Na MWANDISHI WETU
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amewataka vijana kutokubali kutumika kuvuruga amani na utulivu nchini kwa madai ya kudai haki.
Amesema Tanzania haina uadui na nchi nyingine, lakini yapo baadhi ya mataifa, yanayoumizwa na kasi ya maendeleo iliyopo nchini.
Amesema wanafahamu Tanzania inaelekea kujikomboa kiuchumi, hivyo kuondoka katika kundi la kuomba misaada kutoka kwao.
Wasira alieleza hayo Zanzibar, alipozungumza na vijana, akiwa ziarani visiwani humo.
“Tanzania haina nchi adui, yaani rasmi kusema sisi nchi yetu adui yetu yule pale, Tanzania hatuna, lakini siyo kweli, duniani watu wote wanatupenda, hiyo nayo siyo sahihi.
“Wako wengine wakiona tunafanya maendeleo makubwa wananuna, wapo, wengine wana sababu zao siyo sababu zetu, wasingependa tujitegemee kwa kuwa, tukijitegemea tutaachana na habari ya kwenda kwao kuomba, wangependa wakati wote iwe ‘spoon feed’ yaani tunakaa tunangoja msaada.
“Wakiona Chama kinafanya jitihada za kutuondoa katika kuombaomba, hawapendi. Wakiona Zanzibar imepiga hatua miaka 60 na miaka mitano iliyopita hapa ya awamu ya nane, wanashtuka, wanashangaa hawapendi,” alisema.
WOSIA KWA VIJANA
Aliwataka vijana wa Tanzania wasikubali kutumika kuivuruga nchi yao, kwa kuwa hakutawaletea maendeleo.
“Wosia wangu kwa vijana mliosoma mliohitimu na wale waliohitimu mapema na ambao hawajaenda vyuo vikuu, hii ni nchi yetu sote, nchi hii haina mtu maalumu ambaye anasema anaimiliki, wamiliki wake ni Watanzania ambao ni milioni 60 na zaidi.
“Kwa hiyo, mkitaka kuwa na maendeleo makubwa, suala la amani ni lazima wala siyo hiyari, maana ukiondoa amani kwa kudanganyika ukidhani unadai haki tutapoteza haki zote, maana utabaki na ipi? Katikati ya vurugu hata haki ya kuishi unapoteza,” alisema.




