Na MWANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amekabidhiwa tuzo tatu kuu za utalii wa kimataifa, ambazo Tanzania imeshinda katika tuzo za Shirika la Utalii Duniani (WTA 2025), maarufu ‘World Travel Awards 2025’.
Tuzo hizo zilikabidhiwa kwa Rais na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji, kwa niaba ya wadau wa utalii katika hafla iliyofanyika, Ikulu ya Tunguu, Zanzibar.
Miongoni mwa tuzo hizo ni Tuzo ya Nchi Inayoongoza Duniani kwa Utalii wa Safari yaani ‘World’s Leading Safari Destination’, iliyotolewa katika kilele cha utoaji tuzo za utalii duniani zilizofanyika nchini Bahrain, Desemba 6, mwaka jana.
Washiriki wengine katika kipengele hicho ni Botswana, Kenya, Namibia, Afrika Kusini, Uganda, Zambia na Zimbabwe.
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ilitajwa kuwa hifadhi bora duniani kwa mwaka 2025, ikizitangulia hifadhi za Kruger ya Afrika Kusini na Yellowstone ya Marekani.
Tanzania pia ilishinda kuwa nchi inayoongoza kwa kutembelewa na watalii barani Afrika kwa mwaka jana wakati wa hafla ya kutunuku Tuzo za Dunia za Safari Afrika na Bahari ya Hindi, zilizofanyika Juni 28, 2025 jijini Dar es Salaam, ikishindanishwa na vivutio kadhaa vya juu vya utalii barani Afrika.
APONGEZA TAASISI ZA UTALII NCHINI
Rais Dk. Samia amezipongeza taasisi na wataalamu katika sekta ya utalii na uhifadhi kwa kulinda vivutio vya taifa na kuimarisha hadhi ya utalii wa kimataifa wa Tanzania.
Alisema mafanikio hayo yanaakisi upekee wa asili ya Tanzania, juhudi endelevu za uhifadhi na utangazaji wa kimkakati wa bidhaa za utalii.
Kwa mujibu wa Rais Dk. Samia, mafanikio hayo yanaakisi utajiri wa maliasili, wanyamapori, uhifadhi endelevu, vyanzo vya maji, na ukarimu wa wananchi wake wanaovutia wageni kutoka mataifa mbalimbali.
Tuzo hizo zinathibitisha nafasi ya Tanzania kuwa nchi inayoongoza duniani kwa utalii unaozingatia asili na kusisitiza dhamira ya serikali katika uhifadhi na ushindani endelevu wa kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Zanzibar imeshinda tuzo ya Eneo Bora Afrika kwa Mikutano na Matukio ya Kitaasisi.
Ubora wa Tanzania ulionekana tena baada ya kuibuka mshindi wa tuzo za ‘World Travel Awards’, ambapo Tanzania ilishinda jumla ya tuzo 45 katika Afrika, zikihusisha sekta za umma na binafsi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Pia, Tanzania ilipata tuzo mbili zaidi katika kundi la Sekta Binafsi, ikiwemo Kampuni Bora ya Safari za Puto Duniani, iliyotwaliwa na kampuni ya Serengeti Balloon Safaris na Kisiwa Bora cha Mapumziko Duniani na Jumaira Thanda Resort katika Kisiwa cha Mafia nchini Tanzania.
Tuzo za Wolrd Travel zilianzishwa 1993 zikiwa ni miongoni mwa tuzo zenye viwango vinavyoheshimika duniani katika sekta ya utalii.
Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), sekta hiyo ilipata ufanisi mkubwa ikiwa ni pamoja na ongezeko la asilimia 9.02 la watalii kwa mwaka na kufikia 2,097,823 na kuweka rekodi ya kukusanya mapato ya dola za Marekani bilioni 4.2 mwaka jana, ikilinganishwa na dola bilioni 1.3 mwaka 2021.




