NA SULEIMAN JONGO
WATANZANIA wanaadhimisha miaka 64 ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) ambao ulipatikana Desemba 9, mwaka 1961 huku kukiwa na mafanikio mbalimbali ya mfano.
Kupatikana kwa Uhuru kunatokana na msukumo wa wananchi wa Tanzania Bara kutaka kujinasua katika makucha ya wakoloni ambayo hawakutoa nafasi kwa Waafrika weusi kujiletea maendeleo katika sekta mbalimbali zenye kurahisisha maisha na maendeleo ya mwanadamu.
Tangu nchi ilipopata uhuru, imeshapita katika awamu sita za uongozi akianza Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye alitawala katika awamu ya kwanza, akafuatiwa na Rais wa Awamu ya Pili, Hayati Alhaji, Ali Hassan Mwinyi, kisha chini ya Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin Mkapa, ikafuata ya Awamu ya Nne iliyoongozwa na Rais Dk. Jakaya Kikwete ambaye alimwachia kijiti Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Magufuli na sasa Tanzania ipo katika awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Hayati Mwalimu Nyerere katika awamu yake, aliweka msingi wa kuhakikisha Watanzania wanaondokana na unyonge kwa kutangaza vita dhidi ya maadui watatu ambao ni maradhi, ujinga na umasikini, kisha akaanza kutekeleza kwa vitendo hatua za kukabiliana nao
Viongozi waliofuata baada ya hapo kila mmoja alitekeleza vema dhima ya kuwakabili maadui hao kwa namna mbalimbali alimradi Watanzania waondokane na changamoto za maradhi, ujinga na umaskini.
Ni kutokana na mtazamo huo, mwaka 2000 serikali iliamua kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ikiwa mbinu ya kusaidia harakati za kukabiliana na umaskini kwa kuwahusisha wananchi moja kwa moja.
TASAF ilionesha kuanza kufanikiwa kati ya mwaka 2009 hadi 2012, ilipofanya mradi wa majaribio ya uhawilishaji fedha taslimu kwa masharti ‘Conditional Cash Transfer’ (CCT) ambayo yalifanyika katika Wilaya za Kibaha, Bagamoyo (Mkoa wa Pwani) na Chamwino (Dodoma).
Matokeo ya majaribio hayo yalionesha mafanikio makubwa katika sekta za afya, elimu na kuongezeka kwa rasilimali za kaya.
Mwaka 2012 TASAF ilianza utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini – ‘Productive Social Safety Net’ (PSSN I) ambao ulikuwa na lengo la kuziwezesha kaya masikini kuongeza vipato na fursa za kujikimu.
PSSN I ilifanikiwa kusajili kaya 1,118,752 kutoka vijiji 9,831 katika Mamlaka za Maeneo ya Utekelezaji 161 ikiwa Halmashauri za eneo la Mradi Jiji, Manispaa, Wilaya na Halmashauri za Miji kwa Tanzania Bara, pamoja na Unguja na Pemba kwa upande wa Zanzibar.
Tangu hapo, TASAF imefanikiwa kubadili historia ya maelfu ya kaya ambazo sasa zinautazama mfuko huo kama njia iliyowapeleka peponi kwa kuwa bila ya uwepo wake hawajui kesho yao ingekuwaje, siyo kwa kula, kulala, kujitibu, kusoma na hata mavazi kwa baadhi yao.
MONICA ATOA USHUHUDA
Monica Masagasi, mama wa watoto wanne, mkazi wa Mtaa wa Mapinduzi, Chamwino jijini Dodoma, anaeleza jinsi TASAF ilivyomwezesha yeye na watoto wake kutoka katika kundi la kaya zisizojua hata chaka cha siku kutokana na hali duni ya uchumi na kuwa mmoja kinamama wa mfano mtaani kwake.
Akizungumza na gazeti hili Monica alisema ni mama wa watoto wanne na kwamba kabla ya kujiunga na Mpango wa kuziwezesha Kaya Maskini, alipitia kipindi kigumu wakati mwingine alilala bila kupata chakula na watoto.
“Sitamani kukumbuka niliyoyapitia, nilikuwa na hali ngumu, watoto walikwenda shule kwa tabu, sikuwa na uwezo hata wa kuwabadilishia sare za shule, lakini sasa nashukuru nimeuona mwanga wa matumaini, hali yake imezidi kuimarika, sasa nina uhakika wa chakula, watoto kusoma na hata matibabu pale tunapougua,” alisema.

Akielezea safari yake ya unufaika, anasema, kutokana na hali ngumu ya kiuchumi aliyokuwa nayo, serikali ya mtaa wake ilimtambua na hivyo kumuweka katika orodha ya kaya zinazostahili kusaidiwa kupitia uwezeshaji wa TASAF.
Kwa mujibu wa Monica, baada ya kukamilika kwa utaratibu wa kujiunga, alianza kupokea sh. 80,000 kila baada ya miezi miwili ambazo zilisaidia yeye na watoto wake wanne ambapo watatu walikuwa wakiendelea na masomo shule ya msingi na sekondari.
Monica alieleza kuwa, fedha hizo zilimsaidia yeye na watoto wake kwa chakula, kuhudumia watoto kwenda shule na alianza kujishughulisha na biashara ndogondogo.
Aidha, alisema mwaka 2024, TASAF ilimfanya aandike historia mpya baada ya kumpatia mtaji wa sh. 200,000 ambao aliutumia kununua nguruwe wawili ambao alianza kuwafuga.
Alifafanua kuwa, kwa sasa nguruwe hao wameongezeka na kufikia 17, hatua ambayo hakuwahi kuifikiria kwa kuwa sasa anaiona kesho yake ikiwa bora zaidi katika kujikwamua kiuchumi.
“Naamini nguruwe hawa wataongezeka, nitafanya biashara kubwa kwa kuwa soko ni kubwa. Naishukuru TASAF imenishika mkono, imenipa uhakika wa kuishi maisha bora,” alieleza.
MKURUGENZI MTENDAJI TASAF
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Shedrack Mziray, akieleza kuhusu shughuli za mfuko huo, alisema tangu ulipoanzishwa umejikita kuwafikia wananchi wenye sifa na kila anayekidhi vigezo amekuwa akifikiwa.
Mziray kwa nyakati amekuwa akisisitiza kwamba, lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo na kuendeleza juhudi za kupunguza umasikini wa kipato kwa kaya maskini hatua ambayo itachochea uchumi wa mtu mmoja mmoja, kaya na taifa kwa ujumla.
Amekuwa akieleza kwamba, mradi huo unatekelezwa katika pande zote mbili za muungano na kwamba hilo litaendelea kuzingatiwa kwa kuhakikisha wananchi wenye sifa na wanaoweza kufikiwa, wananufaika bila kujali mkoa au wilaya waliyopo.
Mapema mwaka huu, Mziray aliiongoza timu ya TASAF kukutana na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hamed Suleiman Abdulla, ambapo alimuahidi kuendeleza ushirikiano.
Alibainisha kuwa, kupitia Awamu ya Pili ya Mpango wa Kusaidia Kaya Maskini ambayo ilifikia kikomo Septemba mwaka huu, zaidi ya walengwa milioni 1.3 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wamenufaika na ruzuku, ajira za muda, na mitaji ya biashara.
Aliongeza kuwa, awamu ya tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini, itakayoanza mwakani na kudumu kwa miaka minne, inalenga kufikia walengwa 575,000 na kwamba, programu hiyo itajikita katika maeneo yaliyoathirika zaidi na umasikini na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ikiwawezesha wananchi kupata ruzuku, ajira za muda na afua mbalimbali za Mpango.
Mkurugenzi Mtendaji Mziray alieleza kuwa, wakati Watanzania wakiadhimisha miaka 64 ya uhuru wa Tanzania Bara, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii, ni sehemu ya mambo yanayopaswa kutajwa kama kielelezo cha mafanikio ya kujiondoa katika umaskini.




