Na AMINA KASHEBA
NGUMI za kulipwa nchini zimekuwa zikiitangaza sana nchi kwa kuandika historia kwa mabondia kufanya vizuri katika mapambano yao ya kitaifa na kimataifa .
Historia hiyo inatokana na mabondia kushinda mapambano yao, kutokana na kufanya mazoezi ambayo yanawapa mbinu za kushinda.
Hivi sasa hapa nchini kuna mabondia wazuri ambao wanafanya vizuri ndani na nje ya nchi.
Lakini mafanikio yao, yametokana na juhudi kubwa zinazofanywa na makocha wao na mabondia wenyewe kwa kujituma.
Abdulrazaq Hamis ni miongoni mwa mabondia wanaofanya vizuri hivi sasa kutokana na kuonesha kipaji chake.
Bondia huyo amekuwa ana uwezo mkubwa wa kurusha ngumi pamoja na wepesi wake wa kuchenzesha miguu akiwa ulingoni.
Hamis mwenye miaka 23, anapigana uzito wa kati (52) alisoma Shule ya Msingi ya Temboni, mwaka 2018 na elimu ya sekondari aslipata katika Shule ya Temboni GVT.
Shule hizo zote mbili zipo eneo la Mbezi Kwa Msuguri iliyopo Wilaya ya Ubungo (2022).
Bondia huyo amecheza jumla ya mapambano manane, ameshinda mapambano sita.
Lakini amewahi kupoteza mapambano mawili tangu alipoanza kucheza mchezo huo wa ngumi.
Hajawahi kutoka sare pambano lolote, bondia huyo tangu alipoanza kushiriki mchezo huo.
NGUMI ZA RIDHAA
Kwa upande wa ngumi za ridhaa, bondia huyo amepanda ulingoni mara 20, ameshinda michezo 18 na kupigwa mapambano mawili.
Bondia huyo alisema alikuwa anapenda mchezo huo tangu anasoma shule ya msingi.
Hata hivyo, bondia aliwekeza nguvu zake katika masomo kwanza kuhakikisha anapata elimu na kuendelea na mambo mengine.
“Kwanza mimi ni mtu wa kufanya mazoezi, nilianza kupenda ngumi, japokuwa nina mwili mwembamba, lakini napenda kujiweka fiti kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza.
“Baada kufanya mazoezi kwa muda mrefu, nilianza kupenda mchezo wa ngumi, lakini nilijipa muda kwanza nimalize masomo yangu,” alisema.
SAFARI YA NGUMI
“Nilianza safari yangu ya ngumi mwaka 2020 nikiwa kidato cha pili chini ya Kocha, Idd Pamba maarufu ‘Man Pamba’ nilikuwa nafanya mazoezi hapo kutokana na kupenda mchezo huu tangu nipo shule.
“Napenda kucheza ngumi tangu nipo shule ya msingi, nilijipa muda wa kusoma kwanza halafu baadae ndiyo nifanye mambo ya ngumi, mwaka 2022 nilianza kujifunza mchezo huo,” alisema.
Bondia huyo aliongeza kuwa baada ya kujifunza sheria na kanuni za mchezo huo, nilianza kufundishwa namna ya kufahamu kujilinda na kufahamu jinsi ya kurusha makonde kwa mpinzani.
Aliongeza kuwa hadi hivi sasa bado yupo anafundishwa na kocha huyo ambaye anazidi kumpatia mafunzo na kumfundisha mbinu za kisasa nakushinda michezo anayocheza.
ALIYEGUNDUA KIPAJI CHAKE
Bondia huyo alifafanua kwamba mtu aliyegundua kipaji chake ni kocha, Man Pamba baada ya kumuona akifanya mazoezi ndani ya wiki moja.
“Aliyegundua kipaji changu ni kocha wangu Man Pamba baada ya kuniona kwa wiki moja nikifanya mazoezi, mimi sikutarajia kabisa kuja kuwa bondia nilikuwa napenda tu mazoezi ya ngumi, ” alisema.
CHANGAMOTO
“Changamoto ni kudharauliwa na watu wangu wa karibu katika jamii inayonizunguka , sikutarajia hata kama wao ndiyo wangekuwa wa kwanza kufanya hivyo.
“Niongeze juhudi ya kufanya mazoezi kwa bidii kutambua kuwa nina kipaji cha kucheza ngumi.
“Ukweli, zipo changamoto kubwa sana nilizopitia kipindi nikiwa naanza mchezo wa ngumi,watu waliniona kama mhuni,” alisema.
MALENGO
“Malengo yangu ni kuwa bingwa wa mkanda wa taifa, mabara pamoja na ubingwa wa dunia kama UBO, IBO, WBF na WBC, pia nahitaji jina langu lizidi kung’ara katika anga za kitaifa na kimataifa,” alisema.
Alisema mbali ya kumiliki mikanda mikubwa, malengo yake mengine ni kuendeleza kipaji chake cha mchezo wa ngumi, pia kuanzisha kademiki ambayo itakuwa chanzo cha kukuza vipaji.
“Kuna vijana wengi wana vipaji vya mchezo wa ngumi, lakini bado hajapata fursa ya kushikwa mkono hivyo malengo yangu ni kuanzisha akademiki ya kuendeleza vipaji,” alisema.
BONDIA WANAOMVUTIA
“Hapa nchini kwetu kuna mabondia wengi wazuri ambao wanafanya mambo makubwa ndani na nje ya nchi, lakini mimi navutiwa sana na Ibrahim Mgender ‘Ibrahim Class’, ‘Juma Choki’ na Hassan Mwakinyo kwa sababu hawa wana uwezo mkubwa.
“Pia, mabondia wa nje ya nchi ambao wananivutia ni mkongwe wa ngumi duniani, Mohamed Ali na Ditrim Bivol kwa sababu wamepata mafanikio makubwa kutokana na ngumi,” alisema.
Aidha, bondia huyo alieleza kuwa yupo tayari kupambana na mtu yoyote ambaye ana hadhi kubwa kuliko yeye.
“Mimi sichagui mtu wa kucheza naye, bondia yoyote napambana naye, nahitaji mtu mwenye hadhi ya juu ambaye atakuwa na faida na mimi, nipo tayari kucheza muda wowote,” alisema.
MAFANIKIO
“Bado sijapata mafanikio yoyote tangu nimeanza kucheza mchezo huu, bado ninaamini nikifanya vizuri,nitanufaika na kutengeneza maisha yangu,” alisema.
IMANI ZA KISHIRIKINA
“Siamini kabisa katika uchawi kamaunasaidia mtu afanikiwe katika ulingoni, siri kubwa ni kufanya mazoezi na kuzingatia maelekezo ya kocha.
“Mwanamichezo kushinda ni juhudi na kujituma katika mazoezi yake na kumuachia Mungu, lakini kujituma na kusikiliza mafunzo ya kocha,” alisema.
KITU AMBACHO HAWEZI KUSAHAU
“Kitu ambacho siwezi kusahau ni matukio mawili niliyokutana nayo katika tasnia ya ngumi, kwanza Agosti 28 mwaka 2022, tulienda mimi na kocha wangu katika mashindano ya ngumi za ridhaa nchini Kenya, tulivyofika kule tulipata ugumu jinsi ya kuwasiliana na mwenyeji wetu.
“Tulikuwa tunawasiliana naye kwa njia ya mtandao, tunashukuru sehemu tuliyofika ilikuwa karibu na eneo la mashindano tulifanikiwa kumpata, japokuwa tulipata changamoto kwa sababu tulikuwa ugenini tena nje ya nchi, pili tulipoteza mapambano kwa kudhurumiwa,” alisema.
FUNDI WA MADIRISHA
Bondia huyo alisema nje ya ngumi yeye ni fundi wa madirisha na milango ya Aluminium hivyo akikosa kupanda ulingoni huwa anafanya kazi zake kwa lengo la kupata kipato.
“Nje ya ngumi mimi ni fundi wa madirisha na makabati ya Aluminium, hivyo nikikosa mapambano huwa nafanya kazi hiyo, kujiongezea kipato,” alisema.
AKIWA NYUMBANI ANAPENDA KUFANYA KITU HIKI
“Nikiwa nyumbani mara nyingi napenda kuangalia tamthilia za wasanii wa Tanzania ikiwemo Kombolela na hupenda kuangalia mpira wa miguu.
“Nafuatilia kwa umakini mkubwa michuano ya ligi mbalimbali za Barani Ulaya na Ligi Kuu ya Tanzania Bara,” alisema.
Bondia huyo alifafanua kuwa anapenda kufanya kazi za nyumbani kama kufyeka majani na nyinginezo.
Pia, alisema anapenda sana kupika chakula pamoja na kuangalia mapambano ya mabondia kutoka nje ya nchi kwa lengo la kujifunza.
KITU KINACHOMKERA
“Kuna kitu kinanikera mno katika tasnia ya ngumi, kwani kuna baadhi ya viongozi wanakuwa na mabondia hivyo huwa hawatendi haki kipindi akiona bondia wake anapigwa na kumpatia ushindi ambao sio wake, binafsi hili jambo linanikera sana, ” alisema.
Hata hivyo, bondia huyo aluiwaomba waamuzi wa mchezo huo kutoa maamuzi ya haki ili kukuza vipaji vya mabondia wafike mbali kupitia mchezo huo.
MASHABIKI
“Mashabiki zangu nawashukuru sana kwa kunipa sapoti, nina amini bila wao siwezi kufika popote kwani sapoti yao inanipa nguvu ya kupambana nikiwa ulingoni ndiyo maana napambana kuongeza bidii katika mazoezi yangu, ” alisema.
Bondia huyo aliongeza kuwa bado anaendelea kujipanga vizuri zaidi ili afanye vizuri katika mapambano yanayomkabili.




