Na NASRA KITANA
KAIMU Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Miguel Gamondi amemrejesha nyota wa Aalborg BK ya Denmark, Kelvin John, katika kikosi cha timu hiyo kitakachoingia kambini kujiandaa na mechi ya kirafiki kalenda ya FIFA dhidi ya Kuwait.
Pambano hilo, limepangwa kufanyika Novemba 14 jijini Cairo nchini Misri.
Kelvin aliitwa mara ya mwisho na kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’, Machi 14, mwaka huu, wakati timu hiyo ikijiandaa na mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Morocco.
Tangu hapo hakuitwa tena, licha ya kuanza vizuri msimu wa 2025/26 akiwa na kikosi cha Aalborg BK kinachoshiriki Ligi Daraja la Kwanza huko Denmark ambapo ni msimu wake wa pili mfululizo.
Chini ya Gamondi, mshambuliaji huyo ameitwa kwa mara nyingine tena akiwa mhimili mkubwa wa safu ya ushambuliaji ya Aalborg, akifunga mabao saba na kutoa ‘asisti’ tatu katika mechi 15 alizocheza.
Kelvin ameitwa huku nahodha wa Stars, Mbwana Samatta anayekipiga Le Havre ya Ligi Kuu Ufaransa na Simon Msuva wa Al Talaba wa Iraq wakitoswa kama ilivyokuwa katika kikosi cha mwisho kilichocheza mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Zambia.
Katika kikosi kilichotangzwa mapema asubuhi ya jana, kocha Gamondi amewaita makipa, Yakoub Suleiman (Simba), Hussein Masalanga (Singida BS) na Zuberi Foba wa Azam FC.
Wengine ni Bakari Mwamnyeto (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Mohamed Hussein (Yanga), Alphonce Mabula (Shamakhi, Azerbaijan), Feisal Salum (Azam FC), Morice Abraham (Simba), Abdul Suleiman (Azam FC) na Paul Peter wa JKT Tanzania.
Wengine ni Mudathir Yahya (Yanga), Wilson Nangu (Simba), Novatus Dismas (Göztepe FC, Uturuki), Pascal Msindo (Azam FC) na Ibrahim Abdulla wa Yanga.
Haji Mnoga (Salford City, Uingereza), Dickson Job (Yanga), Habibu Idd (Singida BS), Tarryn Allarakhia (Rochdale AFC, England), Charles M’Mombwa (Floriana FC, Malta) na Seleman Mwalimu kutoka Simba.
Gamondi ambaye ni Kocha Mkuu wa timu ya Singida Big Star, Novemba 4, mwaka huu, alitangazwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kukaimu nafasi iliyoachwa na Hemed Suleiman ‘Morocco’ aliyesitishiwa mkataba.
Kocha huyo atasaidiwa na Ahmad Ally ambaye anakinoa kikosi cha JKT Tanzania.




