fani za vipaji vyao kwani kuwasaida kujulikana zaidi duniani na uchumi wao utazidi kuimalika.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) mkoani Morogoro, Joan Nangawe, alisema wao kama SIDO wana jukumu la kuwasaidia wajasiliamali katika maeneo makuu manne.
Alitaja maeneo hayo ni pamoja na teknolojia,mafunzo,masoko na mitaji na kwamba katika eneo la teknolojia SIDO huangalia masuala ya ubunifu na namna gani vijana wanaweza kutumia teknolojia hizo katika ubunifu mbalimbali.
Alisema kuwa SIDO imekuwa ikitoa ushirikiano kwa ubunifu ili kuwatia moyo ikiwa ni pamoja na kuendeleza kuwashauri bidhaa hizo ziwe na tija kwa maslahi na upana wa taifa,
Aidha, alimpongeza Kilongola kijana aliyebuni mitego ya panya ambapo amewataka vijana wengine kuiga mfano huo kwa kuonesha ubuifu wao, SIDO itaendelea kuwapa ushurikiano kutimiza azma zao.
COSTECH
Dk. Amos Nungu ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), alisema ubunifu umesaidia kutekelezwa kwa mpango wa kutekeleza mpango wa maendeleo kitaifa na hata kusaidia vijana wengi kujiajiri wenyewe.
Dk. Nungu alipongeza jitihada za serikali katika kuhamasisha na kuendeleza ubunifu nchini ambapo ameeleza kuwa mwitikio wa Watanzania katika kipindi hiki umeongezeka kwa kiwango kikubwa na kusema kwamba serikali imekuwa ikitoa mazingira wezeshi kwa wabunifu hatua ambayo imechangia kuibua bunifu nyingi zinazowasaidia wananchi.
“Vijana wetu wabunifu wanatakiwa kuhakikisha teknolojia na bidhaa wanazozizalisha zinatatua changamoto za jamii na kuwa na uwezo wa kuingiza fedha ili wakopesheke na kuwawezesha kurejesha mikipo hiyo,”alisema Dk. Nungu.
Aidha, Mkurugenzi huyo amewataka vijana wabunifu akiwemo Kilongola, ambaye ni mbunifu wa mitego ya panya na wanyama waharibifu wa mazao shambani kuhakikisha wanakuwa haki miliki ili kuwawezesha kuwa na uhalali wa kulinda kazi zao za ubunifu.
Dk. Nangu alisema COSTECH itaendelea kuwawezesha na kuendeleza bunifu za vijana ili kazi zao ziweze kupanuka na kufahamika zaidi kwa manufaa ya wabunifu wao wenyewe na taifa kwa ujumla.
Wateja
Wateja wa mitego hii ya panya wakiwemo wafanyabiashara wanasema mitego hiyo ina sifa mbalimbali ikiwemo kudumu muda mrefu bila kuchakaa kama ilivyo kwa mitego ya kichina ambapo wamempongeza mbunifu huyo kwa ubunifu wake.
Amos Abel ni miongoni mwa wateja hao mbali na kumpongeza mbunifu huyo, ameiomba serikali kuangalia namna ya kumwezesha zaidi Kilongola ili mitego hiyo iweze kusambaa maeneo mbalimbali nchini hususan kwa wakulima ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya wanyama kuharibu mazao yao shambani.




