Na JOE NAKAJUMO
KATIKA miji kuna masoko ambako watu wanakwenda kupata bidhaa wanazozihitaji kwa matumizi. Kuna aina mbalimbali za masoko.
Yapo masoko ya bidhaa mchanganyiko zikiwemo nafaka, mboga mboga,nyama,samaki,kuku,viazi mbatata na vitamu,vitunguu, nyanya,matunda, nguo,vipodozi na kadhalika.
Lakini, kuna masoko maalumu ya bidhaa moja kwa mfano samaki, nyama,mbogamboga na matunda.
Jambo la msingi kwa aina yoyote ya soko, usafi ni suala la kupewa umuhimu wa pekee.
Hapa Tanzania, serikali imejitahidi na inaendelea kujenga masoko ya kisasa na kukarabati ya zamani kwa kuboresha miundombinu.
Baadhi ya miji yenye masoko ya kisasa ni Dar es Salaam, ambapo kuna soko la Kisutu, Magomeni, Kibada, Tandale, Mbagala Zakhem.
KARIAKOO KIMATAIFA
Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, lina sura ya pekee ya kimataifa. Soko hili liliungua moto Julai 10,mwaka 2021 na limefanyiwa ukarabati.
Pembezoni kulikuwa na soko dogo, ambalo lilivunjwa na kujengwa upya. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alizindua Soko la Kariakoo Februari 8, mwaka huu. Mradi huo uligharimu sh.bilioni 28.
Katika jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya serikali na Chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM), yamejengwa masoko mapya ya kisasa.
Moja limepewa jina la ‘Soko la Ndugai’ kwa heshima ya aliyekuwa Mbunge wa Kongwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, marehemu Job Ndugai.
Ingawa jina la soko lilikuwepo tangu akiwa Spika siku nyingi kabla ya umauti haujamkuta. Soko lingine Dodoma ni ‘Machinga Complex,’
Ndani ya manispaa ya Morogoro kuna soko jipya la kisasa na katika jiji la Mwanza, ujenzi wa soko kuu jipya ulikuwa unaendelea. Hii ni mifano michache ya masoko ya kisasa yanayojengwa katika miji mbalimbali.
Hivi karibuni, Waziri Mkuu,Dk. Mwigulu Nchemba alikuwa katika ziara mkoani Arusha. Moja ya shughuli zake ilikuwa ni kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa soko la Kilombero ambalo litalogharimu sh. bilioni 9.50.
Akiwa ziarani mkoani Kigoma, mwishoni mwa mwezi uliopita, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Kenani Kihongosi, alizungumzia mradi wa soko la Mwanga na Katonga, unaogharimu sh. bilioni 16.5 unaotarajiwa kukamilika Aprili 26,mwaka huu.
Rais Dk. Samia akifungua Soko la Kariakoo, aliagiza bidhaa zote zitakazouzwa katika Soko Kuu la Kariakoo, zizingatie viwango vya kitaifa na kimataifa, kulifanya soko liaminike ndani na nje ya nchi.
Dk. Samia aliagiza soko lisimamiwe kwa misingi ya nidhamu, uwazi wa mapato na matumizi ya mifumo ya kisasa, liwe kitovu cha biashara kimataifa na kusisitiza kuwa Soko la Kariakoo ni mali ya Watanzania wote.
VYUMBA KULELEA WATOTO
Mkuu wa nchi aliuagiza uongozi wa soko kutenga vyumba maalumu, vya kulelea watoto kwa mama wafanyabiashara kwa kuwa huduma ya kunyonyesha lazima iendane na mazingira salama ya malezi ya mtoto.
Ni jambo la kutia moyo kwamba siku chache baada ya agizo la Rais, uongozi wa Soko la Kariakoo, tayari umetenga eneo la kulelea watoto na linajenga miundombinu.
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, imeanza kutekeleza mradi wa kimkakati wa uanzishaji vituo vya kulelea watoto wadogo mchana maeneo ya masoko. Hatua hii ni kuwawezesha wazazi na walezi wenye watoto wadogo kuendelea na biashara bila kikwazo chochote.
Maeneo yaliyopangwa kuanza mradi huu ni pamoja na masoko ya Mbagala Zakhem, Magomeni na Kibada, mkoani Dar es Salaam. Mkoani Dodoma, mradi utatekelezwa katika Soko la Machinga Complex, Soko la Kibaigwa (Kongwa) na Soko la Buigiri (Chamwino).
WATOTO UVUNGUNI
Tathmini iliyofanywa, inaonesha watoto wengi wa wafanyabiashara katika masoko makubwa kama Kariakoo na Mbagala hulazimika kulelewa katika mazingira yasiyo rasmi, ikiwemo kuwekwa chini ya meza za biashara wakati wazazi wakiendelea na shughuli za ujasiriamali.
Akizungumza na wananchi alipoweka jiwe la msingi la Soko la Kilombero, Waziri Mkuu Dk. Mwigulu, aliagiza kufungwa mifumo ya kidijitai katika masoko yote nchini na kutunza kumbukumbu sahihi za wafanyabiashara.
TEHAMA SOKONI
“Masoko yote nchini kuanzia hivi sasa,yafungwe mifumo ya TEHAMA ya kidijitali, ambayo itaimarisha uwazi, uwajibikaji na ulinzi wa raslimali za umma,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Dk. Mwigulu alisema, mfumo wa kidijitali hauhitaji mtu wa kati, hivyo utaondoa mianya ya udanganyifu katika upangaji na umiliki wa vibanda.
Alitoa onyo kali kwa baadhi ya watumishi wa umma, kumiliki baadhi ya vizimba kwa bei ya sh.100,999, kisha kuvipangisha kwa wafanyabiashara wengine hadi sh. milioni 1.5 kwa mwezi.
Waziri Mkuu alisema hatarajii kuwakuta watumishi wa umma wameshikilia vizimba na kutaka ifanyike sensa ya wafanyabiashara. Lengo la serikali ni kuwawezesha wafanyabiashara wa kweli kuinua uchumi.
USAFI ENDELEVU
Amewahimiza wafanyabiashara kuhakikisha usafi wa soko, unadumishwa kuunda mazingira mazuri ya biashara.
Kila soko linapaswa kuwa na mifereji ya maji safi, meza zenye mpangilio mzuri na maboksi nadhifu kuepuka magonjwa na kuhifadhi mali za wananchi,aliongeza Dk. Mwigulu.
Katika hotuba yake kwa wananchi, Waziri Mkuu, alidokeza kuwa serikali imepanga kuongeza asilimia tano fedha za miundombinu ya masoko katika mwaka ujao wa fedha, kujenga masoko ya kisasa na kuboresha mazingira ya wafanyabiashara wadogo.
WATUMISHI NA VIZIMBA
Miaka michache iliyopita, Rais wa serikali ya awamu ya tano, Hayati Dk. John Magufuli aliwaumbua watumishi wa umma, siku ya ufunguzi wa soko la kisasa katika manispaa ya Morogoro.
Alibaini watumishi wa umma kugawana vizimba katika soko jipya na kisha kuwakodisha wengine kwa bei ya ‘kuruka’ kwa maana bei ya juu sana kuliko viwango halali vilivyowekwa.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi, Kenani Kihongosi, alitoa onyo kwa viongozi wa Halmashauri ya Kigoma/Ujiji kuhusu usimamizi na upangaji wa wafanyabiashara katika soko jipya la Mwanga na Katonga.
Alielekeza soko hilo litakalobeba wafanyabiashara 4,000, lisimamiwe kwa umakini mkubwa kuhakikisha linawanufaisha walengwa halisi. Ametaka upangaji vizimba kufanyika kwa haki, uwazi na kwa kuzingatia orodha ya wafanyabiashara waliokuwepo kabla ya ujenzi kuanza.
Haitakubalika kuona wafanyabiashara waliopisha mradi wakiachwa nje, huku nafasi zao zikichukuliwa na watu wengine wasiokuwa na sifa stahiki.
Lengo la soko la Mwanga na Katonga ni kuinua uchumi wa wananchi wa Kigoma kwa kuwapatia mazingira bora ya kufanyia biashara, alisisitiza Kihongosi katika mkutano wake hadhara mbele ya umati wa wananchi.
SOKO LA KWASAKWASA
Mkuu wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni amesema haridhishwi na hali ya usafi katika soko la mjini Same ‘Soko la Kwasakwasa’. Katika ziara yake ya kushtukiza sokoni hapo, Mkuu wa Wilaya aliona kuwa soko ni chafu na linaweza kuhatarisha afya za wafanyaviashara na wananchi.
Kasilda ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Same na Mamlaka ya Mji Mdogo Same, kuboresha usafi katika soko na kuweka taa kuruhusu biashara kufanyika hadi saa nne usiku. Kukosekana kwa taa kumechangia kuwepo vitendo viovu, ukiwemo wizi wa bidhaa na vitendo vya uvunjifu maadili kwa jamii.
TANDALE MURUA
Mwenyekiti wa Soko la Tandale, Dar es Salaam, Sultan Kiyungo, alisema ujenzi wa soko umewasaidia kukuza uchumi wa wafanyabiashara.
Ubora wa soko umewasaidia wafanyabiashara kuuza bidhaa nzuri zenye ubora kwa bei ya faida, tofauti ilivyokuwa katika soko la zamani.
Soko la Tandale lina uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 1,000. Ujenzi wake ulianza mwaka 2019 na kukamilika mwaka jana 2025 kwa gharama ya sh. bilioni 10.
Baadhi ya wafanyabiashara wamenukuliwa wakisema siku hizi hawana shida tena, hata mvua ikinyesha, bidhaa zao zipo salama.
Kauli hii ya Tandale kuhusu mazingira mazuri ya kufanyia biashara ni kinyume kabisa na mazingira yaliyopo katika Soko la Ilala, ambalo ni tegemeo kubwa kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake.
TOPE ILALA SOKONI
Soko la Ilala ni chafu,linaelea katika tope na maji machafu katika barabara za mitaa ya kuingia sokoni.
Mitaa inayoingia eneo la soko ni Utete, Moshi, Bukoba, Nzasa, Kigoma, Tabora, Morogoro na sehemu ya barabara ya Uhuru kutazamana na Ofisi ya Makao Makuu ya CCM, Wilaya ya Ilala.
Hali katika mitaa hii ni hatarishi, hasa wakati huu ambapo mvua zinaendelea. Siyo ajabu ukatokea mlipuko wa magonjwa kikiwemo kipindupindu.
Katika kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika, Disemba 9 mwaka 2024, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alitangaza mikakati itakayodumisha usafi katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Aliitaja mikakati ni kufanyika operesheni ya kuwapanga wafanyabiashara wadogo ’machinga’ katika maeneo rasmi na kuwaondoa sehemu walizokatazwa.
Mkakati mwingine ni kuanzisha mashindano ya usafi katika masoko kila baada ya miezi mitatu, kuimarisha kampeni ya upandaji miti na kufanya usafi katika fukwe za Bahari ya Hindi kwa nia ya kutunza mazingira.
Mpogolo alisema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambayo ni sura ya mkoa wa Dar es Salaam, ina mikakati mbalimbali ya usafi itakayotekelezwa kikamilifu.
Kwa sasa Mpogolo anakagua eneo la Kariakoo usiku na mchana kuhakikisha barabara zote zinazoingia katika Soko Kuu la Kariakoo zinapitika wakati wote.
Ni juhudi chanya zinazofanywa na Mpogolo, lakini ingefaa pia atupie jicho hali ya usafi katika Soko la Ilala, kwani mazingira yake ni hatarishi kwa wafanyabiashra na wateja wanaokwenda soko hilo.
DK. MPANGO
Juni Mosi mwaka 2024, aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, alizindua kampeni ya wiki ya usafi katika Soko la Ilala. Katika uzinduzi huo alitoa maagizo kadhaa ya kufanyiwa kazi.
Alisema mji usipokuwa msafi unaweza kuwa chanzo cha milipuko ya magonjwa kama kipindupindu, pale mvua zinaponyesha na kuwa usafi lazima uwe endelevu.
“Kuna adha kama hii, ukifika hapa harufu hii mbaya ilinipokea, nani anapenda hivi, kwa hiyo lazima tusafishe miji yetu iwe endelevu,” alisisitiza.
Makamu wa Rais ambaye sasa ni mstaafu tangu Novemba mwaka jana, baada ya serikali mpya kuundwa kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29.
Kauli hizi za Makamu wa Rais mstaafu Dk. Mpango na Waziri Mkuu,Dk. Mwigulu kuhusu usafi katika masoko na maeneo mengine zinafaa zifanyiwe kazi hata ikibidi kulifunga Soko la Ilala kwa muda.
Mwishoni mwa mwaka 2023, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Albert Chalamila,alisema masoko yasiyofanyiwa usafi atayafunga kwa muda wa siku tatu, iwe fundisho kwa wafanyabiashara na watendaji kufanya usafi bila kushurutishwa.
Siku za nyuma wakati wa awamu ya serikali ya kwanza, miaka ya 1970 hadi 1980, masoko yote yalikuwa yanafungwa saa nane mchana siku za Jumapili kupisha kufanyika usafi. (Mawasiliano na Mwandishi WhatsApp 0784291434;email nakajumoj@gmail.co m).




