Na IRENE MWASOMOLA
Ni ziara ya kiuchumi, hivi ndivyo unavyoweza kuuelezea ujio wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, ambapo kupitia ziara hiyo amekutana na kuzungumza na mwenyeji wake Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na kukubaliana kushirikiana katika maeneo saba.
Baadhi ya maeneo hayo ni kuendeleza ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (ECOP), bomba la kusafirisha gesi kutoka Tanzania kwenda Uganda, bomba la kusafirisha mafuta safi kutoka Uganda kuja Tanzania, ujenzi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) kutoka Isaka hadi Murongo nchini Uganda na kutumia bandari za Tanga na Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam, baada ya kukutana kwa mazungumzo na Museveni, Rais Dk. Samia alisema baada ya kusafirisha mafuta kupitia ECOP kuanzia Julai mwaka huu, meli ya kwanza itatoka Tanga kupeleka mafuta katika maeneo yatakayokusudiwa.
Rais Samia akizungumza katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Museveni, alisema katika mkutano wao walizungumza kuhusu ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi litakaloitoa Tanzania kwenda Uganda na bomba la kusafirisha mafuta safi kutoka Uganda kuja Tanzania.
“Tumezungumzia mabomba mawili mengine, kuna bomba la gesi litakalotoa gesi Tanzania kupeleka Uganda na la mafuta safi ambayo yatakuwa yamesafishwa Uganda yatakwenda katika nchi yatakayouzwa, tutatumia ushoroba huo huo kusafirisha hadi Tanga na kutafuta safari yanakopelekwa,” alisema.
UGANDA KUTUMIA BANDARI
Aidha, Rais Dk. Samia alisema wamezungumza na Rais Museveni kuhusu namna nchi hiyo itakavyopata nafasi kutumia bandari za Tanga na Dar es Salaam, kusafirisha mizigo.
Pia, alisema wamezungumza kuhusu ujenzi wa reli ya SGR, ambapo ameiomba serikali ya Uganda kuiunganisha kutoka kipande cha Isaka (mkoani Shinyanga) hadi Murongo nchini Uganda.
Alifafanua kuwa reli hiyo ilikusudiwa kwenda nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hivyo sasa itakwenda hadi Uganda kwa lengo la kurahisisha usafirishaji wa bidhaa.
“Tumezungumza reli ya SGR ambayo tunaipeleka Isaka tumeomba serikali ya Uganda kuunga hapo kuelekea Murongo, hilo ni ombi letu tumewapa,” alisema.
Mbali na hilo, Rais Dk. Samia alisema serikali ina nia ya kujenga reli itakayounganisha Tanga hadi Musoma, ambapo baada ya kufika Musoma itasafirisha bidhaa kwenda Uganda, kupitia Ziwa Victoria.
MELI YA MV NEW MWANZA
Rais Dk. Samia alisema pia wamezungumza kuhusu meli ya MV New Mwanza ambayo itatoa huduma hadi Uganda, hatua ambayo itaendelea kuchochea ukuaji wa biashara na uchumi.
Vilevile wamekubaliana kuondoa vikwazo vya kibiashara baina ya nchi hizo.
Kwa mujibu wa Rais Samia, vikwazo hivyo vikiondolewa itasaidia nchi hizo kukuza soko la Afrika Mashariki.
Halikadhalika, Rais Samia alisema biashara baina ya Uganda na Tanzania imekua, ingawa kuna vikwazo ambavyo serikali zao zimejipanga kuviondoa, kwa lengo la kukuza zaidi uchumi.
NISHATI
Pia, alisema wamezungumza kuhusu utengenezaji wa miradi midogo midogo itakayozalisha nishati kwa matumizi ya nchi hizo.
Rais Dk. Samia alisema katika ngazi za kimataifa Tanzania na Uganda zinafanya kazi kwa ukaribu na kwamba Uganda imeaichia Tanzania nafasi ya kuwania kiti cha ujumbe katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN), ambacho nchi hiyo nayo ilikuwa inakiwania.
Alifafanua kuwa nchi zote mbili zilikuwa zinagombea nafasi hiyo ambayo uchaguzi wake utafanyika mwaka 2027.
“Mwakani Tanzania na Uganda tulikuwa tunagombania kiti cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini nilipomuomba akasema mimi (Uganda) najitoa Tanzania endelea,” alisema.
Aidha, Rais Dk. Samia alisema Tanzania nayo itaipa ushirikiano Uganda katika nafasi nyingine inayogombea ya uwakilishi wa kiti cha Baraza la Usalama la Afrika.
Rais Samia aliongeza kuwa Rais Museveni ni Mwenyekiti wa Nchi za Maziwa Makuu, Tanzania imeahidi kumpa ushirikiano na kumuunga mkono katika mkakati wake wa kuanza mazungumzo ya kuleta amani.
Alimshukuru Rais Museveni kwa kufanya ziara nchini, ikiwa muda mfupi tangu amalize uchaguzi mkuu, hatua ambayo inaonesha anatoa umuhimu mkubwa kwa ajenda za ushirikiano baina ya Uganda na Tanzania.
MUSEVENI
Kwa upande wake, Rais Museveni alisema amefurahi kufanya ziara nchini na kwamba serikali ya Uganda itaendelea kushirikiana na Tanzania.
Alisema katika mazungumzo yake na Rais Samia walizungumzia nia ya nchi za Afrika kupata ukombozi.
Rais Museveni alitaja malengo matatu muhimu ambayo yaliwekwa na nchi za Afrika ambayo ni kupata uhuru, kuwa na maisha bora na kujihami kwa Afrika.
“Maisha bora kwa enzi hizi ni kuzalisha mali, bidhaa au huduma na kuuza na ukishazalisha mali, lazima upate mtu wa kununua kutoka kwako na ukipata watu wanaonunua ndiko kukua,” alifafanua.
HALI YA BIASHARA
Mauzo ya Tanzania kwenda Uganda mwaka 2025 yalifikia dola za Marekani milioni 134.7, huku uagizaji kutoka Uganda ukiwa dola milioni 88.2.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, mradi wa bomba la ECOP, hadi Januari mwaka huu ulifikia asilimia 79 na unatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu.




