Na FRED ALFRED, Dodoma
SERIKALI imezindua kituo cha kupoza umeme Mtera, chenye thamani ya sh. bilioni 9.7, kitakacho hudumia Mkoa wa Iringa na wilaya mbili mkoani Dodoma, ambazo zilikabiliwa na changamoto ya kukatika kwa umeme.
Akizungumza katika uzinduzi wa kituo hicho, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi alisema kuanza kazi kwa kituo hicho kutasaidia hali ya umeme kutengamaa katika mikoa ya Iringa na Wilaya za Kongwa na Mpwapwa, ambazo zilikabiliwa na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.
Alisema hiyo ilitokana na umbali mrefu wa kusambaza umeme katika maeneo hayo, kwani uliozalishwa Mtera ulisafirishwa hadi kituo cha kupozea umeme cha Zuzu, ambacho ni umbali wa kilometa 150 hali iliyosababisha kukatika au kukosa nguvu unapowafikia wananchi.
”Lakini sasa kuzinduliwa kwa kituo hiki kunamaanisha kuwa umeme utazalishwa na kupozwa hapa hapa, hivyo wananchi wa maeneo ya Iringa na Wilaya za Kongwa na Mpwapwa wataondokana na tatizo la kukatika kwa umeme, ambalo lilikwamisha viwanda vikubwa kufunguliwa kwenye wilaya hizo,” alisema Ndejembi.
Aliongeza kuwa :”Kuzinduliwa kwa kituo hicho ni juhudi za serikali kuhakikisha wananchi wanafikiwa na maendeleo ya kweli, kwa kupitia nishati ya umeme ikiwemo uwekezaji wa viwanda vikubwa na vidogo ambavyo vinahitaji umeme wa uhakika.”
Kwa mujibu wa Ndejembi, hadi sasa vijiji vyote nchini vimefikiwa na hivi karibuni watasaini mkataba wa kupeleka umeme katika vitongoji 9,009, katika kuhakikisha vijiji na vitongoji vyote vinafikiwa na nishati hiyo.
MRAMBA
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, alisema Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imefanya kazi kubwa ya kusambaza umeme vijijini.
Alisema lengo la kuimarisha huduma za umeme nchini ni kuhakikisha inakuwa ya uhakika, siyo ya kukatika ili wananchi wafanye shughuli zao za maendeleo bila bughudha
REA
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Hassan Saidy, alisema umeme unaopozwa katika kituo hicho ulishaanza kufanya kazi, kwa Mkoa wa Iringa kuhudumiwa na megawati tatu huku Mkoa wa Dodoma ukihudumiwa kwa megawati sita.
Alisema hali hiyo imepunguza muda wa wananchi kukosa umeme kutoka saa 18 kwa mwezi hadi kufikia dakika 40 kwa mwezi, hali inayowafanya wananchi kufanya shughuli zao za maendeleo kwa wakati.
RC DODOMA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema mkoa huo una ziada ya umeme kwani unaozalishwa ni megawati 200, huku matumizi ya mkoa yakiwa megawati 86 na hivyo, kuwa na ziada ambayo haitumiki.




