Na ABDUL DUNIA
KLABU ya soka ya Simba inamsubiri kocha wake mpya kutoa mapendekezo ya maboresho ya kikosi hicho kwa mechi zijazo za Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) na Kombe la Shirikisho kuhakikisha miamba hiyo inaingia sokoni kuimarisha timu katika dirisha dogo.
Simba ambayo ipo katika hatua za mwisho kumtangaza kocha mpya baada ya kuachana na Meneja Mkuu Dimitar Pantev, inajipanga na usajili katika dirisha dogo linalotarajiwa kufunguliwa mwezi ujao.
Hivi karibuni, uongozi wa klabu hiyo ulikiri kupokea maombi ya makocha zaidi ya 100 ambapo majina raia wa Afrika Kusini, Steve Becker ambaye ni Kocha wa Stellenbosch na raia wa Hispania, Antonio Casano anayekinoa kikosi cha Atletico Luanda ya Angola ndio wametajwa sana mmoja wapo kupewa mikoba ya Pantev.
Miamba hiyo inahitaji kufanya uboreshaji wa kikosi hicho kwa kuongeza nyota mahiri na kuwakata baadhi ya wachezaji wake wa sasa, lakini kabla ya kuchukua uamuzi huo kwanza itasubiri mapendekezo ya benchi jipya la ufundi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema tayari klabu hiyo inaripoti ya kiufundi ya hali ya kikosi chake na nini cha kufanya katika dirisha dogo.
Hata hivyo, Ahmed amesema kabla ya uongozi kushusha mchezaji yoyote kwanza itasubiri mapendekezo ya kocha wake mpya atakayepatikana hivi karibuni kuhakikisha kila mchezaji anayetua anakuwa chaguo lake.
“Maboresho ya kikosi yanasubiri ujio wa mwalimu mpya ndiyo atoe mapendekezo yake kulingana na ripoti za kiufundi zilizopo,” alisema.
Ahmed amesema timu hiyo inarejea mazoezini Desemba 28, mwaka huu kujiweka fiti kwa muendelezo wa Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika na michuano mingine.
Meneja huyo aliweka wazi kuwa, Simba imepanga kufanya vyema katika michuano yake yote hasa CAFCL ambayo imeanza kwa kusuasua katika hatua ya makundi.
Katika michuano hiyo, Simba inaburuta mkia katika kundi D ikiwa haina pointi baada ya kupokea vichapo viwili mfululizo dhidi ya Petro Atletico ya Angola (1-0) na Stade Malien kutoka Mali (2-1).
Simba katika kundi hilo imebakisha mechi nne dhidi ya Esperance ya Tunisia (nyumbani na ugenini), Petro (ugenini) na Stade Malien (nyumbani).
Katika Ligi Kuu Bara, Wekundu hao wa Msimbazi wamepoteza mechi moja kati ya tano ilizocheza ikianza kwa ushindi dhidi ya Fountain Gate (3-0), Namungo (3-0), JKT Tanzania (2-1) na Mbeya City (3-0) kabla ya kufungwa na Azam FC (2-0).




