Na NASRA KITANA
TIMU za soka za Singida Black Stars na Yanga, leo zinashuka dimbani kuchuana katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mchezo huo wa 12 kwa timu hizo unatarajiwa kupigwa saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Airtel uliopo Singida.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves amesema timu yake ipo vizuri kuwania pointi tatu.
Pedro alisema anajua wachezaji wake wanajua umuhimu wa kucheza kwa kujituma, licha ya mechi kuwa ngumu watahakikisha wanapata ushindi.
“Hakuna jambo muhimu kuliko alama tatu, ili upate alama tatu dhidi ya timu kama Singida unahitaji ufanye kazi ya ziada, kuwa makini dakika zote 90 na kuwa na utimamu wa kimwili ili kukabiliana na kasi ya mchezo, ili tushinde hii mechi lazima tuoneshe njaa ya kutaka alama tatu.
“Nikiri tunapitia changamoto kadhaa ikiwemo baadhi ya wachezaji muhimu kupata majeraha, kwa bahati mbaya Dickson Job naye ameongezeka katika idadi ya wachezaji ambao wanakabiliwa na majeraha, mtumaini yetu ni kuwa majeraha hayo siyo makubwa sana, unapokosa wachezaji wako muhimu ni wazi lazima kuna kitu kitapungua katika ufanisi wa timu,” alisema Pedro.
Naye mchezaji wa Yanga, Abubakar Nizar Othman ‘Ninju’, alisema Singida ni timu nzuri lakini amekiandaa kikosi chake kupata pointi tatu.
Alisema timu bora siku zote inatengenezwa na mwalimu na wachezaji kuwa na utayari wa kupokea maelekezo na kuyafanyia kazi.
“Mpira wa miguu ni mchezo ambao hubadilika kulingana na mazingira na wapinzani unaokutana nao, Yanga ni timu kubwa ambayo ina wajibu wa kusaka alama tatu lakini pia kutoa burudani kwa mashabiki. Hatuwezi kuwa bora katika kila nyakati, kuna nyakati tutapata alama tatu lakini katika mazingira magumu, katika mchezo huu tutamkabili mpinzani kwa namna atakavyokuja,” alisema Ninju.
Naye Kocha wa Singida BS, Othmen Najjar, alikiri wanakwenda kucheza na timu yenye wachezaji wengi wazuri lakini hawatakubali kupoteza.
“Kwa mechi kama hii, kisaikolojia kila mmoja hujiandaa vizuri kwa sababu ni mchezo muhimu na wanapaswa kucheza katika kiwango cha juu kabisa, kama tulivyofanya katika michezo mingine.
“Tunaelewa huu utakuwa mchezo mkubwa, kila mmoja husubiri aina hii ya mechi dhidi ya timu kubwa kama Yanga, ambao ni vinara wa ligi na wameshinda mataji mengi katika misimu iliyopita,” alisema Najjar.
Naye mchezaji wa timu hiyo, Kennedy Juma, alisema kila mchezaji amejiandaa vizuri kushindana kwa kiwango cha juu na kutumia kila nafasi watakayoipata kuvuna pointi tatu.
“Tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kutushangilia kwa nguvu. Tutawapa burudani. Hizi ni alama tatu muhimu katika uwanja wetu wa nyumbani,” alisema.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Yanga inashika nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 29 huku Singida Black Stars ikishika nafasi ya tisa na kujizolea pointi 19 baada ya wote kushuka dimbani mara 11.




