Na MWANDISHI WETU
BENKI ya NMB imeendelea kuchochea upatikanaji wa huduma za kifedha katika maeneo mbalimbali yakiwamo yenye changamoto, kwa kuongeza magari mahususi kwa maeneo hayo.
Uwepo wa magari hayo ambayo sasa yamefikia 15 ni fursa muhimu kwa kuwa hayatoi tu huduma za kifedha pekee, bali pia hutoa elimu ya kifedha, ufunguaji wa akaunti, huduma za mikopo, malipo na ushauri wa kibiashara kwa urahisi zaidi.
Akizungumza kabla ya uzinduzi rasmi wa magari mapya manane yanayotoa huduma za kifedha, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, amesema kuwa magari haya yamebuniwa mahsusi kutoa huduma rasmi za kifedha moja kwa moja kwa jamii zisizo na matawi ya kawaida, ikiwamo vijiji vya mbali, sokoni na maeneo ya biashara kama minada.
“Haya siyo magari tu, ni milango ya fursa. Yanawawezesha wakulima, wafanyabiashara wadogo, wafugaji na wajasiriamali wadogo kupata huduma za akiba, mikopo, malipo na ushauri bila usumbufu wa kusafiri umbali mrefu au gharama kubwa,” amefafanua.
Kupitia huduma hii, mfanyabiashara hatumii siku nzima kusafiri kuweka fedha benki, na mkulima haasubiri siku ya soko ijayo kufungua akaunti. Badala yake, benki inafika moja kwa moja pale alipo kumhudumia.
Zaipuna aliongeza kuwa, utaratibu huo unaonesha imani thabiti ya NMB kwamba ujumuishaji wa kifedha lazima uende kwa wananchi, hususan walioko kwenye sekta zisizo rasmi, ambao ndio msingi wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Huduma ya kibebki kupitia magari hayo pia inasaidia kutoa elimu ya kifedha na kuwajumuisha wananchi moja kwa moja katika mfumo rasmi wa kifedha.
Amesema huduma hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kutekeleza mkakati wa NMB wa ‘Village Banking’ ambao lengo lake kuu ni kizipeleka huduma za kifedha vijijini.
Pia, ameeleza kuwa mkakati huo ni moja ya nguzo za msingi za Ajenda 2030 ambayo inalenga kupanua wigo wa upatikanaji huduma za kifedha, kuhamasisha ujasiriamali na kuharakisha mabadiliko ya kijamii na kiuchumi nchini.
Uzinduzi wa magari hayo unaashiria jitihada za NMB kuimarisha ujumuishaji wa kifedha nchini na kutekeleza mkakati wake wa kupeleka huduma za benki karibu na wananchi, huku akitumia teknolojia na mbinu bunifu kufanikisha maendeleo ya kiuchumi vijijini na kwenye jamii zisizo rasmi.
Kutambulishwa kwake kulikuwa sehemu ya unzinduzi wa Ajenda 2030 uliofanyika juzi, ukiwa Mpango Mkakati wa Kati wa NMB kwa kipindi cha 2026–2030, unaolenga pamoja na mambo mengine kupanua ujumuishaji wa kifedha nchini na kuharakisha ukuaji wa kijamii na kiuchumi.
Uzinduzi huo ulisimamiwa na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, aliyeipongeza NMB kwa mchnago wake katika ujenzi wa taifa na kuboresha maisha ya Watazania kupitia masuluhisho bunifu na jumuishi.




