Na Mussa Yusuph,
Lindi
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema utekelezaji wa mradi wa gesi ya LNG unaotarajiwa kufanyika mkoani Lindi ni ukombozi wa kiuchumi katika mkoa huo na Taifa.
Kutokana na hilo, Majaliwa ametoa wito kwa wananchi mkoani Lindi kumpigia kura Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan akamilishe taratibu zilizobaki kutekeleza mradi huo wa kimkakati.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi, Majaliwa alisisitiza kwamba mradi huo umewekwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030, jambo linaloonesha dhamira ya Chama kuhakikisha wananchi wa Lindi na Watanzania wananufaika.
“Ilani hii inakuja kutukomboa na kufungua milango ya mkoa wetu. Mradi mkubwa wa LNG unakuja kutekelezwa hapa Lindi. Kwa kuwa utekelezaji huu upo kwenye Ilani ya CCM 2025–30, basi ni juu yetu wana Lindi kumpigia kura, Dk. Samia ili akamilishe taratibu zilizobaki,” alisema.
Akizungumzia ujenzi wa kiwanja cha ndege katika mkoa huo, alisema uwanja huo utakuwa wa kisasa wenye uwezo wa kuhudumia ndege mbalimbali.
“Kiwanja chetu cha ndege kina njia kuu tatu tofauti na viwanja vyote vya ndege Tanzania. Unaweza kutua kutoka popote, jambo linalokwenda sambamba na mradi unaokuja wa LNG. Ilani hii inakuja kutukomboa na kufungua milango ya mkoa wetu,” alisema.
Alibainisha kuwa ilani hiyo pia inatilia mkazo uhifadhi wa mazingira kwa kujenga ukuta maalumu utakaosaidia kuzuia mmomonyoko katika fukwe za Lindi.