• ePaper
Wednesday, March 18, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home Habari

ALAMA TATU KUMUENZI JPM

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
March 17, 2026
in Habari, Kitaifa
0
ALAMA TATU KUMUENZI JPM
0
SHARES
4
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na WAANDISHI WETU

MAKAMU wa Rais, Dk. Emmanuel Nchimbi, ametaja mambo matatu makubwa ambayo Hayati Dk. John Magufuli, atakumbukwa nayo katika uongozi wake.

Akizungumza katika misa takatifu ya kumbukizi ya miaka mitano ya Hayati Dk. Magufuli iliyofanyika Wilaya ya Chato, mkoani Geita, Dk. Nchimbi, amesema uongozi wake umeacha alama kwa Watanzania.

Amesema Hayati Dk. Magufuli alikuwa kiongozi hodari mwenye kipaji cha uongozi na uwezo mkubwa wa kutenda kwa manufaa ya taifa na watu wake.

“Kila siku ya maisha yake alitoa funzo kwa kila mtu aliyefanya naye kazi, kimsingi maisha yake yalikuwa darasa zuri kwa sisi viongozi na kupitia uongozi wake aliweza kulea vijana wapya,”amesema.

Makamu wa Rais Nchimbi alisema siyo jambo rahisi kueleza ndani ya muda mfupi na ufasaha sifa na mema mengi aliyofanya Dk. Magufuli enzi za uhai wake, lakini atamkumbuka kwa mambo makubwa matatu.

“Mambo hayo tukiweza kuyashika tutaweza kumuenzi kwa vitendo. Jambo la kwanza kupitia yeye (Hayati Magufuli) tunajifunza kwa wito wa kila Mtanzania kujitoa na kufanya kazi kwa bidii.

“Hayati Dk. Magufuli alijitambulisha kwa falsafa yake ya Hapa Kazi Tu, alitaka kila mtu kujituma na kutoa mchango wake kwa taifa kwa njia ya kazi, aliamini hiyo ndiyo njia pekee ya kututoa katika umaskini kwenye ngazi ya mtu mmoja mmoja, kaya hadi taifa,”amesema Dk. Nchimbi.

Amesema Hayati Dk. Magufuli alihimiza kufanya kazi kwa weledi, bidii kwa kiwango cha juu iwe katika masomo, kazi za nyumbani, ofisini, kilimo, viwandani au utoaji huduma kwa jamii.

Jambo la pili, kupitia uongozi wake Watanzania wana funzo la kujifunza ujasiri na uthubutu wake katika kufanya uamuzi mgumu wenye manufaa kwa taifa.

“Alitufundisha umuhimu wa kuwajibika kusimamia misingi ya haki na usawa katika kuwahudumia wananchi wote,”amesema.

Makamu wa Rais Nchimbi alisema Hayati Dk. Magufuli hakuyumbishwa katika kupigana vita vya uzembe na wala rushwa.

“Jambo la tatu alitufundisha hatima ya Tanzania na Afrika kwa ujumla ipo mikononi mwetu wenyewe, alinukuliwa mara kadhaa akisema tuna utajiri mkubwa wa rasilimali ambazo tukizilinda na kuzitumia vizuri zitatutoa katika umaskini,”amesema.     

Dk. Nchimbi amesema Hayati Magufuli aliamini wajibu wa kutatua matatizo ya Tanzania ya kijamii, kisiasa na kiuchumi upo mikononi mwa Watanzania.

“Kwa kutambua na kuenzi mchango wa Hayati Dk. Magufuli, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amekuwa akifuatilia kwa karibu ujenzi wa makumbusho yake, na ametaarifiwa ujenzi huo ukamilike imepungua sh. milioni 100 na Rais ameamua kutoa fedha hizo kukamilisha kazi hiyo,”amesema Makamu wa Rais.

KAULI YA Dk. MWINYI 

Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, alisema Watanzania wanaendelea kumuenzi Hayati Magufuli kutokana na uongozi wake mahiri ulioacha alama muhimu.

Amesisitiza namna bora ya kumuenzi Hayati Dk. Magufuli, ni kuwajibika na kuwajali wananchi wanyonge.

“Makamu wa Rais, wageni waalikwa na ndugu wananchi, ni dhahiri namna bora ya kumuenzi na kumkumbuka Hayati Rais Magufuli, ni kuendeleza dhamira yake ya kuhimiza uwajibikaji na kuwajali wananchi, hasa wanyonge na kuhakikisha rasilimali za nchi zinalindwa kwa maslahi ya Watanzania wote.

“Hayati Rais Magufuli alikuwa muumini mkubwa wa Muungano wa Tanzania akihakikisha wananchi wa pande zote mbili wananufaika na muungano huo, kwa dhamira ileile ya waasisi wa taifa letu; Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na marehemu Mzee Abeid Amani Karume,”amesema Dk. Mwinyi.

WASIRA

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, alisema Hayati Dk. Magufuli amefanya mambo mengi ya maendeleo kwa Watanzania.

“Sifa ambayo Hayati Magufuli alikuwa nayo ni uwezo wa kuthubutu, kuna mambo ambayo wengine wasingeyaweza, yeye ndiyo aliyetekeleza uamuzi wa TANU wa mwaka 1954 kuyapeleka makao makuu Dodoma.

“Kila mtu ana karama yake, lakini Dk. Magufuli alikuwa na karama ya kuthubutu, wapo waliosema alikuwa mzalendo mimi ninakubaliana nao

“Ninatoa ushuhuda wa uzalendo wake madhumuni ya chama cha TANU na CCM yameandikwa, moja ni kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumika kuondoa umaskini, maradhi na ujinga,”alisema Wasira.

Alieleza Hayati Dk. Magufuli alipambana na wawekezaji wa madini ambao walikuwa wanatoa mrabaha wa asilimia tatu, akihakikisha serikali inamiliki asilimia 16 ya migodi mikubwa.

“Hicho ndicho kielelezo cha uzalendo, wengine wakipewa wanaanza kula ule mrahaba, lakini yeye alihakikisha nchi inapata faida kutokana na madini,” aliongeza Wasira.

Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Bara, Chama kinamkumbuka Dk. Magufuli kwa kufanya kazi kubwa katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015-2020.

DK. MPANGO

Makamu wa Rais mstaafu Dk. Philip Mpango, alisema anamkumbuka Hayati Dk. Magufuli, ni kiongozi aliyemtegemea Mungu katika kila jambo.

Alisema wakati akikabiliwa na maradhi ya mgongo, Hayati Dk. Magufuli alimpa kitabu cha Mawaridi, kumtafutia watawa wa kanisa katoliki pamoja na kumshirikisha Mama Janeth kumwombea apone maradhi hayo.

Pia alisema alipomteua kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na baadaye Waziri wa Fedha na Mipango, alimsisitizia nafasi hiyo amepewa na Mungu, hivyo awajibike katika kupandisha makusanyo ya kodi ya serikali.

Dk. Mpango alisema mambo yote aliyofanya kwa kushirikiana na uongozi wa Hayati Magufuli, ataendelea kuyakumbuka.

MAJALIWA

Waziri Mkuu Mstaafu, Kassim Majaliwa, alisema Hayati Dk. Magufuli alikuwa kiongozi mwenye uzalendo katika maisha yake.

“Leo hii tuko katika kumbukizi hii, hatuwezi kujitenga na sifa hizi, alikuwa kiongozi mzalendo na uzalendo unajengwa na uaminifu, uwajibikaji na kupenda maendeleo,”alisema.

Majaliwa alimkumbuka Hayati Dk. Magufuli, kwa tabia yake ya kuwa mkweli, kutokuwa na mzaha katika mambo yake kwa kukemea vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.

Alisema Hayati Dk. Magufuli alikuwa mwalimu kwa viongozi aliowaongoza akiwemo yeye, Rais wa Zanzibar Dk. Mwinyi na Rais Dk. Samia, wakati huo akiwa Makamu wake wa Rais.

Alifafanua kwa kuwa alikuwa mwalimu mzuri, alimwezesha Rais Dk. Samia kutekeleza miradi yote ya kimkakati aliyoacha.

Majaliwa alisema kutokana na umahiri wake wa uongozi, Watanzania wameguswa kwa kumpoteza, lakini bado yuko katika mioyo yao.

PINDA

Naye Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, alisema wananchi wanapaswa kuiga pamoja na kuthamini mambo ya kiroho aliyokuwa akiyaamini Dk. Magufuli.

JAJI MKUU

Jaji Mkuu George Masaju, alisema alimfahamu Hayati Magufuli alipokuwa akisoma Chuo Kikuu Dar es Saalam (UDSM), alipokwenda kusoma shahada ya pili, yeye akisoma shahada ya kwanza.

“Tulikuwa tunakaa Hall 4 tulipofahamiana hatukuwa marafiki sana, lakini nilipokuwa namaliza masomo yangu alijitolea kunipeleka nyumbani na gari lake,”alisema.

Jaji Masaju alisema mwaka 2015, Dk. Magufuli alimteua kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali akimpandisha kutoka nafasi ya Naibu Mwanasheria wa Serikali.

“Aliniteua kwasababu alikuwa ananifahamu tunaweza kumsaidia kazi, aliniteua kwa miaka miwili kabla ya kuniteua kuwa jaji wa mahakama kuu,”alibainisha.

“Dk. Magufuli alikuwa na huruma, nikiwa mwanasheria mkuu wa serikali baada ya baba yangu kufariki dunia kule usukumani, aliniambia atanisaidia kujenga kama kumbukumbu ya baba, kwangu ilinigusa sana,”alisema.

“Baada ya kuchelewa kuunda Baraza la Mawaziri kulikuwa na Kamisheni Polisi tulikuwa tumekaa na Janeth Magufuli, akaniambia shemeji naomba mshauri sana ndugu yako muwe mnapumzika mtaumia,” alisema jaji mkuu. 

Alisema Hayati Dk. Magufuli alikuwa mchapakazi kiasi cha kuleta matokeo makubwa.

NAIBU SPIKA

Naibu Spika, Daniel Sillo, alisema Hayati Dk. Magufuli, alikuwa kiongozi mwenye maono makubwa kwa Tanzania, uthubutu na ujasiri.

“Dk. Magufuli aliasisi miradi mikubwa ambayo katika hali ya kawaida siyo rahisi kutekeleza, ikiwemo mradi wa SGR, Bwawa la Nyerere, Daraja la Busisi na miradi mingine mingi.

“Pamoja na kutoa maelekezo kwa watendaji wa serikali, pia alikuwa akiwashirikisha viongozi katika hatua mbalimbali ya miradi hiyo, ndiyo maana baada ya yeye kuondoka, Rais Dk. Samia amekamilisha na ameanza kutekeleza miradi mipya ya kimkakati,”alisema.

MABEYO

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo, alisema Hayati Dk. Magufuli aliwafundisha mambo mengi na hadi sasa watu wanayaishi.

“Tunaendelea kumuenzi na kumwombea kwa Mungu aendelee kumpa pumziko la milele mbinguni,”alisema Mabeyo.

Alisema ana imani Hayati Magufuli alipo anaiombea Tanzania katika maendeleo ambayo aliyaanzisha na yale aliyokuwa akiyatarajia kufanya.

Dk. KIPILIMBA

Mkurugenzi Mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk. Destus Kipilimba, alisema amefanya kazi na Hayati Dk. Magufuli na alijifunza mambo mengi kutoka kwake.

“Katika jambo moja ambalo sitasahau alikuwa mfanyakazi asiyechoka usiku na mchana anafanya kazi, kwasababu hiyo alikuwa anatuhamasisha wote tulikuwa hatulali tunategemea simu saa tisa usiku atakupigia,” alisema.

Dk. Kipilimba alisema ana furaha kuona kazi alizofanya zilileta matokeo na mafanikio na hatasahaulika kwa kuwa alikuwa rafiki, kiongozi na mfano wa kuigwa.

DK. BITEKO

Naibu Waziri Mkuu Mstaafu, Dk. Doto Biteko, alisema Hayati Magufuli bado anaishi kwenye mioyo ya Watanzania, ingawa hayupo duniani.

“Hii haikutokea kwa bahati mbaya ni kwasababu alifanya kazi nzuri na haliwapenda Watanzania, kazi ambayo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameiendeleza kwa kasi kubwa, hasa kwa miradi ambayo aliianzisha,” alisema Dk. Biteko ambaye hivi sasa ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe.

MAMA JANETH

Kwa upande wake Mama Janeth alimshukuru Rais Dk. Samia, kuendelea kutoa mchango wake katika kumbukizi za Hayati Dk. Magufuli.

Pia, aliwashukuru viongozi na watu waliohudhuria kumbukizi ya kiongozi huyo.

JESCA MAGUFULI

Jesca Magufuli, ambaye ni mtoto wa Dk. Magufuli, alisema familia inamshukuru Rais Samia kwa ushirikiano aliowapa baada ya baba yao kufariki dunia.

“Kwa taifa Dk. Magufuli anakumbukwa kama kiongozi ambaye dhamira yake kwa Watanzania, hakuwahi kuyumba wengi walimtambua baba yangu kama Rais, waziri na mbunge, lakini kwetu alikuwa mtu mwenye nidhamu, unyenyekevu na imani thabiti kwa Mungu,” alisema.

Alisema mara kwa mara aliwaasa hakuna mafanikio bila kufanya kazi na mara nyingi alikuwa akisema kama wanataka heshima katika maisha wafanye kazi.

“Kwake Tanzania haikuwa eneo la kijiografia, bali ilikuwa dhamana ya kizazi kilichopo, hivyo ni jukumu letu sote kulinda na kuijenga kwa vizazi vijavyo,” aliongeza Jesca, ambaye ni mbunge wa viti maalumu.

Alisema moja ya mafunzo makubwa aliyowapa kama watoto wake ilikuwa ni somo la unyenyekevu.

“Licha ya nafasi aliyokuwa nayo hakuwahi kujitenga na wananchi wa kawaida aliwasikiliza walimu, wakulima, wafanyakazi, vijana na watu wenye mahitaji maalumu na kuchukua hatua,” alisema.

Aidha, Jesca alimkabidhi Dk. Nchimbi risiti ya malipo ya sh. milioni 50 ukiwa ni mchango wa Rais Samia kwenye ujenzi wa kanisa.

ASKOFU

Akitoa salamu kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu wa Jimbo Katoliki Geita, Mhashamu Flaviana Kassala, alitoa shukrani kwa familia na kuikumbusha kufanya ibada ya baba yao.

“Hii inaonyesha wazi familia ambavyo inaamini na kupenda kuungana na wapendwa wetu waliotangulia azimisho liwe kubwa la tumaini lao,” alieleza Askofu Kassala.

Dk. Magufuli alifariki dunia Machi 17, 2021 kutokana na maradhi ya moyo.

Previous Post

SERIKALI KUIFANYA TANZANIA KITOVU CHA BIASHARA – DK. YONAZI

Next Post

MWIGULU AWAWEKA MTEGONI VIGOGO WILAYA, HALMASHAURI

Next Post
MWIGULU AWAWEKA MTEGONI VIGOGO WILAYA, HALMASHAURI

MWIGULU AWAWEKA MTEGONI VIGOGO WILAYA, HALMASHAURI

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

HADHI YA TANZANIA KIMATAIFA ILINDWE KWA GHARAMA ZOZOTE

HADHI YA TANZANIA KIMATAIFA ILINDWE KWA GHARAMA ZOZOTE

3 months ago
DK. NCHIMBI ATOA AGIZO KWA PROF. MKENDA

DK. NCHIMBI ATOA AGIZO KWA PROF. MKENDA

3 months ago

Popular News

  • MANDONGA AJA KIVINGINE

    MANDONGA AJA KIVINGINE

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • SERIKALI YATUMIA BILIONI 64/- KUBORESHA UWANJA WA NDEGE IRINGA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • MWIGULU AWAWEKA MTEGONI VIGOGO WILAYA, HALMASHAURI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • ALAMA TATU KUMUENZI JPM

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • SERIKALI KUIFANYA TANZANIA KITOVU CHA BIASHARA – DK. YONAZI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?