NA MWANDISHI WETU, Dodoma
SERIKALI imeanza uchunguzi dhidi ya baadhi ya Maofisa Rasilimali Watu maarufu kama Ma – HR, wanaodaiwa kutumia namba za malipo ya mishahara (cheque number) za watumishi wa umma, kuomba mikopo binafsi kinyume cha sheria.
Hayo yalisemwa jijini hapa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, alipofungua mafunzo ya maofisa rasilimali watu na wahasibu kutoka wizara na taasisi za umma.
Alisema uchunguzi huo, unaendelea kubaini ukweli wa tuhuma hizo na watakaobainika, wanachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria, kanuni na utaratibu.
“Matumizi ya mifumo na taarifa za kiutumishi, yanapaswa kufanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, akiwataka maofisa wanaotumia taarifa hizo kwa maslahi binafsi, kuacha mara moja.
Aliongeza; “Tunachunguza mnyororo huu kubaini ukweli na kama kuna mtu amehusika, hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa taratibu”.
Katika hatua nyingine, Mkomi alitoa wito kwa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), kuangalia namna ya kuongeza wigo wa fidia kwa wafanyakazi wanaopata madhara mengine wakiwa kazini, yakiwemo matatizo ya kiafya kama presha.
Aidha, aliwaonya waajiri wanaowatelekeza watumishi wanapopata madhara au kuugua wakiwa kazini bila kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dk. John Mduma, alisema wameweka mkakati wa kuhakikisha wahasibu wanafuatilia na kuhakikisha michango ya watumishi inawasilishwa kwa wakati.
Dk. Mduma, alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha haki za wafanyakazi zinalindwa na wanapata huduma na stahiki zao kwa wakati wanapopata madhara yanayotokana na kazi.




