Na ATHNATH MKIRAMWENI
SERIKALI imetoa wito kwa sekta binafsi kujitokeza kwa wingi kuwekeza katika usafiri wa reli ya kisasa (SGR).
Pia, serikali imesisitiza kuongeza ushiriki wa wawekezaji, ndilo suluhisho la kuhakikisha mfumo huo, unakuwa endelevu na wenye tija kwa taifa.
Kauli hiyo, ilitolewa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alipotembelea maonesho ya kwanza ya wiki ya usafiri endelevu ardhini, yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja.
Alisema serikali inafungua mfumo wa ‘open access’ kuruhusu kampuni binafsi kuleta mabehewa na vichwa vya treni, hatua itakayoongeza ufanisi wa huduma na matumizi ya reli hiyo.
Alieleza ujenzi wa SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa upande wa nje, umekamilika kwa kiasi kikubwa, tayari safari za abiria, zimeanza kufanyika kwa mafanikio.
Profesa Mbarawa, alisema abiria wengi, wameridhishwa na huduma hiyo mpya, inachangia kwa kiasi kikubwa, mabadiliko katika sekta ya usafiri nchini.
Waziri huyo, alisisitiza ili reli hiyo itumike kwa saa 24 kama inavyokusudiwa, sekta binafsi zinapaswa kujumuishwa kikamilifu.
“Hatupaswi kuwa na treni inayosimama saa tano asubuhi hadi kesho saa 11. Tunataka treni ziendelee kupita muda wote,” alisema.
Alisema sekta binafsi, zinaweza kuwekeza katika mabehewa, vichwa vya treni na kuanza kutoa huduma za kusafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma na maeneo mengine.
“Tanzania inalenga kuwa na mfumo wa reli usio na ajali kwa kutegemea utaratibu wa kufuata kanuni. Tukifuata miongozo tuliyonayo, tutakuwa na ‘zero accident’, ajali hazitatokea kama kila mmoja atafuata taratibu,” alisema.
Profesa Mbarawa, alisema SGR itadumu na kufanya kazi kwa ufanisi wa juu kwa miaka mingi, ikiwa nidhamu ya uendeshaji, uwekezaji wa sekta binafsi na ufuataji wa kanuni, utaendelea kupewa kipaumbele.




