Na Jacqueline Liana
UKOSEFU wa maadili ya utumishi wa umma kwa baadhi ya viongozi na watendaji, umekuwa ni kikwazo kimojawapo cha kutofikiwa kwa malengo ya maendeleo yanayotarajiwa ama serikalini, mashirika ya umma au taasisi nyingine za umma.
Machi 2, mwaka, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alitoa wito kwa viongozi na watendaji serikalini kujitathmini kama wana maadili ya uongozi na utendaji katika utumishi wa umma.
Aliyasema hayo alipofanya mkutano wa faragha wa mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Arusha (AICC), jijini Arusha.
“Watu tunao, ardhi tunayo na siasa safi ipo, suala la kujadili ni kuhusu uongozi bora, baada ya kumaliza kikaokazi hiki kila mmoja ajitathimini kama maadili ya kiongozi bora tuliyoambiwa yapo au la!” alisema Dk. Samia.
Lengo la kikao hicho lilikuwa pamoja na mambo mengine, ni viongozi na watendaji hao waandamizi kuelekezana juu ya kutimiza ipasavyo wajibu wao kwa dhamana walizonazo katika ofisi za umma.
“Katika jukumu lenu la utawala, mnategemewa kuwa makini na mahiri katika kutumia na kusimamia rasilimali watu, vifaa na fedha za umma, kuwa na mipango na mikakati thabiti ya kutekeleza na kusimamia majukumu hayo,” alisema kiongozi mkuu wa nchi.
Aliwaambia viongozi hao kwamba, wanawajibu wa kuzifahamu kwa kina shughuli za wizara walizomo ziweze kufanyika kwa umakini na weledi, vinginevyo watashindwa kupanga malengo ya kutimizwa kwa walio chini yao kwani watakuwa hawajui nini cha kuelekeza na watashindwa kusimama kwa kuwa hawatakuwa wanajua nini cha kusimamia.
Katika uongozi wa nchi wa Rais Dk. Samia, Watanzania wanashuhudia maendeleo katika kila sekta kwa kiwango cha kustajaabisha.
Sekta zinazogusa maisha ya Mtanzania moja kwa moja; afya, elimu na maji, zimepanuliwa na kuboreshwa kwa kazi ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Methali ya “mnyonge mnyongeni haki yake mpeni”, inamstahili Dk. Samia, licha ya uwepo wa kasoro za kiuongozi na kiutendaji zinazosababishwa na baadhi viongozi na watendaji serikalini.
Watanzania wanashuhudia anavyoiongoza serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo ambayo Watanzania walidhani, ingekuwa ni “basi tena”.
Miongoni mwa miradi ambayo ilidhaniwa ingeishia njiani ni Ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHEP) na ujenzi wa reli ya kisasa maarufu SGR.
Rais Dk. Samia anaingia madarakani miradi hiyo ikiwa katika hatua za awali, kwa sasa bwawa linaingiza umeme katika gridi ya taifa na safari za kupita juu ya SGR kwa treni siyo ndoto tena.
Mwandishi wa vitabu Peter Ferdinand
Drucker, ameandika; “uongozi wa kupigiwa mfano siyo wa kutengeneza hotuba nzuri zenye kukonga nyoyo za watu
au kupendwa, bali uongozi mzuri hutazamwa kwa matokeo”.
Mwandishi wa vitabu mwingine, John Maxwell, aliandika “kiongozi mzuri ni yule
anayeijua njia, anapita katika njia hiyo na kuonyesha wengine njia hiyo”.
Dk. Samia hapana shaka anajua vyema Watanzania wanahitaji kufika wapi na njia ipi wapite taifa lao lifike huko wanakokutamani.
Ilizoeleka kuona miradi ya maendeleo ikitekelezwa kwa miaka kadhaa hadi kukamilika na wakati mingine kutokuendelezwa, kama bwawa hilo la kufua umeme ambalo lilianza kuzungumzwa tangu uongozi wa nchi wa Mwalimu Nyerere katika miaka ya 1970.
Uongozi wa nchi wa Dk. Samia, umeua utaratibu wa wanafunzi wanaochaguliwa kuanza kidato cha kwanza kuanza kwa mafungu, kwa sasa wote wanaanza kwa mkupuo mmoja.
Huduma za afya zimeimarishwa kuanzia zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, mikoa hadi hospitali za rufaa, kwa serikali kuendeleza ujenzi wa miundombinu, usambazaji wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba.
Upatikanaji na usambazaji wa maji safi na salama mijini na vijijini umeendelezwa kwa kasi, ikiwa ni utekelezaji wa kaulimbiu ya “Kumtua Mama Ndoo Kichwani”, ambayo muasisi wake ni Dk. Samia.
Ukosefu wa maji karibu na makazi ya watu lilikuwa ni tatizo sugu, licha ya Tanzania kuwa na vyanzo vingi na vikubwa vya kupata maji ya uhakika.
Barabara zimeendelea kujengwa na kuboreshwa mijini na vijijini na kuwa kichocheo cha kufanyika kwa ufanisi kwa shughuli mbalimbali za kuingiza vipato kama kilimo na biashara.
Kilimo kimepewa msukumo wa pekee chini ya uongozi wa nchi wa Rais Dk. Samia, hivyo kutekeleza kwa vitendo kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ya “Kilimo ni Uti wa Mgongo” wa uchumi wa taifa.
Kwa kuwa Tanzania inayo ardhi kubwa yenye kufaa kwa kilimo, uongozi wa Dk. Samia unataka rasilimali hiyo itumiwe kuwezesha nchi kuwa na uhakika wa chakula.
Septemba mwaka juzi, akihutubia Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF 2023), Rais Dk. Samia alisema viongozi wa Afrika wanatakiwa kuwa tayari kuhakikisha Afrika inajitosheleza kwa chakula.
“Asilimia 60 ni vijana ambao ni nguvu kazi, sisi viongozi wa Afrika tupo tayari kuondoa aibu ya Afrika ya kuwa walalamikaji tupo tayari kulisha Afrika na duniani kwa ujumla,” alisema.
Alisema licha ya rasilimali zilizopo, Waafrika wamebaki kuwa walalamikaji badala ya kutafuta suluhisho kuelekea njia ya mapinduzi ya uchumi wa kijani.
Alisema, katika kuelekea mageuzi wanayoyataka katika sekta ya kilimo, mataifa ya Afrika hayana budi kuweka mipango na mikakati kufikia Afrika wanayoitaka.
Chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia, sekta ya kilimo imekuwa na mabadiliko makubwa ambayo matokeo yake ni nchi kuwa na chakula cha kuwatosha wananchi wake na ziada ya kuuza nchi nyingine.
Uongozi unaosababisha uwepo wa matokeo chanya yenye tija kwa kila mwananchi ndiyo unaotakiwa si tu kwa Tanzania, bali kwa bara la Afrika kwa jumla.
Hata hivyo, rais wa nchi pekee hawezi kufanya kazi yenye kutoa matokeo yanayotarajiwa kama viongozi na watendaji walio chini yake hawatakuwa ni wachapakazi wanaoimba wimbo mmoja wa maendeleo.
Tanzania kama silivyo nchi nyingine za Afrika, watu wake wanachotaka kuona ni unafuu wa maisha katika leo yao wakiilinganisha na jana yao.




