Na SOPHIA ASHERY
SIKU moja kabla ya fainali za ‘Miss Grand International 2026 (MGM), wadau wa urembo wamemtabiria ushindi, Miss Grand Tanzania, Jihan Dimark.
Fainali za MGM 2026, zinatarajiwa kufanyika kesho jijini Bangkok, Thailand, kwa kushirikisha warembo 79, kutoka nchi mbalimbali duniani.
Jihan, Miss Tanzania 2016, juzi usiku alitwaa mataji mawili, katika vipengele viwili tofauti, katika shindano dogo lililoshirikisha warembo wote wanaoshiriki shindano hilo.
Mlimbwende huyo, anayepewa nafasi kubwa ya kutwaa taji kuu, alishinda taji la chaguo la mashabiki na mrembo mwenye mvuto zaidi.
Ushindi wa tuzo hizo, umezidi kumsafishia njia Jihan na kumuweka katika nafasi nzuri ya kushinda taji.
Pamoja na tuzo hizo, mrembo huyo anaongoza kwa kupata kura nyingi katika kipengele cha nchi yenye nguvu katika upigaji kura kwa mlimbwende wake, akichuana vikali na Miss Grand Equador, Shyare Andrade, hadi jana jioni, kabla ya zoezi la kupiga kura kufungwa usiku na mshindi kutangazwa leo alfajiri, Jihan alikuwa akiongoza kwa pointi milioni 27.289 dhidi ya milioni 18.366.
Akizungumza na gazeti hili, Ofisa Itifaki kutoka kamati ya Miss Tanzania, Hidan Rico, alisema Jihan ana nafasi kubwa ya kushinda taji kutokana na mvuto wake.
Rico alisema, kujiamini kwa Jihan, kuvaa mavazi yenye mvuto, nidhamu, uhusiano na washiriki wenzake, umbo na idadi kubwa ya kura na mashabiki, vimeiweka Tanzania katika nafasi nzuri.
Alisema na Jihan kuongoza, Watanzania wanapaswa kuendelea kupiga kura kwa wingi na kumuongezea mrembo nafasi ya kushinda taji.
Mwanamitindo Miriam Odemba alisema Watanzania ni watu wenye upendo, umoja na wamekuwa wakimuunga mkono mrembo wao tangu siku ya kwanza ya shindano, ndio maana bendera ya Tanzania inazidi kupepea.
Miriam alisema idadi kubwa ya kura zinazopigwa na Watanzania, kutoka sehemu mbalimbali duniani, zinaendelea kumuweka Jihan katika nafasi nzuri zaidi ya kubeba tuzo na kuwaomba kuendelea kupiga kura bila kuchoka.
Mbunifu wa mitindo, Mustafa Hassanal alisema hadi sasa anaamini kuwa Tanzania ina asilimia 95 ya kushinda.
Hassanal alisema tuzo alizopata Jihan hadi sasa, alama za awali anazopewa na majaji tayari zimeonesha kuwa mlimbwende huyo anaweza kuisimamisha dunia.
Hadi sasa, Jihan amebeba tuzo tatu huku vazi la ubunifu lililoonesha utajiri, historia, utamaduni, hazina ya madini yaliyopo nchini ikiwemo Tanzanite, urithi na utalii wa Zanzibar, na kulifanya vazi hilo kutajwa kuwa vazi bora la ubunifu MGM 2026.
Pamoja na Jihan, baadhi ya warembo wanaowania taji hilo ni Sara Shehu (Albania), Amest Aretunian (Armenia|), Cat Jane Sherpherd (Australia), Anonna Fatima (Bangladesh), Emily Baesen (Ubelgiji), Kaithlain Da Rocha (Bolvia|), Paula Ansuacao (Brazil) na Patricia Seward (Canada).
Wengine ni Ignacia Micheleson (Chile), Liu Mengmeng (China), Hana Dedkova (Jamhuri ya Czech), Keith Familia (Jamhuri ya Domonica), Shyare Andrade (Equador), Menna Elbatran (Misri), Valeria Amaya (El Salvado) na Axelle Valin (Ufaransa).
Pia wamo Adelaide Twum (Ghana), Estaphenie Charles (Haiti), Yolanda Liu (Hongkong), Lakshita Thiragalaj (India), Dilza Salsabila (Indonesia), Tanin Alemi (Iran), Angelica Marzial (Italia), Somone Gardner (Jamaica), Sara Chiba (Japan) na Alba Fazlija (Kosovo).



