Na NASRA KITANA
WAKATI joto la pambano watani wa jadi, Yanga na Simba likizidi kupanda, makocha wa timu hizo wametambiana huku kila mmoja akisisitiza kuibuka na ushindi kutokana na ubora wa kikosi chake.
Yanga na Simba zinatarajiwa kushuka dimbani kesho katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Uwanja wa New Amaan, Complex, visiwani Zanzibar.
Yanga itaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mabao 5-0 mbele ya JKT Tanzania huku Simba ikitoka suluhu dhidi ya Dodoma Jiji.
Pia Yanga itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuifunga Simba mechi sita mfululizo za mashindano tofauti.
Mara ya mwisho Simba kuifunga Yanga ilikuwa katika Ngao ya Jamii iliyochezwa Agosti 13, 2023 kwa mikwaju ya penalti 3-1, baada ya hapo, Yanga imetembeza vipigo vinne katika Ligi na Ngao ya Jamii mara mbili.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, alisema kuwa kila mchezo kwake ni kama fainali, hivyo hatokubali kuona wanapoteza kwani wanahitaji pointi tatu muhimu na kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Alisema kuwa ni mechi nzuri dhidi ya Simba na kila mmoja anaisubiria kwa muda mrefu, lakini wao wamepata motisha kueleka mchezo huo kutokana na ushindi wa mabao 5-0 waliyopata dhidi ya JKT Tanzania.
“Kilichopo ni kufikiria namna ya kiwango cha timu, mpaka hivi sasa tunaendelea vizuri na maandalizi hata mabeki wetu wanajipanga vizuri kuzuia mashambulizi, ninafurahi sana kwani ninaamini tutaibuka na ushindi.
“Tangu nilipofika hapa visiwani Zanzibar, mashabiki wetu wamekuwa wakituunga mkono kila wakati na hata tunapotoka nje ya Dar es Salaam, tunapata ushirikiano wa kutosha.
“Tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kuhakikisha wanatupa sapoti ya kutosha ili tuweze kuwapa burudani ya aina yake,” alisema.
Hata hivvyo kocha huyo alisema kuwa hana hofu na wachezaji wake kwani wanaendelea kufanya marekebisho katika mapugufu yaliojitokeza katika mechi za awali ili kufanya vizuri zaidi katika mchezo huo.
Kwa upande wa Kocha wa Simba, Steve Barker alisema walikuwa wanahitaji kupata ushindi dhidi ya Dodoma Jiji lakini haikuwezekana, hivyo watapambana kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo.
Barker alisema kuwa hana hofu na kikosi alichokuwa nacho kwani kila mchezaji yupo vizuri na anamorari ya kutosha kuelekea katika mchezo huo muhimu.
Alisema kuwa anajua utakuwa mchezo mgumu na wenye changamoto kubwa huku ukifuatiliwa na mashabiki lukuki, watapambana kuhakikisha wanapata ushindi wa kishindo.
Alisisitiza wamejipanga kupata matokeo mazuri na kuendelea kusogea nafasi za juu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Kila mechi ina presha yake, tumejipanga kufanya vyema baada ya kuboresha kikosi chetu kutokana na mapungufu tuliyoyaona katika mchezo uliopita dhidi ya Dodoma Jiji.
“Tunahitaji kushinda mechi iliyopo mbele yetu kuhakikisha tunaendelea kujiweka katika mazingira mazuri ya kusogea juu ya msimamo.
“Itakuwa mechi ngumu, Yanga ina timu nzuri na sisi pia tuna timu nzuri, ni mechi kubwa hapa nchini na Afrika kwa ujumla, matumaini yetu ni kwamba mashabiki watafurahia burudani tutakayoitoa tukiwa uwanjani,” alisema.
WAAMUZI HADHARANI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), jana lilitangaza waamuzi wa mchezo huo ambapo mwamuzi wa kati atakuwa ni Nassoro Mwinchui kutoka Tanga, akisaidiana na Kassim Mpanga wa Dar es Salaam, Hamdan Said wa Mtwara na Ramadhani Kayoko wa Dar es Salaam.
REKODI ZA TIMU HIZO ZIPO HIVI
Rekodi zinaonyesha, Yanga imeifunga Simba mara sita mfululizo katika mashindano tofauti timu hizo zilipokutana Ligi Kuu Bara mechi nne na Ngao ya Jamii mara mbili.
Mara ya mwisho Simba kuifunga Yanga ilikuwa katika Ngao ya Jamii iliyochezwa Agosti 13, 2023 kwa penalti 3-1.
Baada ya hapo, matokeo ya Ligi Kuu Bara yalikuwa Simba 1-5 Yanga (Novemba 5, 2023), Yanga 2-1 Simba (Aprili 20, 2024), Simba 0-1 Yanga (Oktoba 19, 2024) na Yanga 2-0 Simba (Juni 25, 2025).
Pia mechi mbili za Ngao ya Jamii Yanga 1-0 Simba na Yanga 1-0 Simba.




