Na WAANDISHI WETU
SERIKALI imetangaza neema kwa wakazi wa Mkoa wa Lindi kupitia Bandari ya Uvuvi ya Kilwa.
Imesema itanunua meli tano na kujenga kongani ya viwanda katika eneo hilo.
Hatua hiyo, itasaidia kuongeza fursa za ajira kwa wananchi wa Lindi na kukuza pato la taifa kwa mwananchi mmoja mmoja.
Akizungumza wilayani Kilwa alipokagua ujenzi wa bandari hiyo, Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba, alisema mradi huo, umejengwa kwa fedha za Watanzania na umegharimu zaidi ya sh. bilioni 280.
“Zitanunuliwa meli tano, hatutavizia zinazotoka mbali, zitanunuliwa meli ukiweka na sekta binafsi (meli), nchi yetu inakwenda kuandika historia mpya kwenye mambo ya uvuvi,” alisema.
Alisema mradi huo, umefikia zaidi ya asilimia 90, baada ya miezi miwili, unatarajiwa kuzinduliwa, huku ajira zaidi ya 30,000 zikitarajiwa kupatikana.
“Kwenye sekta hii (uvuvi) Mheshimiwa Rais (Dk.Samia) anaendelea na programu nyingine ikiwemo ya kugawa boti za uvuvi na kujenga vizimba,” aliongeza.
Pia, Dk. Mwigulu, alisema bandari hiyo ni mojawapo ya miradi ya kielelezo iliyoendelezwa na Rais Dk. Samia, ikiwa ni sehemu ya miradi mingine ya kimkakati, ikiwemo ya Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere, Daraja la Kigongo Busisi na Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR).
Aidha, Waziri Mkuu, alisema ameridhishwa na ujenzi wa bandari hiyo kwa kuwa, unaendana na thamani ya fedha zilizotumika.
ULIPAJI FIDIA UWANJA WA NDEGE
Dk. Mwigulu alisema Rais Dk. Samia ameendelea kulipa fidia za muda mrefu, ambapo hivi karibuni alitoa zaidi ya sh. bilioni 50 kulipa fidia katika mradi wa upanuzi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Alisema serikali chini ya Rais Dk. Samia, itaendelea kulipa fidia katika miradi mbalimbali ikiwemo ya awamu zilizopita.
“Kulikuwa na fidia pale Uwanja wa ndege Dar es Salaam, hivi tunavyoongea sh. bilioni 50 zimeshalipwa, kulikuwa na fidia uwanja wa KIA zimeshalipwa, kulikuwepo na fidia Engaruka, Liganga na Mchuchuma zimeshalipwa hizi siyo za jana ni za siku nyingi, Rais Samia amechukua uongozi na anazishughulikia.” aliongeza
Alisema matatizo ya Watanzania, hayawezi kushughulikiwa kwa siku moja, ingekuwa hivyo, Rais Samia asingekuta fidia za mwaka 2010 na miaka mingine iliyopita.
ASISITIZA KUTUNZA AMANI
Aidha, Dk. Mwigulu, aliwataka Watanzania kutokubali kujifunza kuichukia nchi yao, huku akisisitiza ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda amani ya taifa.
Alisema ili miradi mikubwa ifanyike na nchi ipige hatua, lazima kuwe na amani, mnufaika wa kwanza huwa ni Mtanzania mwenyewe.
“Mtanzania usifundishwe kuichukia nchi yako, tunafanya mambo makubwa, niwasisitize lazima nchi yetu iendelee kuwa ya amani, ili miradi mikubwa iendelee kufanyika na tupige hatua. Ni lazima kila Mtanzania awajibike na suala la amani,” alisema.
ELIMU
Dk. Mwigulu, alisema serikali inatoa zaidi ya sh. bilioni 35 kila mwezi kugharimia elimu bila ada.
Alisema awali kidato cha sita na tano hazikuwepo katika mfumo wa elimu bila malipo, lakini sasa wanafunzi wa vidato hivyo, wananufaika.
Vilevile Dk. Mwigulu, alisema Rais Samia, alifanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu, ikiwemo kujenga vyumba vya madarasa 79,000 shule 1,300 za sekondari na shule 2,700 za msingi.
KILIMO
Akizungumza kuhusu sekta ya elimu, Dk. Mwigulu alisema Rais Samia, ameendelea kuboresha sekta ya elimu, amewezesha ujenzi wa miradi ya umwagiliaji zaidi ya 700.
Akijibu swali la mwananchi katika Kijiji cha Somanga, aliyetaka kujua lini serikali itaongeza zahanati na shule, Dk. Mwigulu, alisema katika miaka minne iliyopita, Dk. Samia alijenga zahanati 2,700, hivyo katika kipindi chake cha pili, atajenga shule nyingine za msingi na zahanati za kutosha kila kijiji.
WAZIRI MIFUGO, UVUVI
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Bashiru Ally Kakurwa, alisema kukamilika kwa bandari hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Dk. Bashiru, alisema mradi huo, utakamilika na kukabidhiwa kwa serikali Machi mwaka 2026.
Alisema bandari hiyo, itaongeza fursa za ajira kwa wakazi wa eneo hilo na kwamba, wizara yake, imekusudia kuleta tabasamu kwa Watanzania kupitia utekelezaji wa maagizo ya Rais Dk. Samia.
MENEJA MRADI
Msimamizi wa Mradi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa, George Paul, alisema eneo ambalo bandari hiyo imejengwa, lina hekari 11 na litakuwa na shughuli za kibandari na uchakataji mazao 48.
Pia, alisema viwanda fungamanishi kwa bandari, vitajengwa katika eneo hilo na wavuvi watashusha moja kwa moja katika gati.
Meneja Paul, alisema magati yaliyojengwa katika bandari hiyo, yana uwezo wa kuegesha meli 10 za uvuvi za mita 30 na kushusha kwa wakati mmoja.
WAZIRI ULEGA
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alisema wizara hiyo, imejipanga kufungamanisha barabara na Bandari ya Kilwa kurahisisha usafirishaji.
RC LINDI
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, alitoa pongezi kwa Rais Dk. Samia, akisema uongozi wake, umeleta mageuzi makubwa katika sekta ya miundombinu na huduma za kijamii, hatua iliyosaidia kurejesha utu na heshima kwa Watanzania.
Alisema uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika sekta mbalimbali, umesaidia wananchi kuondokana na kero ya kusubiri huduma muda mrefu.




