NASRA KITANA Na ZIANA BAKARI
WIZARA ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo imepiga marufuku Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kutumika kwa mazoezi ya timu za Simba na Yanga.
Pia, imeeleza uwanja huo upo tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya timu hizo maarufu ‘Dabi ya Kariakoo’, utakaopigwa kesho .
Simba ambao ndio wenyeji wa mchezo huo watashuka dimbani kesho katika mchezo namba 56 wa mzunguko wa saba wa ligi hiyo utakaoanza saa 1:00 usiku.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kaimu Mkuu kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Zaituni Mkwama alisema pamoja na kuruhusu uwanja huo kutumika katika mchezo huo wa dabi, amesisitiza kuwa uwanja huo hautatumika kwa mazoezi na timu yoyote kati ya hizo mbili.
Zaituni alisema kuelekea mchezo huo,kanuni na taratibu zilizowekwa na Bodi ya Ligi kuhusu matumizi ya uwanja wa mashindano, hususani masuala yanayohusu mazoezi ya timu, zizingatiwe kikamilifu.
“Tunapenda kuwafahamisha kwamba kuelekea mchezo huo Uwanja wa Uhuru hautatumika kwa mazoezi na timu yoyote kati ya hizo mbili, kwa kuzingatia matakwa ya kifungu husika cha kanuni za mashindano ya ligi.”
“Tunawaomba wadau wote, mashabiki wa Simba na Yanga, pamoja na umma kwa ujumla, kuzingatia utulivu, amani na taratibu zilizowekwa kuelekea mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na Watanzania wote,” alisema Zaituni.
Kaimu Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Yahya Abushehe alisema taarifa hiyo wameiona ila wamekuwa na vikao na wadau mbalimbali wanaohusika na mchezo huo kuhakikisha kila upande unazingatia taratibu zilizowekwa, pamoja na kushirikiana na Simba ambayo ni mwenyeji wa mchezo huo.
Abushehe alisema wamekuwa wanafanya vikao hivyo ili kuhakikisha kunakuwa na umakini kuelekea siku ya mchezo huo.
“Bodi imekuwa ikiendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa soka pamoja na klabu kuhakikisha kanuni na taratibu zinafuatwa hivyo kila timu itatekeleza wajibu wake,” alisema Abushehe.
Ikumbukwe Machi 8, 2025 Simba iligomea mchezo dhidi ya Yanga baada ya kushindwa kufanya mazoezi siku moja kabla ya mchezo huo uliopangwa kuchezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Baada ya hapo mechi hiyo ilichezwa Juni 15, 2025 katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na Simba kukubali kichapo cha mabao 2-0.
Katika hatua nyingine, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imetangaza kuimarisha ulinzi na usalama katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara, italozikutanisha Simba na Yanga.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Faustine Mafwele, alisema wamejipanga kuhakikisha usalama wa mashabiki na mali zao utakuwepo kabla na baada ya mchezo.
“Jeshi la Polisi linatambua uwepo wa mchezo huo ambao huvutia idadi kubwa ya mashabiki hivyo ulinzi umeimarishwa kwa kushirikiana na wadau na kuhakikisha mashabiki wanaingia na kutoka uwanjani wakiwa salama.
“Niwasihi sana mashabiki na wadau wa soka kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyokiuka sheria kabla, wakati na baada ya mchezo huo,” alisema Mafwele.
Pia, Mafwele aliwataka mashabiki kuutumia mchezo huo kama sehemu ya burudani na ushindani wa michezo kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, kuhakikisha unamalizika kwa amani na utulivu.




