LONDON, England
MSHAMBULIAJI wa timu ya wanawake ya Tottenham, Jess Naz anatarajia kukaa nje hadi mwishoni mwa msimu huu kufuatia kupata tatizo la goti.
Raia huyo wa England, hataonekana tena katika mechi zote za msimu huu kutokana na tatizo linalomkabili.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25, alipata majeraha katika mchezo kati ya timu yake dhidi ya Aston Villa mwishoni mwa wiki iliyopita na hivyo anatarajiwa kufanyiwa upasuaji katika goti la kulia.
Taarifa zilizotoka katika mtandao wa klabu zilisema, Jess aliumia goti mara ya pili baada ya kupata tatizo hilo awali na kuukosa msimu wa mwaka 2019-20.
Ilisema Jess ambaye alianza katika kikosi cha kwanza katika mechi zote msimu huu zikiwemo sita za timu ya taifa ya England, hataonekana tena hadi msimu ujao.
“Jess amepata tatizo la goti la kulia ambapo anatarajiwa kuzikosa mechi zote zilizobakia msimu huu.
“Ni pigi kumkosa Jess katika kikosi cha Spurs kwani ni mmoja wa wachezaji muhimu, amekuwa na msaada mkubwa kwa muda mrefu.
“Jess anatarajiwa kufanyiwa upasuaji muda wowote kuanzia hivi sasa kuhakikisha anarejea katika majukumu yake kama ilivyokuwa awali” ilisema taarifa hiyo.
Wachezaji wengine waliopata tatizo hilo msimu huu ni Michelle Agyemang (Brighton), Maite Oroz (Tottenham), Marie Hobinger (Liverpool), Manu Zinsberger (Arsenal), Sophie Roman Haug (Liverpool), Jill Baijings (Aston Villa) na Katie Reid (Arsenal).
(BBC)




