Na MWANDISHI WETU,
Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar itaendelea kuwakaribisha wawekezaji kwa kuwa, kuna fursa nyingi za uwekezaji zinazohitaji ushirikiano wa wadau na taasisi za kimataifa.
Rais Mwinyi, aliyasema hayo Ikulu Mjini Unguja, alipokutana na Mwenyekiti wa Taasisi ya Commonwealth Enterprise and Investment Council, Lord Swire na ujumbe wake, waliofika Ikulu kwa mazungumzo.
Rais Mwinyi, aliuambia ujumbe huo kuwa, Zanzibar imekuwa ikifanya juhudi kubwa za kuimarisha sekta ya uwekezaji, kwa lengo la kuvutia wawekezaji, hususan sekta mbili kuu za uchumi, ambazo ni uchumi wa buluu na utalii.
Alieleza ujio wa ujumbe huo ni fursa muhimu kwa Zanzibar katika kufanikisha malengo ya uwekezaji.
Alizitaja sekta za uchumi wa buluu na utalii, kuwa ndizo kuu zinazochangia takribani asilimia 30 ya pato la taifa na kuna fursa nyingi ambazo taasisi hiyo, itashirikiana na Zanzibar.
Aidha, Zanzibar imejipanga vizuri kubainisha fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali na maeneo ambayo yanahitaji wawekezaji.
Akizungumzia Bandari Jumuishi ya Mangapwani, Rais Mwinyi, alisema eneo hilo ni la kimkakati, lina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta tofauti, ukiwemo usafirishaji, mafuta, gesi na biashara.
Mwenyekiti wa Commonwealth Enterprise and Investment Council, Lord Swire, alisema Zanzibar ni mshirika muhimu, wako tayari kushirikiana nayo katika nyanja mbalimbali za uwekezaji na biashara kwa maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa wananchi.
Taasisi ya Commonwealth Enterprise and Investment Council, inajishughulisha na kuimarisha ushirikiano, biashara na uwekezaji miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola.




