MUSSA YUSUPH Na SELINA MATHEW,
Dodoma
LITAKUWA Bunge la haki na uwazi, hiyo ndiyo ahadi aliyoitoa Spika mpya wa Bunge, Mussa Zungu, baada ya wabunge kumchagua kwa kura za kishindo kuongoza mhimili huo.
Zungu ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ilala Mkoa wa Dar es Salaam, anakuwa Spika wa Bunge la 13 baada ya kupata kura 378 kati ya kura 383 akiwaacha mbali wapinzani wake, Veronica Tyeah wa Chama cha NFA, ambaye hakupata kura na Anitha Alfan wa Chama cha NLD aliyepata kura moja.
Wengine ni Ndoge Said wa AFP aliyepata kura moja na Amin Yango wa ADC, ambaye pia hakupata kura.
Baada ya kuapishwa, Zungu aliahidi kuliongoza Bunge kwa haki, uwazi na ushirikiano, akizingatia Katiba, Sheria na Kanuni za Kudumu za Bunge bila upendeleo kwa chama chochote chenye uwakilishi bungeni.
“Ingawa bado hatuna upande wa serikali, leo tunaye Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mheshimiwa Hamza Johari, niahidi kutoa ushirikiano kwa serikali, kwamba bunge tutashauri na kutoa maazimio kwa ustawi wa nchi na maendeleo endelevu,” aliahidi.
Pia, alimshukuru Spika mstaafu Dk. Tulia Ackson, kwa imani na ushirikiano aliompa katika masuala ya kibunge, akisema uzoefu huo utakuwa mwongozo muhimu katika kutekeleza majukumu yake mapya.
Wakizungumzia ushindi huo, Mbunge Mteule wa Manyoni, Dk. Pius Chaya, alisema kupitia uongozi wa Zungu, wanatarajia kuona Bunge jipya lenye umoja, kasi na viwango.
“Niseme tu, kwa umri wa Zungu na uzoefu wake ni dhahiri bunge limepata kiongozi na mlezi wa rika zote. Tumeshuhudia mabunge mengi pia duniani maspika ni walezi na ni watu wenye upeo na uzoefu mkubwa,” alibainisha.
Mbunge Mteule wa Hai, Saashisha Mafuwe, alisema bunge limepata spika wa viwango vinavyohitajika kuongoza, mwenye uzoefu mkubwa wa kumudu kanuni, miongozo na mila za bunge.
“Kupitia uongozi wa Zungu tutakuwa na bunge jumuishi, lenye sura ya Kitanzania, uwakilishi na huru ambalo litasimamiwa na mtu mwenye weledi mkubwa,”alisema Mafuwe.
Baada ya kukamilika uchaguzi huo, macho na masikio ya Watanzania yanaendelea kuelekezwa bungeni, ambako siku yoyote kuanzia leo kitendawili cha nani atakuwa waziri mkuu kitateguliwa.
Jina la atakayeshika wadhifa huo kurithi mikoba ya Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa, linatarajiwa kupelekwa bungeni kupitia Mpambe wa Rais (ADC), ambaye atakabidhi bahasha yenye jina la kiongozi huyo kwa Spika wa Bunge.
Baada ya spika kukabidhiwa, ataifungua bahasha na kusoma jina la kiongozi huyo, ambaye wabunge watampigia kura ya kumpitisha au la.
WAGOMBEA WALIVYOJINADI
Awali, akijinadi na kuomba kura, Zungu alisema akipewa ridhaa ya kuongoza atahakikisha analiunganisha bunge na wananchi.
“Serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa unyenyekevu mkuu imetoa dira ambayo inatakiwa kusimamiwa vizuri kusaidia ustawi wa jamii katika afya, miundombinu, elimu, amani na ulinzi wa taifa yaweze kutekelezwa kwa mafanikio makubwa,” alieleza Zungu.
Alisema bunge siyo vita baina yake na serikali au mahakama, bali kazi yake kubwa ni kufanya kazi kwa maslahi ya wananchi na siyo ya watu binafsi.
VERONICA TYEAH
Mgombea kutoka Chama cha National Recontruction Alliance (NRA) Veronica Tyeah, alisema kilichomfanya kugombea nafasi hiyo ni kuhakikisha bunge linaleta mabadiliko chanya.
“Nitaweka kambi rasmi ya majadiliano kubadili taifa liwe katika umoja na mshikamano, nitaweka kaulimbiu isemayo taifa kwanza vyama baadaye kuwa na taifa lenye usawa,” alisema Veronica.
Pia, alimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutokana na kuchaguliwa kwa kura nyingi za kishindo, huku akibainisha matokeo hayo ndiyo yamempa ujasiri wa kusimama bungeni na kuona anaweza kugombea nafasi hiyo.
Mgombea kutoka Chama cha National League for Democracy (NLD), Anitha Mgaya alisema iwapo angepata ridhaa hiyo malengo yake ni kujenga mshikamano, maelewano ndani na nje ya nchi.
Aidha, mgombea wa Chama cha Democratic Party (DP), Chrisant Nyakitita alisema alisukumwa kuwania kiti hicho kwa dhamira ya kushirikiana na wabunge kuisimamia serikali na kuishauri ikiwemo kupitisha bajeti.
“Nikipata ridhaa nitaligeuza bunge hili kuwa la maendeleo kupitia bajeti zitakazoletwa hapa,” alisema Nyakitita.
Mgombea kutoka Chama cha Alliance for Africa Farms Party (AAFP) Ndonge Said alisema akipewa ridhaa atainua zaidi vipato vya wabunge.
Pia, mgombea wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Amin Yango aliahidi kusimamia amani na usalama hususan kudhibiti wanaotaka kuhatarisha amani ya nchi.
“Ninakupongeza Dk. Samia kwa kazi nzuri unazofanya ninachokuomba chapa kazi kuwaletea maendeleo Watanzania, usirudi nyuma,” alisema Yango.
WASIFU WA ZUNGU
Mussa Azzan Zungu ni mwanasiasa mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye amehudumu bungeni kwa miaka 20 mfululizo.
Zungu amejipatia heshima kubwa kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu katika shughuli za bunge na utumishi wa umma.
Kitaaluma mwanasiasa huyo ni mhandisi wa ndege aliyepata mafunzo nchini Tanzania na Canada, akionesha umahiri katika taaluma ya kiufundi kabla ya kuingia katika siasa.
Mbali na kuwa mbunge, amekuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge kati ya mwaka 2016 na 2025 na amekuwa Mwenyekiti wa Bunge kati ya mwaka 2012 na 2021.
Pia, amekuwa Naibu Spika kati ya mwaka 2022 hadi 2025 kabla ya kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la 13.
Akiwa bungeni aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa zaidi ya miaka 16.
Zungu aliwahi kufanya kazi na maspika wanne tofauti, jambo linalompa uzoefu mkubwa wa kiutawala na kibunge.
Katika uongozi wa kimataifa, aliwahi kuwa kiongozi wa Bunge la Tanzania katika mikutano ya Umoja wa Mabunge ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (ACP) na Bunge la Umoja wa Ulaya (EU).
Vilevile, amekuwa kiongozi wa Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA-Tanzania Branch) na mwakilishi wake katika vikao vya kimataifa.
Ameshiriki ziara za mafunzo ya kibunge katika zaidi ya nchi 23, akijenga uelewa mpana wa mifumo ya mabunge duniani.
Kwa upande wa serikali, Zungu aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), nafasi iliyompa uzoefu katika masuala ya utawala wa serikali na ushirikiano wa Muungano.




