Na MWANDISHI WETU, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ),, imeipongeza Benki ya NMB kwa kusaini mkataba wa udhamini wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi kwa miaka mitano.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 inashirikisha timu 10, zikiwemo Yanga, Simba SC, Azam FC, Singida Black na TRA United za Tanzania Bara, Mlandege, KVZ, Fufuni FC na Muembe Makumbi City za Zanzibar na URA ya Uganda.
Katika michuano hiyo inayotarajiwa kufikia tamati Januari 13, mwakani, NMB na Kamati ya Mashindano hayo wamesaini mkataba, ambao hata hivyo haujatajwa thamani yake.
Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo visiwani hapa, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa SMZ, Dk. Riziki Pembe Juma, aliishukuru NMB kwa kuyapa hadhi na thamani mashindano hayo na kwamba imeonyesha kwa vitendo inavyojali ushirikiano dhidi ya serikali yake.
Alisema mkataba huo wa miaka mitano wa NMB, ni mwendelezo wa ushirikiano uliotukuka baina ya benki hiyo na SMZ na kwamba wao kama serikali wanaahidi kuyadumisha kwa maslahi mapana ya Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla.
“NMB mmetuonesha uzalendo mkubwa, kwa kukubali kusaini mkataba huu na Kamati ya Mashindano kwa niaba ya serikali. Tunaahidi kudumisha ushirikiano na benki hii, ambayo udhamini wao huu unaenda siyo tu kubadili taswira ya mashindano, bali ndiyo mkubwa na mnono zaidi kuwahi kutolewa.
“Hata ukiangalia eneo la zawadi zao watakazokuwa wanatoa kwa Mchezaji Mwenye Nidhamu wa Mechi, hatua ya makundi, nusu fainali na hadi fainali, zinaakisi dhamira yao ya kuyaboresha na kuyapa msisimiko mkubwa mashindano haya,” alisema.
Naye Mkuu wa Idara ya Mauzo na Mtandao wa Matawi ya NMB, Donatus Richard, alisema wanajivunia ushirikiano wao wa miaka 13 ya mashindano hayo, na kwamba udhamini wao mkuu kwa kipindi cha miaka mitano, ni kielelzo cha juhudi za taasisi yake katika kuisapoti SMZ.
“Udhamini huu siyo tu kwa ajili ya kufanikisha shughuili za NMB Mapinduzi Cup 2026, bali ni juhudi ya NMB kushirikiana na SMZ katika kuitangaza chapa ya visiwa vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, hii ndiyo maana halisi ya ushiriki wa sekta binafsi katika kuitangaza nchi kimataifa.
“Kwa hatua ya makundi tutatoa tuzo na fedha taslimu sh. 500,000 kwa mchezaji mwenye nidhamu, nusu fainali sh. milioni moja na sh. milioni mbili mchezo wa fainali ambao utashuhudiwa na mgeni rasmi Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi,” alisema Donatus.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya NMB Mapinduzi Cup 2026, Machano Makame Haji, aliishukuru benki hiyo kuyabeba mashindano hayo na kuyafanyia mapinduzi ya kimaboresho yanayoipa hadhi ya kimataifa michuano hiyo.




