Na MWANDISHI MAALUMU
WAZIRI Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba, amemwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), awaandikie barua wakuu wote wa mikoa, waunde timu za ukaguzi wa majengo.
Pia, miradi katika mikoa yao, kama njia ya kukabiliana na wakandarasi wanaokiuka makadirio ya gharama za ujenzi (BOQ) wa miradi ya serikali.
“Yuko Mhandisi ambaye huwa anakagua miradi wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru.
“Wakuu wote wa mikoa, wawe na timu za vijana wa aina hiyo, wasiuziwe mbuzi kwenye gunia.
“Uwe ni utamaduni wa serikali kufanya ukaguzi wa aina hiyo,” alisema Waziri Mkuu.
Dk. Mwigulu alitoa agizo hilo, akizungumza na viongozi na wananchi wa Wilaya za Ruangwa na Nachingwea, mkoani Lindi, akiwa katika ziara ya siku tatu ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani humo.
Baada ya kukagua ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Dk. Mwigulu, alisema kuna baadhi ya miradi ambayo wakandarasi wake hawafuati BOQ.
“Unakuta BOQ, inataka nondo za mm 16, lakini mkandarasi anaweka za mm 12. “Kuna mahali zinatakiwa nondo sita, yeye anaweka nondo nne. Jengo likikamilika, huwezi kuona na kulinganisha makubaliano ya BOQ. Nimeelekeza kila mkoa uwe na timu ya wataalamu wa kukagua miradi ya serikali.”
“Mikoa yote wawe na vitengo hivi, wawe pia na vifaa vya kuchunguza majengo na miradi mingine, badala ya kusubiri uchunguzi unaofanywa wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru.
“Vitengo hivyo, kazi yao ya kila siku ni kufuatilia miradi kubaini maeneo ambako serikali imetoa fedha na hazijatumika vizuri, tuchukue hatua,” alisisitiza.
Mapema, Dk. Mwigulu, aliweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Lindi-Ruangwa- Nachingwea uliojengwa katika Kijiji cha Chimbila A wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Mradi huo ambao chanzo chake kinatoka mito ya Nyangao na Chilua wilayani Lindi, unatekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), utakapokamilka, utanufaisha vijiji 56 katika Wilaya za Ruangwa (vijiji 34), Wilaya ya Nachingwea (vijiji 21) na Wilaya ya Lindi (kijiji kimoja).
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa RUWASA, Mhandisi Walter Kirita, alisema mradi huo, unatarajiwa kugharimu sh. bilioni 119, hadi sasa wameshalipa sh. bilioni 49 ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 67 ya utekelezaji.
Mradi huo, umeanza kutekelezwa Februari, 2023 na awamu ya kwanza (Lot 1) inatarajiwa kukamilika Juni, 2026.
Hata hivyo, Mhandisi Kirita, alimweleza Waziri Mkuu kuwa, ifikapo Februari, 2026 baadhi ya vijiji vitaanza kupata huduma ya maji.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi, Dk. Mwigulu, alisema ameridhishwa na hatua ya utekelezaji wa miradi ambayo imefikiwa.
“Hivi ndivyo Rais Samia anataka kuona namna kazi inavyofanyika. Hapa tumeona asilimia ya utekelezaji ni kubwa kuliko fedha zilizotolewa hadi sasa. ”
Dk. Mwigulu, alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa, kuasisi mradi huo na kufuatilia fedha za mradi kila mara.
AWESO
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alisema mradi huo ulikuwa ombi maalumu la Majaliwa, aliyeomba kutokana na eneo hilo kukosa maji safi na salama.
“Baada ya ombi hilo, Rais Samia, alitoa maelekezo kuhakikisha mradi unaanza mara moja wananchi wa Ruangwa waweze kupata maji safi na salama.
“Mradi huu ni wa sh. bilioni 119 bajeti ya msimu uliopita, ambapo wewe Waziri Mkuu, ulikuwa Waziri wa Fedha, tulipoleta ombi hilo, halikuwa kikwazo na ukatoa fedha zote, mkandarasi hatudai chochote na kabla ya Februari mwakani, kuna baadhi ya vijiji wataanza kunufaika nao,” alisema.
NAIBU WAZIRI WA AFYA
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Florence Samizi, alisema alimpongeza Rais Samia kwa mradi huo mkubwa wa maji.
Aidha, alisema kuanzia Januari mwakani, kutakuwa na bima ya afya kwa wote na katika Mkoa wa Lindi, kutakuwa na wanufaika 26,000 kati ya 900,000.
PROFESA MKUMBO
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alimpongeza Dk. Mwigulu kwa ziara anazofanya, ambazo zinaonesha umahiri katika utendaji wake.




